JNIM: Jinsi kundi hili la wanamgambo lilivyogeuka kuwa moja ya mashirika mabaya zaidi ya kigaidi barani Afrika

Muda wa kusoma: Dakika 7

Kuongezeka kwa ghasia za wanajihadi katika mataifa ya Burkina Faso, Mali na Niger kunaongeza wasiwasi juu ya iwapo eneo la Sahel huko Afrika Magharibi linazidi kukosa udhibiti.

Kikundi kimoja cha mwamvuli chenye uhusiano na al-Qaeda kinadai kuhusika na mashambulizi mengi lakini ni kina nani na wanataka nini?

Pia unaweza kusoma

JNIM ni nani?

Jamaat Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) limekuwa mojawapo ya makundi ya kijihadi hatari zaidi barani Afrika ndani ya kipindi cha miaka michache tu.

Kundi hilo limeundwa nchini Mali, na sasa ilnafanya kazi katika Sahel, eneo kubwa la jangwa linalojumuisha nchi 10 kutoka pwani ya magharibi ya Afrika kuelekea mashariki katika bara zima.

JNIM linadhaniwa kuhusika na zaidi ya nusu ya vurugu zote za kisiasa zilizotokea katika eneo la Sahel ya Kati, kati ya Machi 2017 na Septemba 2023.

Mnamo 2024, takriban 19% ya mashambulizi yote ya kigaidi duniani kote na zaidi ya nusu ya vifo vyote vinavyohusiana na ugaidi duniani vilitokea Sahel, kulingana na Ripoti ya Global Terrorism Index (GTI) ya 2025 iliyochapishwa na Taasisi ya Amani ya 2025.

Ingawa ni vigumu kujua ni wapiganaji wangapi walio sehemu ya JNIM, au wangapi wameajiriwa hivi majuzi, wataalam wanapendekeza kuwa inaweza kuwa maelfu kadhaa - wengi wao wakiwa vijana, wanaume wa ndani.

JNIM ilianza vipi na inataka nini ?

JNIM iliundwa mwaka wa 2017 - kama muunganisho kati ya vikundi vinne vya wanamgambo wa Kiislamu vinavyofanya kazi Afrika Kaskazini na Sahel: Ansar Dine, Katibat Macina, al-Mourabitoun na tawi la Sahara la Al-Qaeda katika Maghreb ya Kiislamu (AQIM).

Kundi hilo linaongozwa na Iyad Ag Ghali, mwanadiplomasia wa zamani wa Mali ambaye anatoka katika kabila la Tuareg lenye Waislamu wengi.

Aliendelea kuongoza maasi ya Tuareg dhidi ya serikali ya Mali mwaka 2012, ambayo ilitaka kuanzisha taifa huru kaskazini mwa Mali.

Pia kuna naibu kiongozi, Amadou Koufa, ambaye anatoka jamii ya Fulani. Wachambuzi wanaamini kwamba uongozi huu mkuu unasaidia kuongoza matawi ya ndani ya JNIM ambayo yanaenea katika Sahel - mtandao unaojulikana kama 'katibat'.

JNIM huchapisha maandishi na maudhui ya video kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kwenye ChirpWire na Telegram kupitia mkono wa vyombo vya habari unaoitwa al-Zallaqa.

Lengo la kundi hilo ni kuchukua nafasi ya mamlaka za serikali na tafsiri ya kihafidhina ya sheria na utawala wa Kiislamu.

Pia awali wametoa wito wa kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni nchini Mali.

Wanafanya operesheni zao wapi?

JNIM ilianza katikati mwa Mali lakini imepanua wigo wake kwa haraka ikidai kuhusika na mashambulizi huko Burkina Faso, Togo, Benin, Niger na Ivory Coast.

Kundi hilo sasa linafanya kazi katika mikoa yote ya Mali na mikoa 11 kati ya 13 nchini Burkina Faso, kulingana na Mpango wa Kimataifa wa Kupambana na Uhalifu wa Kuratibu wa Kimataifa (GI-TOC).

Burkina Faso imekuwa kitovu cha shughuli za kundi hilo - hasa katika mikoa ya mpaka wa kaskazini na mashariki.

Kuanzia Januari-Mei 2025, JNIM ilidai kuhusika na zaidi ya mashambulizi 240 ya watu binafsi - mara mbili ya idadi ya kipindi kama hicho mwaka wa 2024, kulingana na data iliyothibitishwa na BBC.

