Maandamano Tanzania: Disemba 9 yaanza kwa utulivu, ulinzi ukiimarishwa

s
Maelezo ya picha, Kituo cha mafuta Segerea, Dar es Salaam kikiwa kimefungwa kwa tahadhari
Muda wa kusoma: Dakika 2

Huku leo Disemba 9, siku ambayo pia ni kumbukumbu ya Uhuru wa Tanzania bara, ikiwa ndio siku iliyotajwa kwa maandamano yaliyopigwa marufuku, hali katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo imeripotiwa kuwa tulivu asubuhi hii lakini yenye tahadhari kubwa.

Ulinzi umeimarishwa kote nchini Tanzania huku askari wakionekana wakifanya doria katika miji mikubwa.

Hadi kufikia majira ya tano kasoro asubuhi hakuna ripoti ya kuanza kwa maandamano.

Ingawa hakuna mikusanyiko iliyoonekana mapema leo, shughuli nyingi za biashara zimeendelea kubaki zimefungwa kama njia ya kujilinda endapo machafuko yatatokea.

Waandishi wa BBC wameshuhudia baadhi ya vituo vya mafuta, maduka na ofisi binafsi pamoja na za umma zikiwa zimefungwa, hatua inayohusishwa moja kwa moja na kumbukumbu ya maandamano ya Oktoba 29 ambayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Kwa mujibu wa takwimu za awali zilizotolewa na serikali, maandamano hayo yaliharibu ofisi za serikali zipatazo 756, vikaharibu vituo 27 vya mabasi ya mwendo kasi pamoja na mabasi 6 yaliyoteketezwa. Nyumba binafsi 273 zilipigwa au kuchomwa, vituo vya polisi 159 vilishambuliwa, na vituo binafsi vya mafuta 672 navyo viliharibiwa. Aidha, magari binafsi 1,642, pikipiki 2,268, na magari ya serikali 976 yaliteketezwa katika machafuko hayo, hali iliyowaacha wananchi wengi na kumbukumbu nzito kuhusu athari za vurugu hizo.

S
Tazama hapa
Maelezo ya video, Disemba 9 yaanza kwa utulivu Tanzania

Hali ya utulivu asubuhi ya leo imeripotiwa pia katika miji ya Arusha, Mbeya na Moshi, ambayo yalikuwa miongoni mwa maeneo makuu ya machafuko ya mwezi Oktoba. Mkoani Iringa vituo vya mafuta vimefunguliwa na ingawa biashara nyingi zimefungwa yakiwemo maduka na soko kuu na hakuna usafiri wa umma uliokuwa unafanya kazi mapema asubuhi. Ni kumbukumbu kwamba maandamano ya Oktoba 29 hayakuanza mapema, bali yalianza majira ya saa tano asubuhi katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya jiji na nchini.

Kwa upande wa ulinzi, askari wa Jeshi la Polisi na wenzao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wameonekana kwa wingi katika mitaa na barabara mbalimbali. Jeshi la Polisi limekumbusha kuwa maandamano yaliyopangwa kufanyika leo ni haramu kwa kuwa hayakufuata taratibu za kisheria zinazotakiwa. Serikali nayo imesisitiza kuwa inaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha amani na utulivu wa nchi unaendelea bila kuvurugwa.

Aidha, Serikali ilitoa wito jana kwa wananchi kusalia majumbani leo ikiwa hawana dharura. "Serikali inawashauri wananchi wote ambao tarehe 9 Desemba 2025 hawatakuwa na dharura kuitumia siku hiyo kwa mapumziko, hivyo kusherehekea siku hiyo wakiwa nyumbani, isipokuwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vyao," alisema Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.