Je, Kenya ipo mbioni kupitisha sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika ishara ya hivi karibuni ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja katika nchi tofauti za Afrika, mbunge wa upinzani nchini Kenya anaongoza kampeni za bunge kuharamisha jamii ndogo ya LGBTQ nchini humo.

Hatua ya George Peter Kaluma inajiri baada ya taifa jirani la Uganda kupitisha sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, na kukataa vitisho vya Rais wa Marekani Joe Biden kuweka vikwazo na vizuizi vya usafiri kwa "mtu yeyote anayehusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu".

Nilipokutana na Bw Kaluma - mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement cha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya Raila Odinga - alikuwa ameketi nyuma ya meza katika ofisi yake iliyoko mji mkuu wa Nairobi, akisoma ushahidi na kufanya masahihisho ya mswada ambao ananuia kuwasilisha bungeni hivi karibuni. .

"Tunataka kupiga marufuku kila kitu kinachohusiana na wapenzi wa jinsia moja," Bw Kaluma ananiambia, akiongeza kuwa mswada wake utakuwa mpana zaidi kuliko sheria iliyopitishwa na bunge la Uganda na kuidhinishwa na Rais Yoweri Museveni mwezi wa Mei.

Sheria ya Uganda inachukuliwa kuwa mojawapo ya sheria kali zaidi dhidi ya LGBTQ duniani.

Inapendekeza kifungo cha maisha jela kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya mapenzi ya jinsia moja, na adhabu ya kifo kwa kesi zinazoitwa kuwa mbaya zaidi, ambazo ni pamoja na kufanya mapenzi ya jinsia moja na mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 au pale mtu anapoambukizwa ugonjwa wa maisha kama vile VVU.

Kwa upande mwingine wa bara, wabunge nchini Ghana mapema mwezi huu walipiga kura kwa kauli moja kuunga mkono marekebisho ya sheria ya nchi hiyo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, na kuisongeza karibu na kupitishwa kuwa sheria.

Ingawa ni kali kuliko sheria mpya ya Uganda, Mswada wa Kukuza Haki Sahihi za Kimapenzi na Maadili ya Familia ya Ghana unapendekeza kifungo cha miaka mitatu jela kwa yeyote anayejitambulisha kama LGBTQ na kifungo cha miaka 10 kwa yeyote anayeendeleza mapenzi ya jinsia moja.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa hivyo kwa nini nchi tofauti za Kiafrika zinapendekeza hatua za kupinga LGBTQ kwa wakati mmoja?

Wengine wanafikiri kwamba vikundi vya kiinjilisti vya Marekani vinaweza kuwa na jukumu kwa kusukuma ajenda zao katika bara.

Katika safari ambayo Bw Kaluma anasema ililipwa na bunge la Kenya, alihudhuria mkutano wa Jukwaa jipya la Mabunge ya Afrika kuhusu Maadili ya Familia na Utawala uliofanyika nchini Uganda mwezi Machi.

Wabunge, viongozi wa kidini na wanakampeni kutoka zaidi ya mataifa 20 ya Afrika walishiriki, walibadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kukabiliana na kile wanachokiona kuwa vitisho kwa maadili ya kihafidhina ya kidini na kijamii.

"Mswada huo utapendekeza kupigwa marufuku kabisa kwa kile ambacho nchi za Magharibi hukiita maagizo na taratibu mpya za ngono, na kukataza shughuli zote zinazoendeleza mapenzi ya jinsia moja, kwa kuzingatia ... gwaride linaloashiria kundi hilo katika jamii, maonyesho yao, kuvaa rangi zao, bendera na nembo za kundi la LGBTQ," Bw Kaluma anasema.

Mapenzi ya jinsia moja tayari ni haramu nchini Kenya, lakini seŕikali pia inaweza kuvumilia washiriki wa mapenzi ya jinsia moja – kwa mfano, imetoa hifadhi kwa watu kutoka nchi nyingine za Afŕika, ikiwa ni pamoja na Uganda, ambao walikabiliwa na mateso katika nchi zao kutokana na mwelekeo wao wa kijinsia.

Bw Kaluma ananiambia anataka hifadhi yao ifutiliwe mbali, na wao kuondoka Kenya.

Katika kanisa dogo lililofichwa lililoanzishwa ili kuwafariji na kuwaunga mkono washiriki wa LGBTQ katikati mwa jiji la Nairobi, kasisi huyo wa kike anasema mswada wa Bw Kaluma unasababisha "wasiwasi, hofu na woga mwingi".

Mchungaji na waumini wa kanisa hilo wanaomba tusiwatambue kwa sababu wanasema wamekabiliwa na vitisho vingi vya usalama tangu lilipoanzishwa takriban miaka 10 iliyopita.

Anaamini kuwa sheria inayopendekezwa itaongeza ghasia dhidi yao.

"Inatoa nguvu kwa mtu yeyote ambaye angetaka kufanya kitu kwa watu wa jamii hiyo. Inachochea aina fulani ya vurugu ambazo sasa watu wanapanga lakini wanajizuia," ananiambia.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakenya wengi wanaamini kuwa haki za wapenzi wa jinsia moja ni kinyume na dini yao - iwe ya Kikristo au ya Kiislamu

Ingawa mkutano huo nchini Uganda ulidaiwa kuwa ni jaribio la kulinda "uhuru" wa mataifa ya Afrika, kwa hakika ulifadhiliwa na shirika la mrengo wa kulia la Kikristo la Marekani, Family Watch International (FWI).