JNIM pia inafanya uwepo wake kuhisiwa katika maeneo makubwa ya Mali na Burkina Faso.

Wanachama wa kikundi hicho hukusanya 'kodi' kutoka kwa vijiji - vinavyojulikana kama zakat - huweka kanuni kali za mavazi na kuweka vizuizi, ambapo watu lazima walipe ili kuondoka na kuingia eneo hilo, kulingana na Beverly Ochieng, mchambuzi mkuu wa Control Risk, kampuni ya ushauri ya kimataifa.

Toleo hili la Uislamu linaweza kutofautiana na Uislamu unaotekelezwa na jumuiya za wenyeji, anasema Yvan Guichaoua, mtafiti mkuu katika Kituo cha Kimataifa cha Bonn cha Mafunzo ya Migogoro.

"Tabia hizi ni dhahiri zinaachana na mazoea yaliyowekwa na kwa hakika sio maarufu sana," anasema. "Lakini kama inavutia au la, inategemea pia kile ambacho serikali inaweza kutoa, na kumekuwa na kukata tamaa kwingi katika kile ambacho serikali imekuwa ikifanya kwa miaka iliyopita."

Je, mashambulizi ya JNIM yanaongezeka kiwango?

Zaidi ya mashambulio 3000 yalifanywa na kundi hilo huko Burkina Faso, Mali na Niger mwaka jana, kulingana na shirika la Mahali pa Migogoro ya Kivita na Takwimu za Tukio {Armed Conflict Location and Event Data ACLED).

Ochieng anaeleza makundi hayo hutumia mbinu mbalimbali zilizobuniwa kusababisha usumbufu mkubwa. "Wanatega IED (mifumo ya vilipuzi iliyoboreshwa) kwenye barabara muhimu, na wana silaha za masafa marefu."

"Pia (pia) wanalenga vikosi vya usalama katika kambi za kijeshi, hivyo silaha zao nyingi zinatokana na hilo. Pia wameshambulia raia - katika matukio ambayo jamii zinadhaniwa kushirikiana na serikali," anaongeza.

Mashambulizi yamekuwa makali zaidi na ya mara kwa mara katika miezi michache iliyopita. Kundi hilo lilidai kuhusika na shambulizi kubwa mwezi Juni katika mji wa Boulikessi nchini Mali, ambapo wanajeshi 30 waliuawa, kulingana na vyanzo vya Reuters.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa wanajeshi zaidi ya 400 wanakisiwa kuuawa na waasi tangu mwanzoni mwa mwezi Mei katika kambi za kijeshi na miji iliyotawanyika kote nchini Mali, Niger na Burkina Faso, na kusababisha mshtuko katika eneo ambalo tayari halijatulia na lina uwezekano wa kufanya mapinduzi.

"Mashambulio ya mara kwa mara ya wiki iliyopita hayajasikika hadi sasa," anasema Guichaoua. "Kwa kweli wameongeza shughuli zao katika wiki zilizopita."

Ingawa ukandamizaji dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na kupungua kwa idadi ya vyombo vya habari - magazeti na watangazaji - ulifungwa kufuatia msururu wa mapinduzi nchini Burkina Faso, Niger na Mali, inamaanisha kuwa idadi ya mashambulizi yanayohusishwa moja kwa moja na makundi ya wanamgambo huenda hayaripotiwi.

Mapinduzi ya kijeshi yalifanyika Niger mwaka 2023, Burkina Faso mwaka 2022 na Mali mwaka 2020.

JNIM inafadhiliwa vipi?

JNIM hupata pesa kupitia njia mbalimbali. Hapo awali hii ilikuwa ni pamoja na kuteka nyara mateka wa kigeni kwa ajili ya fidia na kuomba fedha kwa ajili ya kupita kwenye njia za kupitisha madini na mifugo.

"Wizi wa ng'ombe ndio chanzo kikuu cha mapato kwa JNIM," mchambuzi mmoja kutoka GI-TOC ambaye BBC ilizungumza naye.

Mchambuzi huyo hakutaka jina lake litajwe kwani linaweza kuhatarisha usalama wao nchini.

"Mali ni msafirishaji mkubwa wa ng'ombe kwa hivyo ni rahisi kwao kuiba wanyama na kuwauza."

Utafiti wa GI-TOC unaonyesha kuwa katika mwaka mmoja katika wilaya moja tu, JNIM ilipata FCFA milioni 440 ($768,00 USD).

