Kwa nini Bashar al-Assad alikimbilia Urusi na ni hatima gani inayomngoja yeye na familia yake?

Asma al-Assad akiwa na mumewe ,ambaye ni rais wa Syria aliyeondolewa ,wamesafiri hadi Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Asma al-Assad akiwa na mumewe ,ambaye ni rais wa Syria aliyeondolewa ,wamesafiri hadi Urusi
    • Author, Sam Hancock
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kuondolewa kwa Bashar al-Assad nchini Syria kumetamatisha si tu urais wake wa miaka 24, bali pia utawala wa zaidi ya miaka 50 wa familia ya Assad nchini Syria.

Kabla ya Assad kuchukua madaraka mwaka 2000, baba yake, Hafez al-Assad, alikuwa rais wa Syria kwa miongo mitatu hadi kifo chake.

Sasa, na kuundwa kwa serikali ya mpito ya upinzani inayongozwa na kundi la kiislamu la Tahrir al-Sham, mustakabali wa rais aliyeondolewa, mke wake, na watoto watatu uko katika hali ya kutatanisha.

Familia ya Assad sasa imekimbilia Urusi, ambapo imewapa hifadhi. Lakini ni nini kinachowasubiri?

Kwanini Assad alikimbilia Urusi?

Urusi ilikuwa na ukuruba mkubwa wa Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria na inamiliki vituo viwili vikubwa vya kijeshi nchini humo.

Mwaka 2015, Urusi ilianza kushambulia angani kumsaidia Bashar al-Assad nchini Syria, na kupindua mwelekeo wa vita kwa faida ya serikali ya Assad.

Kundi la uangalizi lenye makao yake Uingereza liliripoti kuwa miaka tisa baada ya operesheni kuanza, zaidi ya watu 21,000, wakiwemo raia 8,700, wameuawa katika mashambulizi ya kijeshi ya Urusi.

Lakini kutokana na Urusi kuingia katika vita vya Ukraine, Moscow imekuwa haiko tayari kuingilia matukio ya hivi karibuni ya Syria au kushindwa kusimamisha kasi ya mapambano ya waasi ambayo yalianza mwishoni mwa mwezi Novemba.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Saa kadhaa baada ya vikosi vya waasi kuchukua udhibiti wa Damascus, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kuwa Assad na familia yake walifika Moscow, ikidaiwa kuwa wangepewa hifadhi kwa "misingi ya kibinadamu."

Lakini alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu mahali alipo Assad na ombi lake la hifadhi, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema: "Sina jambo lolote la kusema kwa sasa. Kwa wazi, uamuzi kama huo [wa kutoa hifadhi] hauwezi kufanywa bila idhini ya rais. Uamuzi huu ni wake."

Ripoti ya uchunguzi ya Financial Times ya mwaka 2019 ilionyesha kuwa familia ya Assad na jamaa zao walinunua angalau vyumba 18 vya kifahari katika mji mkuu wa Urusi, wakiwa wametoa mamilioni ya dola wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.

Kwa upande mwingine, mtoto mkubwa wa Assad, Hafez, mwenye umri wa miaka 22, ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu mjini Moscow,

Wakati wa kilele cha mabadiliko nchini Syria, televisheni ya serikali ya Urusi iliripoti kuwa maafisa wa nchi hiyo mjini Moscow walikuwa wakifanya mazungumzo na "waasi wa Kisyria waliokuwa na silaha" kuhakikisha usalama wa vituo vya kijeshi vya Urusi na maeneo ya kidiplomasia.

Ni kipi tunachojua kuhusu mke na watoto wa Bashar al-Assad

Bashar al-Assad amemuoa Asma, raia wa nchi mbili wa Syria na Uingereza.

Wazazi wa Asma ni raia wa Syria na alizaliwa na kulelewa magharibi mwa Uingereza.

Alimaliza masomo yake ya shule na chuo kikuu mjini London na alifanya kazi kama mshauri wa uwekezaji wa benki kabla ya kuolewa.

Asma alihamia Syria kwa kudumu mwaka 2000 na akaolewa na Bashar katika kipindi alipokuwa akichukua madaraka kutoka kwa baba yake.

Dkt. Nasrin Al-Rifai, mtafiti wa muda katika Shule ya Uchumi na Sayansi ya Siasa ya London, aliiambia BBC kwamba Asma "ana pasipoti ya Uingereza" na anaweza "kurudi Uingereza" badala ya kukaa Urusi.

Aliongeza: "Hata hivyo, Marekani imeweka vikwazo kwa Dkt. Fawaz Al-Akhras, baba wa Asma, ambaye pia anasemekana kuwa yupo Urusi." Kwa sababu hii, Asma pia anaweza kupendelea kubaki Moscow kwa sasa.