Dk Kapya Kaoma, kasisi wa Zambia katika Kanisa la Anglikana na msomi katika Chuo Kikuu cha Boston nchini Marekani, anasema nchi za Afrika zinalengwa na FWI na mashirika kama hayo ya Marekani, na kwamba athari za ushawishi wake zimekuwa "za kutisha na zisizo za kibinadamu" katika sehemu fulani za Afrika, na kuchochea kile anachokiita "chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia".

"Ni jambo moja kusema: 'Sikubaliani na wewe kuwa mpenzi wa jinsia moja', lakini hatukuwa na chuki, ambapo wanasiasa sasa wanasema: 'Unaenda jela maisha, unaenda jela kwa kuzungumza kuhusu kuwa mpenzi wa jinsia moja, unaenda jela kwa sababu unaishi na mwanamke mwenzako," Dk Kaoma anasema.

Hata hivyo, mwanzilishi wa FWI Mormons Sharon Slater anakanusha kuwa kikundi hicho kinaendeleza sheria za kupinga wapenzi wa jinsia moja barani Afrika.

"Family Watch inapinga sheria ambayo inaadhibu mtu kwa jinsi anavyojitambulisha," anasema katika jibu la barua pepe kwa BBC.

Bi Slater alihutubia wabunge wa Afrika, makasisi na wanakampeni katika kongamano lao katika jiji la Ziwa la Uganda la Entebbe mwezi Machi, baadaye alionekana katika picha ya pamoja na Rais Museveni katika makazi yake rasmi.

Kwa zaidi ya miaka 20, Bibi Slater ameshawishi serikali juu ya kile anachokiita "maadili ya familia" na amefanya dhamira yake kufanya kampeni dhidi ya watoto na vijana wanaopewa Elimu Kamili ya Kijinsia (CSE), programu ya elimu ya ngono inayotegemea mtaala unaoendeshwa na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine.

Ananukuu mwongozo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa vijana wasiokwenda shule mashariki na kusini mwa Afrika, akisema unakuza mapenzi ya jinsia moja.

"Inapunguza tamaa watoto kufanya ngono," anasema.

Bibi Slater pia ananukuu kutoka kwa mwongozo huo, ikijumuisha mistari inayosema kwamba wawezeshaji wa masomo wanapaswa kuwa na "mtazamo usioegemea upande wowote, wa kukubali kuhusu mapenzi ya jinsia moja".

Ninapowasiliana na Maria Bakaroudis, mtaalamu wa CSE wa UNFPA kwa Afrika mashariki na kusini, kwa maoni, anasema hana nia ya kuzungumzia "upinzani", anaporejelea FWI.

Anaongeza kuwa mwongozo huo ni mwongozo tu, na kila nchi inaweza kuurekebisha ili kuendana na mazingira yao.

Bi Bakaroudis anatetea CSE, akisema inatoa "taarifa za kuokoa maisha" ili kupunguza viwango vya juu vya mimba zisizotarajiwa, VVU, na magonjwa ya zinaa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ingawa Bw Kaluma alihudhuria mkutano huo nchini Uganda uliofadhiliwa na FWI, anakanusha kufanya kazi na kundi hilo kuhusu mswada wake, ambao anasema utapendekeza kupiga marufuku kufundisha CSE akisema ni sehemu ya "ajenda ya LGBTQ".

"Inasukumwa sana na nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na nchini Kenya. Tutakuwa tunaipiga marufuku kabisa katika mswada huo, ili kuturuhusu kupata elimu ya ngono, ambayo inazingatia umri, maendeleo, na utamaduni unayofaa katika muktadha wetu," anasema.

Bw Kaluma anahoji kuwa "ajenda ya LGBTQ" imekuwa "sekta kubwa, hasa katika nchi za Magharibi" na, licha ya upinzani dhidi yake kutoka kwa baadhi ya raia wao wenyewe, serikali za Magharibi zinataka kuikuza barani Afrika.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Kenya, Kimani Ichung'wah, anaambia BBC kwamba muungano unaotawala Kenya Kwanza hauna msimamo kuhusu sheria inayopendekezwa na Bw Kaluma lakini utawapa wabunge wake uhuru wa kupiga kura wapendavyo iwapo utawasilishwa.

Rais wa Kenya William Ruto hajazungumzia mipango ya Bw Kaluma, lakini alisema mapema mwaka huu kwamba "utamaduni na dini zetu haziruhusu ndoa za watu wa jinsia moja".

Bw Kaluma ana imani kwamba mswada huo utakuwa sheria, jambo linalozua wasiwasi mkubwa katika jumuiya ya LGBTQ nchini Kenya.

Baadhi ya dazeni au zaidi ya watu katika kanisa la Nairobi wananiambia kwamba mapendekezo ya Bw Kaluma si sehemu ya mjadala wa kisiasa tu, bali yanaingia kwenye kiini cha vita vyao, ili kuwepo tu.

"Siwezi kubadili nilivyo. Huyu ni mimi. Sisi pia ni binadamu. Tunafanya kazi yetu. Tunalipa bili. Tunalipa kodi, kwa hivyo wanapaswa kutukubali," mwanamke mmoja aliyebadili jinsia anasema.