Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, nta ya sikio inaweza kufichua maradhi uliyonayo?
- Author, Jasmin Fox-Skelly
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kuanzia magonjwa ya akili hadi saratani, uchafu wa sikio (nta) unaweza kutoa viashiria muhimu juu ya afya ya mtu. Wanasayansi wanachambua nta kwa matumaini ya kupata njia mpya za kugundua magonjwa.
Nta una rangi ya chungwa na unanata. Nta ni mchanganyiko wa nywele, ngozi iliyokufa na uchafu mwingine. Mara baada ya kuundwa kwenye mfereji wa sikio, husafirishwa kutoka ndani ya sikio hadi nje.
Faida za Nta
Miongoni mwa sababu za kuzalishwa nta ni kuuweka mfereji wa sikio safi na kuulainisha. Pia hutumika kama mtego, kuzuia bakteria, kuvu na wadudu wengine kutoingia katika sikio.
Fauka ya hayo, kutokana na tafiti kadhaa za kisayansi - nta sasa unaweza kutumika kugundua aina fulani ya habari za maana na muhimu kuhusu afya ya binadamu.
Kwa mfano, idadi kubwa ya watu wa asili ya Ulaya au Afrika wana nta wenye unyevunyevu, ambao una rangi ya manjano au machungwa na unanata. Hata hivyo, 95% ya watu wa Asia Mashariki wana nta mkavu, ambao ni wa kijivu na usio nata.
Jeni inayohusika na kutoa nta wa masikio wenye unyevu au mkavu inaitwa ABCC11. Jeni hii pia inahusika kwenye kuzalisha harufu ya makwapa. 2% ya watu - wenye nta mkavu – jeni hii huwafanya makwapa yao kutonuka.
Tafiti kuhusu nta
Mwaka 1971, Nicholas L Petrakis, profesa wa dawa katika Chuo Kikuu cha California, San Francisco, aligundua kuwa wanawake Wazungu, Weusi na Wajerumani huko USA, ambao wote walikuwa na "nta wenye unyevu," wana uwezekano mara nne wa kufa kutokana na saratani ya matiti kuliko wanawake wa Kijapani na Taiwan walio na nta "mkavu."
Mwaka 2010, watafiti kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Tokyo walichukua sampuli za damu kutoka kwa wanawake 270 walio na saratani ya matiti, na wanawake wasio na saratani 273. Waligundua kuwa wanawake walio na saratani ya matiti walikuwa na uwezekano wa hadi 77% wa kuwa na jeni ambayo inafanya nta kuwa wa unyevu kuliko wale wasiokuwa na saratani.
Ugonjwa wa Covid-19 pia wakati mwingine unaweza kupimwa kwa kutumia nta wa masikio, na nta wa masikio pia unaweza kukuambia kama mtu ana kisukari cha aina ya 1 au cha pili. Tafiti pia zinasema nta unaweza kutoa ugunguzi kwa aina fulani ya ugonjwa wa moyo.
Nelson Roberto Antoniosi Filho, profesa wa kemia katika Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Goiás nchini Brazili, ameorodhesha ugonjwa wa kisukari, saratani, kupoteza kumbukumbu na mishipa ya fahamu, kama mfano wa magonjwa ambayo huzalisha aina fulani ya kemikali au huacha kuzalisha, na hivyo ugonjwa unaweza kugunduliwa kupitia sampuli za nta."
Maabara ya Antoniosi Filho imegundua kuwa nta wa masikio hubeba kemekili za magonjwa hayo, zaidi kuliko vimiminika vingine vya kibayolojia kama vile damu, mkojo, jasho na machozi.
Utambuzi wa magonjwa
Kwa kuzingatia hili, Antoniosi Filho na timu yake wanatengeneza "cerumenogram" - chombo cha uchunguzi wanachodai kinaweza kutabiri kwa usahihi ikiwa mtu ana aina fulani za saratani kulingana na nta wa masikio yake.
Katika utafiti wa 2019, timu ya Antoniosi Filho ilikusanya sampuli za nta kutoka kwa watu 52 wenye saratani. Watafiti pia walichukua nta kutoka kwa watu 50 wasio na saratani.
Watafiti waligundua kemikali 27 kwenye nta wa sikio, kemikali ambazo hutumika katika utambuzi wa saratani. Kwa maneno mengine, timu hiyo inaweza kutabiri kwa usahihi wa 100% ikiwa mtu ana saratani ya damu na ngozi kulingana cha kemikali hizi 27.
"Katika siku zijazo, tunatumai cerumenogram itatumika katika uchunguzi wa kawaida wa kliniki, kwa kutumia sehemu ya nta ya sikio, kugundua magonjwa kama vile kisukari, saratani, magonjwa ya neva, na magonjwa ya akili na pia kutathmini mabadiliko ya kimetaboliki," anasema Antoniosi Filho.
Kwa sasa pia wanafanya kazi ya kutengeneza kifaa cha majaribio kinachofanana na kile unachonua kwa ajili ya kupima Covid-19.
Perdita Barran, mwanakemia na profesa katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza, anakubali kwamba, kinadharia, inawezekana nta kutumika kuangalia dalili za ugonjwa.