Tovuti ya gazeti la Uingereza la Daily Mail iliripoti, ikinukuu majirani wa familia ya Asma, kuwa baba yake, mtaalamu wa magonjwa ya moyo, na mama yake, Sahar, ambaye ni balozi mstaafu, wanataka kusafiri hadi Moscow "kumfariji" binti yao na mumewe.

Bashar al-Assad na Asma wana watoto watatu: Hafez (mwanafunzi wa shahada ya uzamivu), Zain, na Karim.

Aliyekuwa rais wa Syria Hafez al- Assad pamoja na mkewe Anisa na watoto wake (kushoto hadi kulia) Maher,Bashar,Bassel,na Majd katika picha iliyopigwa mwaka 1990

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliyekuwa rais wa Syria Hafez al- Assad pamoja na mkewe Anisa na watoto wake (kushoto hadi kulia) Maher,Bashar,Bassel,na Majd katika picha iliyopigwa mwaka 1990

Idara ya marekani imeripoti kuwa bunge la marekani mwaka 2022 kuwa thamani ya utajiri wa familia ya Assad inakadiriwa takriban dola bilioni moja hadi dola bilioni mbili ,lakini inasema kuwa huenda ni vigumu kuwa na kiwango kamili cha utajiri wao kwani mali na fedha zao ''zimetawanyika huku zingine wakiwa wamezificha katika sekta mbali mbali.''

Kulingana na ripoti hiyo pia,Bashar na mkewe Asma walikuwa na ukaribu sana na wawekezaji katika sekta ya uchumi na ''walitumia baadhi ya kampuni katika ulanguzi wa fedha na kufadhili utawala wa Assad''.

Ripoti pia zinasema Asma alikuwa mshawishi mkubwa katika kamati ya uchumi nchini Syria na alikuwa kifua mbele katika uamuzi wa ''ruzuku katika bidhaa kama vile chakula,mafuta na biashara.''

Pia Asma alikuwa na ushawishi katika mpangilio wa maendeleo nchini Syria ambapo msaada kutoka mataifa ya kigeni yalielekezwa katika kukarabati maeneo kadhaa nchini humo.

Mwaka 2020,aliyekuwa katibu mkuu wa Marekani Mike Pomper alisema Asma akisaidiwa na mumewe alikuwa mfanyibiashara aliyefaidika zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria,

Afisa mkuu katika utawala wa Trump pia alimtaja kama Asma kama kichwa cha familia ikifika ni masuala ya uchumi na mjumbe wa serikali ambaye alikuwa akishindana na binamu wa Bashar anayefahamika kama Rami Makhlouf.

Rami Makhlouf ni mmoja wapo wa mabwenyenye tajika nchini Syria .

Mzozo wa kifamilia ulikuwa dhahiri kiasi cha kwamba Makhlouf alirusha video mitandaoni akilalamikia kuwa alikuwa akihujumiwa na familia ya Assad.

Je,Bashar al- Assad atahukumiwa?

Baada ya kuanguka kwa Assad, Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnes Callamard, alisema kuwa watu wa Syria walikumbana na "mfululizo wa ukiukwaji wa haki za binadamu ambao ulisababisha mateso yasiyo na mwisho na yanayojulikana" chini ya utawala wake.

Hii ni pamoja na "shambulizi za silaha za kemikali, mabomu yakushtukizia na uhalifu mwingine wa kivita, pamoja na mauaji, mateso, kupotea katika njia tatanishi na mauaji ya kimbari, yote haya ni makosa dhidi ya ubinadamu."

Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa wale wanaoshukiwa kwa kuvunja sheria za kimataifa na ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu wanashitakiwa na kushtakiwa kwa makosa yao.

Jumanne wiki jana, kiongozi wa upinzani wa kiislamu nchini Syria alitangaza kuwa majina ya maafisa wakuu wa utawala wa Assad walioshiriki katika mateso ya wafungwa wa kisiasa yatafichuliwa.

Abu Muhammad al-Julani pia alisema kuwa "Serikali ya Ukombozi ya Syria" itajaribu kuwarejesha maafisa makatili ambao wamekimbilia nchi nyingine nchini Syria.

Nchini Ufaransa, majaji wanaochunguza Bashar al-Assad wameomba hati ya kukamatwa kwa mashitaka ya ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita ambao ilitokea katika shambulizi la kemikali ambalo liliua maelfu mwaka 2013. Hatua hii inategemea ''mamlaka ya kisheria ya kimataifa."

Upelelezi ni mchakato wa kisheria ambapo mtu anarudishwa kwa nchi nyingine au jimbo ili kukabiliwa na kesi ya mashitaka kwa tuhuma za uhalifu.

Hata hivyo Urusi hairejeshi raia wake ambaye ni mkosaji ahukumiwe katika nchi aliyofanya makosa.

Itakuwa vigumu kwa Assad kuondoka Urusi na kwenda nchini nyingine ambayo itamrejesha nchini Syria au nchi ambayo inaweza kumhukumu kwa mashtaka dhidi yake.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid