Je, China itakuwa na uwezo wa kuwalisha watu wazee milioni 300?

Huanchun Cao na mkewe wanakabiliwa na tatizo linalowakabili wazee wengi wa China - ni nani atakayewatunza?

Chanzo cha picha, Lan Pan/ BBC

Maelezo ya picha, Huanchun Cao na mkewe wanakabiliwa na tatizo linalowasumbua wazee wengi wa China - ni nani atakayewatunza?

Muulize mkulima Huanchun Cao mwenye umri wa miaka 72 kuhusu pensheni yake na anajibu kwa mshituko wa koo.

Anakunja sigara yake ya kujitengezea, na kuinamisha kichwa chake kana kwamba swali hilo ni la kipuuzi. "Hapana, hapana, hatuna pensheni," anasema akimtazama mke wake wa zaidi ya miaka 45.

Bw Cao ni wa kizazi kilichoshuhudia kuzaliwa kwa China ya Kikomunisti. Kama nchi yake, amekuwa mzee kabla ya kuwa tajiri. Kama wafanyakazi wengi wa mashambani na wahamiaji, hana chaguo ila kuendelea kufanya kazi na kuendelea kuchuma mapato, kwa sabanu ameangukia kwenye wavu dhaifu wa usalama wa kijamii.

Kudorora kwa uchumi, kupungua kwa faida za serikali na sera ya miongo kadhaa ya mtoto mmoja kumezua mzozo wa idadi ya watu nchini China.

Chungu cha pensheni kinakauka na nchi inakosa wakati wa kujenga hazina ya kutosha kutunza idadi inayoongezeka ya wazee.

Katika muongo ujao, takriban watu milioni 300, ambao kwa sasa wana umri wa miaka 50 hadi 60, wanatazamiwa kuacha kufanya kazi. Hili ndilo kundi kubwa zaidi la umri, karibu sawa na ukubwa wa idadi ya watu nchini Marekani.

Nani atawaangalia? Jibu linategemea unaenda wapi na unauliza nani.

.

Bw Cao na mkewe wanaishi katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Liaoning, kitovu cha zamani cha viwanda nchini China.

Sehemu kubwa za mashamba na vilima vilivyochimbwa huzunguka jiji kuu la Shenyang. Moshi mwingi kutoka kwa viwanda vya kuyeyusha hujaa anga, pamoja na baadhi ya maeneo ya kitamaduni yaliyohifadhiwa kutoka kwa nasaba ya Qing.

Karibu robo ya idadi ya watu hapa wana umri wa miaka 65 au zaidi. Idadi inayoongezeka ya watu wazima wenye umri wa kufanya kazi wanaondoka kwenye viwanda vizito kutafuta kazi bora katika miji mikubwa.

Watoto wa Bw Cao wamehama pia lakini bado wako karibu vya kutosha kuwatembelea mara kwa mara.

"Nadhani ninaweza kuendelea kufanya hivi kwa miaka mingine minne au mitano," Bw Cao anasema, baada ya yeye na mkewe kurejea kutoka kuokota kuni. Ndani ya nyumba yao, miali ya moto hupiga chini ya jiko lenye joto - linaloitwa "kang" - ambalo ni chanzo chao kikuu cha joto.

xx

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

Wanandoa hao wanatengeneza karibu dola 2,700 kwa mwaka. Lakini bei ya mahindi wanayolima inashuka na hawawezi kumudu ikiwa wataugua.

"Katika miaka mitano, ikiwa bado nina nguvu za kimwili, labda naweza kutembea peke yangu. Lakini ikiwa nitakuwa dhaifu, basi ninaweza kufungiwa kitandani. Ni hivyo, kwisha. Nadhani nitakuwa mzigo kwa watoto wangu. Watahitaji kunitunza."

Hizo sio siku zijazo Guohui Tang mwenye umri wa miaka 55 anataka. Mumewe alipata ajali kwenye eneo la ujenzi na elimu ya chuo kikuu ya binti yao ikamaliza akiba yake.

Kwa hivyo mchimbaji huyo wa zamani aliona fursa katika utunzaji wa wazee ili kufadhili uzee wake mwenyewe. Alifungua nyumba ndogo ya kutunza yapata saa moja kutoka Shenyang.

.

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

Bi Tang anaonyesha kwenye kundi la watu wanne wanaocheza kadi huku jua likiwaka kwenye kihifadhi kidogo.

"Ona huyo mzee wa miaka 85 - hana pensheni, anategemea mtoto wake wa kiume na wa kike kabisa. Mwanawe analipa mwezi mmoja, binti yake analipa mwezi mwingine, lakini wanahitaji kuishi pia."

Ana wasiwasi kwamba yeye pia atamtegemea binti yake wa pekee: "Sasa nitalipa pensheni yangu kila mwezi, hata ikiwa inamaanisha kuwa siwezi kumudu kula au kunywa."

Kwa vizazi, Uchina imekuwa ikitegemea utunzaji wa watoto kujaza mapengo katika huduma ya wazee. Lilikuwa jukumu la mwana au binti kuwatunza wazazi waliozeeka

Lakini kuna wana na mabinti wachache kwa wazazi wazee kutegemea - sababu moja ni sheria ya "mtoto mmoja" ambayo ilizuia wanandoa kupata watoto wawili au zaidi kati ya miaka 1980 hadi 2015.

z

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

Kutokana na ukuaji wa uchumi, vijana pia wamehama kutoka kwa wazazi wao, na hivyo kuacha idadi kubwa ya wazee kujitunza au kutegemea malipo ya serikali.