Kulingana na takwimu hii, JNIM inaweza kuwa inapata mamilioni kutokana na wizi wa mifugo.

"Migodi ya dhahabu ni eneo lingine kubwa la mapato, wanatoza ushuru watu wanaoingia na kutoka katika eneo lao."

Mkuu wa Kamandi ya Marekani Afrika Jenerali Michael Langley, aliwaambia waandishi wa habari wa Marekani wiki jana kwamba anaamini mojawapo ya malengo ya msingi ya JNIM ni kudhibiti ukanda wa pwani, ili "waweze kufadhili shughuli zao kupitia magendo, biashara ya binadamu na biashara ya silaha."

Vipi kuhusu juhudi za kukabiliana na waasi?

Vikosi vya kijeshi vya Ufaransa vilikuwa vikiunga mkono serikali ya Mali kwa karibu muongo mmoja - na zaidi ya wanajeshi 4,000 wakiwekwa katika vikundi vya mapigano vya Sahel kama JNIM.

Ingawa walipata mafanikio ya awali mwaka wa 2013 na 2014, kurejesha maeneo kutoka kwa makundi ya wanajihadi na kuua makamanda kadhaa wakuu, jitihada hizi zinaonekana kushindwa kuzuia ukuaji wa JNIM wa siku zijazo.

"Juhudi za kukabiliana na waasi zimeshindwa hadi sasa kwa sababu ya wazo hili kwamba JNIM inaweza kushindwa kijeshi, lakini ni kwa mazungumzo tu ndipo kundi litaisha," mchambuzi wa GI-TOC alipendekeza.

Miaka michache iliyopita nchi za Sahel ziliungana na kuunda Kikosi Kazi cha G5 Sahel, kikundi cha wanajeshi 5000 wa kimataifa.

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Burkina Faso, Mali na Niger zimejiondoa, na kudhoofisha uwezo wa kikosi kazi kukabiliana na uasi.

MINUSMA, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa - ingawa sio juhudi za kukabiliana na ugaidi - pia kilikuwa nchini Mali kwa muongo mmoja kusaidia juhudi, hizo.

Je, mapinduzi ya kijeshi yamekuwa na athari gani kwa JNIM?

Ripoti zinaonyesha vifo katika eneo la Sahel vimeongezeka mara tatu kutoka viwango vilivyoonekana mwaka 2020, wakati mapinduzi ya kwanza ya kijeshi katika eneo hilo yalipotokea nchini Mali.

Utawala mbovu chini ya mamlaka ya kijeshi nchini Burkina Faso, Mali na Niger hatimaye umeruhusu makundi ya wanamgambo, kama vile JNIM, kushamiri kulingana na wachambuzi.

Wanamgambo hao walikuwa wepesi kuwaambia wanajeshi wa Ufaransa kuondoka, na kuwabadilisha na usaidizi wa Urusi na kikosi cha pamoja kilichoundwa na nchi tatu za Saheli. Hatahivyo, kundi la wanamgambo wa Urusi Wagner sasa linaondoa wanajeshi wake kutoka Mali.

Nchini Burkina Faso, jeshi linaloitwa 'jeshi la kujitolea' ni mkakati mmoja unaotumiwa kupambana na wanamgambo.

Rais, Ibrahim Traore, amesema anataka kuajiri wapiganaji 50,000. Lakini wataalam wanasema wengi wa wajitolea wanaandikishwa kwa nguvu na mafunzo duni inamaanisha mara nyingi wanapata hasara kubwa.

Wanajeshi wenyewe pia wameshutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kufanya ukatili dhidi ya raia, hasa watu wa jamii ya Fulani, kwa madai ya kushirikiana na makundi ya wanamgambo, na hivyo kukwamisha juhudi za amani.

Kati ya Januari 2024 na Machi 2025, vikosi vya serikali na washirika wao wa Urusi walihusika na mauaji ya raia 1486 nchini Mali, karibu mara tano zaidi ya JNIM, kulingana na GI-TOC.

Unyanyasaji huu uliokithiri dhidi ya raia umezua hasira kwa serikali, na kuchochea kuajiri zaidi kwa wapiganani wa JNIM.

Huku nchi zikijitahidi kuzuia uasi huo kuna wasiwasi kwamba JNIM itaendelea kupanuka katika eneo lote la Sahel.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdallla