'Ngao' ya Kiteknolojia inayoilinda Taiwan dhidi ya China

Mbele ya nchi yenye nguvu kubwa duniani kuna kisiwa kidogo ambacho hakifikii ukubwa wa Cuba.

Taiwan, kilomita 180 tu kutoka Jamhuri ya Watu wa Uchina, inaishi akimtazama adui yake wa milele ambaye inashiriki lugha moja na uwepo wa ndugu kwa pande zote , lakini serikali tofauti za kisiasa.

Upande mmoja wa mlango bahari huo, Beijing inaongoza China ya kikomunisti yenye watu bilioni 1.3 chini ya uongozi wa chama kimoja.

Katika upande mwingine, Taipei inaendesha jamhuri ya kidemokrasia yenye watu milioni 23.

Mzozo kati ya nchi hizo mbili ambao umedumu tangu mwaka 1949 ambao umezidi kuwa mbaya katika siku za hivi karibuni kutokana na ziara ya spika wa bunge la Congress la Marekani, Nancy Pelosi umeinyima Taiwan kupata mashirika ya kimataifa na kuipa hadhi isiyojulikana na utambuzi mdogo wa kimataifa.

Lakini, baada ya miaka mingi ya uhasama na mvutano, Taiwan ilipata mkakati unaosaidia maisha yake ya kitaifa katika mzozo huu usio na usawa na ambayo imeweza kuzuia uvamizi wa Wachina: kinachojulikana kama "ngao ya silicon".

"Silaha" ambayo hakuna mtu anayeweza kuiga kwa muda wa mfupi au mrefu kutokana na kiwango chake cha utata.

Sekta muhimu ambayo inategemea, kutoka kwa utengenezaji wa ndege za kivita hadi paneli za jua au kupitia michezo ya video.

Kabla ya mzozo huu wa hivi punde, BBC Mundo ilikuwa imezungumza na Craig Addison, mwandishi wa habari aliyebuni neno hilo kwa kuchapishwa kwenye kitabu chake Silicon Shield: Ulinzi wa Taiwan dhidi ya Mashambulizi ya Kichina ("Ngao ya silicon: ulinzi wa Taiwan dhidi ya shambulio la China ") .

Tunaweza kuielezeaje ngao ya Silicon?

Ngao ya silicon ni sawa na dhana ya vita baridi ya MAD (mutually assured destruction) yaani maangamizi makubwa ya uhakika, kwa sababu hatua zozote za kijeshi katika Mlango-Bahari wa Taiwan zitakuwa na madhara kwa Uchina kama zilivyo kwa Taiwan na Marekani.

Kwa hivyo, kwa kweli, inazuia mzozo kuanza na kulinda eneo dogo kutokana na shambulio la kijeshi lililoamriwa na Beijing.

Gharama ya hatua hiyo itakuwa kubwa, si kwa dunia pekee, bali kwa China yenyewe, kiasi kwamba serikali ya Xi Jinping ingelazimika kufikiria mara mbili kabla ya kutoa agizo hilo.

Je, kuna mifano yoyote katika historia ya hivi karibuni ya ulinzi huu?

Ukweli kwamba serikali ya China imeshindwa kufuata nia yake iliyoelezwa ya kuchukua Taiwan kwa nguvu ikiwa ni lazima inaonyesha kwamba "ngao ya silicon" inafanya kazi.

Ikiwa Taiwan isingekuwa mtoaji muhimu wa teknolojia kwa ulimwengu, China inaweza kuwa tayari imechukua hatua za kuchukua eneo hilo.

Katika mzozo wa makombora wa Taiwan Strait wa 1996, Marekani ilituma vikundi viwili vya kivita kuzuia mazoezi ya kivita ya China yaliyolenga Taiwan, ambayo ni pamoja na kurusha makombora.

Huu ni mfano maalum wa maslahi yaliyopo ili shambulio lisifanyike.

Kwa hivyo Marekani inaunga mkono upande gani wa mgogoro huu?

Wataalamu wengi wa masuala ya kijeshi wanakubali kwamba China haina uwezo wa kijeshi wa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Taiwan.

Katika ushahidi wake mbele ya Bunge la Marekani mwezi Juni, Jenerali Mark Milley, mwenyekiti wa wakuu wa pamoja wa wafanyakazi, alisema shambulio litakuwa "gumu na la gharama kubwa" kwa China.

Katika kuamua kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Taiwan, China inapaswa pia kuzingatia ikiwa Marekani itaingilia kati kutetea kisiwa hicho.

Ni vigumu kuamini kwamba Marekani ingetulia na kuiacha China iichukue Taiwan kwa nguvu.

Kwanini?

Mbali na usumbufu mkubwa ambao ungetokea kwenye mnyororo wa ugavi wa teknolojia duniani na kwa uchumi wa Marekani wenyewe, uvamizi ungeipa China udhibiti wa viwanda vya juu zaidi vya kutengeneza vifaa maalum vya kompyuta ‘’chip’’ duniani.

Na nchi hii kubwa barani Asia ingekamata silaha za hali ya juu za vita ambazo Washington imeiuzia Taipei kwa miaka mingi.

Je, kuna mtu yeyote anadhani Marekani itakaa kimya na kuruhusu hilo lifanyike?