Lakini mfuko wa pensheni unaweza kukosa pesa ifikapo 2035, kulingana na Chuo cha Sayansi cha Kichina kinachoendeshwa na serikali. Hayo yalikuwa makadirio ya 2019, kabla ya janga, ambalo liliathiri sana uchumi wa China.

China pia inaweza kulazimika kuongeza umri wa kustaafu. Ina mojawapo ya umri wa chini zaidi wa kustaafu duniani - 60 kwa wanaume, 55 kwa wanawake wa kazi za ofisini na 50 kwa wanawake wa kundi la kufanya kazi.

a

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

"Karibu nyumbani kwangu," anakaribisha Bibi Feng mwenye umri wa miaka 78, ambaye alitaka tu kutumia jina lake la mwisho.

Ni vigumu kufuatana naye anapokimbia kando ya korido ili kumwonya mumewe kwamba wageni wako njiani kuelekea chumba chao kwenye Jumba la Utunzaji la Sunshine. Darasa la mazoezi ya asubuhi, ambapo alikuwa akicheka na kusengenya nyuma ya jengo na marafiki zake, liliisha.

Wazee

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nyumba hiyo ilijengwa kwa kukaa zaidi ya wakazi 1,300. Takriban vijana 20 wanajitolea kuishi hapa bila malipo kwa ajili ya kusaidia kuwatunza baadhi ya wazee. Kampuni za kibinafsi kwa sehemu hufadhili makao, na kuondoa shinikizo kutoka kwa serikali ya mtaa.

Hili ni jaribio wakati viongozi wakiwinda suluhu kwa China inayozeeka. Hapa Hangzhou, kusini mwa China, wanaweza kumudu majaribio hayo.

Huu ni ulimwengu tofauti na Liaoning - majengo mapya yanayong'aa ambayo yanaibuka ya makampuni ya teknolojia kama vile Alibaba na Ant, kivutio cha wajasiriamali wadogo wadogo.

Fengs wamekuwa hapa kwa miaka minane. Nyumba ya wauguzi inaonekana kuwa nzuri na kuna mengi ya kufanya - kutoka kwa mazoezi na tenisi ya meza hadi uimbaji na michezo wa kuigiza.

"Ni muhimu sana kuweza kumaliza sehemu ya mwisho ya maisha mahali pazuri," Bibi Feng anasema. Yeye na mume wake wamekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 50. Ilikuwa upendo mara ya kwanza, wanasema.

Mjukuu wao alipohitimu kutoka shule ya upili, waliamua kuwa kazi yao ilikuwa imekamilika.

"Kuna watu wachache wa umri sawa ambao wanafikiri kama sisi," Bibi Feng anasema. "Inaonekana tunajali zaidi kufurahia maisha. Wale ambao hawakubaliani wanafikiri kuwa sio lazima kulipa pesa nyingi kuishi hapa ilhali wana nyumba zao."

Lakini anasema ana "nia iliyo wazi" zaidi: "Nilifikiria vizuri. Nilimpa mwanangu nyumba yangu. Tunachohitaji sasa ni kadi zetu za pensheni."

Chumba cha wanandoa kwenye nyumba ya utunzaji kinagharimu karibu Yuan 2,000 kwa mwezi. Kama wafanyikazi wa zamani wa kampuni zinazomilikiwa na serikali, wote wawili wana pensheni ya kutosha kufidia gharama.

xx

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

Lakini hata kwa wateja walio na pensheni nzuri, Nyumba ya Utunzaji Sunshine inaendesha kwa hasara. Mkurugenzi huyo anasema nyumba za utunzaji ni gharama kuanza na kuchukua muda kupata faida.

Beijing imekuwa ikishinikiza makampuni ya kibinafsi kujenga vituo vya kulelea watoto wadogo, wadi na miundombinu mingine ya kutunza umri ili kuziba mapengo yaliyoachwa na serikali za mitaa zenye madeni. Lakini wataendelea kuwekeza ikiwa faida iko mbali?

Nchi nyingine za Asia Mashariki kama vile Japani pia zinatafuta pesa za kutunza idadi kubwa ya wazee. Lakini Japan ilikuwa tayari tajiri wakati ilipokuwa na mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya watu wazee duniani.

Uchina, hata hivyo, inashuhudia kuongezea kwa watu wazee haraka. Kwa hivyo, wazee wengi wanalazimika kujitafutia njia zao wenyewe katika umri ambao wanapaswa kupanga kustaafu kwao.

Huko Liaoning, moshi wa kuni unapanda kutoka kwenye mabomba ya moshi, kuashiria wakati wa chakula cha mchana. Bw Cao anawasha moto jikoni kwake ili kuchemsha maji ili kupika wali.

x

Chanzo cha picha, Xiqing Wang/ BBC

“Nikifikisha miaka 80, natumai watoto wangu watarudi kuishi nami,” anasema huku akipata sufuria.

"Sijiungi nao mijini. Kwao hamna lifti na unahitaji kutembea hadi orofa tano. Hiyo ni ngumu zaidi kuliko kupanda mlima."

Kwa Bw Cao hii ni njia ya kufanya mambo. Inabidi aendelee kufanya kazi mpaka asiweze tena .

"Watu wa kawaida kama sisi wanaishi hivi," anasema, akionyesha mashamba ya nje ambayo bado yamefunikwa na barafu. Msimu wa kupanda utarudi- ambayo ni kazi zaidi kwa ajili yake na mke wake.

"Ukilinganisha na maisha ya mjini, bila shaka, wakulima wana maisha magumu zaidi. Unawezaje kupata riziki ikiwa huwezi kustahimili ugumu huo?"

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi