Tatizo la uhaba wa ajira ni kubwa kiasi gani Tanzania?

    • Author, Na Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania

Moja kati ya mambo yanayotofautisha nchi tajiri na zile masikini ni ajira. Katika nchi mfano zile za Ulaya, watu ni wachache na ajira ni nyingi. Kwa lugha nyingine, kuna kazi zinazokosa watu wa kufanya.

Na kwa sababu hiyo nchi hizo kuanzisha programu za kuchukua wahamiaji kutoka mataifa masikini, ama wakimbizi na watafuta hifadhi kutoka maeneo yenye migogoro na vita, kwenda kuziba hilo pengo la uhaba wa rasilimali watu.

Lakini katika mataifa masikini hasa barani Afrika, watu ni wengi na kazi ama ajira ni chache. Afrika ndilo bara lenye vijana wengi kuliko bara lolote. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 70 ya wakaazi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wako chini ya umri wa miaka 30.

Nchi za Ulaya na zile za Asia ndizo zinaongoza kuwa na idadi kubwa ya wazee. Mfano, asilimia 12 ya idadi jumla ya watu wa China ni wenye umri wa miaka 65 na kwenda juu. Hali ni tofauti katika nchi kama Nigeria ambayo wazee ni asilimia 3 tu.

Nchi zinapokuwa na vijana wengi, maanake wengi wao hutaka kufanya kazi ili kujenga maisha yao. Neema ya Afrika kuwa na vijana wengi imekuja na gharama ya ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana hao.

Ukubwa wa tatizo nchini Tanzania

Akikiri uwepo wa tatizo la ajira Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba Januari 07, 2022 alieleza, “serikali yenu, tunajua tatizo la ajira na tutajitahidi kutengeneza fursa mbalimbali ili vijana wapate ajira.”

Kuna namna mbili ya kuangalia ukubwa wa tatizo la uhaba wa ajira. Mosi, kuangalia matukio yanaashiria moja kwa moja uwepo wa tatizo hilo. Pili, kuziangalia takwimu kwa mujibu wa serikali au mashirika yanashughulika na tafiti za aina hiyo.

Siku ya juzi, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Angelina Kairuki, alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa, waomba ajira 419 walidanganya ni walemavu kati ya waombaji 171,916 walioomba katika kada ya ualimu na afya kupitia Wizara hiyo.

Katika kada hizo mbili, waliopata ajira ya ualimu ni waombaji 13,130. Upande wa afya ni 5,319. Kwa hesabu za jumlisha na toa; jumla ya waliopata ajira katika kada zote mbili ni watu 18,449, na waliachwa kwa sababu mbalimbali ni 153,512. Hii inatoa picha pana ya ukubwa wa tatizo la ajira.

Licha ya kundi kubwa la waombaji wa nafasi ya ualimu kuachwa, kelele juu ya uhaba wa waalimu katika mashule ya serikali bado zitaendelea kusikika. Ndipo mjadala wa ajira unatupeleka katika kauli mzunguko; serikali haina pesa za kuajiri waalimu wote na shule za serikali zina uhaba wa walimu.

Juni 2014 zaidi ya watu 1000 walijitokeza katika uwanja wa taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa maombi ya kazi katika Idara ya Uhamiaji. Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, ilieleza kulikuwa na nafasi 70 pekee zilizohitaji waajiriwa wapya.

Kwa mujibu ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umasikini Tanzania (REPOA) ya 2019, takribani vijana milioni moja wanahitimu kila mwaka kutoka taasisi mbalimbali za kielimu, huku idadi ya ajira zinazozalishwa kutoka serikalini na sekta binafsi ni 250,000, kwa wastani wa kila mhitimu anatumia miaka 5.5 kupata ajira.

Hali ikoje barani Afrika?

Hadi mwezi Aprili 2023 takwimu za ajira nchini Kenya zinaonesha uwepo wa asilimia 4.9 ya watu wasio na ajira, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya nchi hiyo (KNBS). Ofisi hiyo hukusanya takwimu kwa kuzingatia watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini hawana kazi na wanaendelea kutafuta kazi.

Mwezi Aprili 2022, mamia ya vijana walipiga mstari nje ya ubalozi wa Urusi nchini Ethiopia kwa siku kadhaa kwa matumaini ya kuandikishwa kwenda kupigana vita upande wa Urusi nchini Ukraine. Licha ya ubalozi huo kukanusha kusajili watu, picha katika mitandao ya kijamii zilionesha makundi ya vijana wakiwa nje ya ubalozi.

Kwenda vitani mara nyingi huwa ni chaguo la mwisho ikiwa hakuna chaguo la kupata pesa pasi na kushika silaha. Yumkini vijana hawa ikiwa wangekuwa na kazi za maana, na mishahara mizuri, wasingepanga foleni kuomba kusajiliwa katika vita visivyo wahusu.

Kuna mambo kadhaa yanayochangia mamia ya Waafrika kufanya safari ya hatari kupitia jangwa la Sahara hadi Afrika Kaskazini, kisha hutumia maboti kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya. Baadhi ya safari hizi hugeuka misiba.

Ukosefu wa ajira katika bara la Afrika ni moja kati ya hizo sababu, zinazochangia Waafrika hasa vijana kukimbilia Ulaya. Kutoka 2014 hadi 2022 inakadiriwa watu 2,062 wamefariki wakijaribu kuvuka bahari hiyo na kuna maelfu ambao wamepotea.

Bilashaka kila taifa barani Afrika lina mbinu zake za kupambana na tatizo hilo, kuna miradi ya kusaidia vijana, misaada kutoka mataifa mengine na mashirika binafsi – ingawa bado ukubwa wa tatizo ni mkubwa. Hapa ni kusema; Afrika bado ina safari ndefu kutokomeza tatizo la uhaba wa ajira.