Masuala gani tete kwenye mkataba mpya wa Marekani, DRC na Rwanda?

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Akiripoti kutoka, BBC Swahili News
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walitia saini makubaliano mapya ya amani tarehe 27 Juni 2025 chini ya mwamvuli wa Marekani.

Makubaliano hayo yanalenga kustawisha amani ya muda mrefu, na kuongezeka kwa biashara ya kiuchumi na usalama.

Baada ya miongo mitatu ya vita na mivutano kati ya majirani hao wawili tangu baada ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi , matumaini ni kwamba makubaliano haya yataweka misingi ya maendeleo ambayo yatayanufaisha mataifa yote mawili.

Kwa Donald Trump ilikuwa ni fursa ya kuonyesha ufanisi wa sera yake ya kigeni, inayolenga mabadilishano na manufaa ya kwa kila mhusika.

Makubaliano yaliyofikiwa na kila taifa

Mwanzoni kabisa maelezo mengi ya makubaliano hayo yalibakia kutojulikana hadi kusainiwa kwake. Kipengele kimoja kilichojitokeza ni madai kwamba DRC iliachana na matakwa yake ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda kutoka katika eneo lake.

Makubaliano ya hivi punde ya amani yanahusu maslahi ya usalama, kisiasa na kiuchumi ya mataifa yote mawili.

Maelezo mahususi ya kina ya mkataba huu hayakuwa wazi . Lakini kulingana na mfumo na ripoti zilizovuja zinaelezea kwamba mataifa yote mawili lazima yaheshimu mamlaka ya eneo la kila mmoja na kuacha kusaidia vikosi vya waasi. Hii itajumuisha uratibu wa pamoja wa usalama, na kufanya kazi na ujumbe uliopo wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya hayo, wakimbizi wa Congo waliokimbia mashariki mwa DRC - wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 80,000 - wataruhusiwa kurejea. Hatimaye, mataifa hayo mawili yataanzisha mbinu za kuimarisha ushirikiano mkubwa wa kiuchumi.

Ni nini hasa kilichomo ndani ya mkataba huu?

Ni mkataba unaojumuisha vifungu tisa muhimu, ambavyo ni:

  • Kutokiuka uhuru wa DRC na Rwanda na kujiepusha na uhasama;
  • Kupokonya silaha, kupokonywa silaha, na kujumuishwa kwa wapiganaji katika jeshi na polisi la DRC kunaweza kutokea kwa kuzingatia masharti fulani;
  • Kuanzisha utaratibu wa pamoja wa ufuatiliaji wa usalama kwa lengo la kulitokomeza kundi la waasi la FDLR linalopambana na serikali ya Rwanda na kukomesha msaada wote wa serikali kwa kundi hilo na makundi mengine yanayohusiana nayo;
  • Kuwarejesha makwao wakimbizi, kuwarekebisha wakimbizi wa ndani na kuwezesha mashirika ya kibinadamu katika shughuli zao chini ya usimamizi wa serikali ya DRC;
  • Kuunga mkono shughuli za ujumbe wa MONUSCO, ikiwa ni pamoja na kujitolea kutekeleza azimio nambari 2773 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ( ambalo pia linaitaka Rwanda kuondoa majeshi yake katika eneo la DRC na kuacha kuunga mkono M23 mara moja na bila kuchelewa, na M23 kusitisha uhasama na kuondoka katika maeneo ambayo imeteka);
  • Ajenda ya biashara ya kiuchumi pia inajumuisha uwazi zaidi kuhusu madini ya thamani;
  • Kuundwa kwa kamati ya kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano hayo na kutatua masuala yoyote yanayoweza kutokea, ikijumuisha mpatanishi wa AU, Qatar na Marekani;
  • Masharti ya mwisho ni pamoja na kwamba mkataba huu utaendelea kwa muda usiojulikana na kwamba unaweza kusitishwa na pande zote mbili (Rwanda na DRC) kwa kutoa taarifa ya miezi sita kwa upande mwingine;
  • Na ukweli kwamba mikataba hii inaanza kutumika mara moja baada ya kusainiwa.
Unaweza pia kusoma:

DRC pia imeonyesha nia yake ya kuvutia wawekezaji wa Marekani. DRC bado ina utajiri mkubwa wa madini ambayo bado yamelala ardhini. Uwekezaji wa Marekani unaweza kuendeleza uchimbaji madini ambao ni salama zaidi na kutoa kiasi kikubwa cha madini kuliko mbinu za sasa. Kinshasa pia imekubali kukabiliana na ufisadi na kurahisisha mfumo wa ushuru.

Ingawa motisha nyingi zinalenga kampuni za uchimbaji madini, pia zinajumuisha kampuni za usalama za kibinafsi. Kushindwa kwa jeshi la Congo kuwashinda M23 'kunaashiria' mazingira yenye matatizo ya usalama ambayo baadhi ya watu nchini DRC wanaamini kuwa yanaweza kushughulikiwa kupitia uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni. Hata hivyo, dhamana hizi za usalama bado hazijulikani kwa kiasi na zinakabiliwa na matatizo ambayo yanaweza kuathiri mafanikio ya makubaliano yoyote.

Katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka 65 ya uhuru wa DR Congo Jumatatu, Rais Félix Tshisekedi makubaliano hayo ni "hatua muhimu ya kumaliza mzozo uliodumu kwa takriban miaka 30 ambao umesababisha mateso mashariki mwa nchi yetu, na kusababisha mamilioni ya vifo na kuhama makazi yao."

Ameyataja kuwa makubaliano "yanayofungua enzi mpya ya utulivu, ushirikiano, na maendeleo kwa nchi yetu, eneo la Maziwa Makuu na bara zima kwa ujumla."

Je makubaliano haya yanaweza kuleta amani?

Ni vigumu kuamini kuwa makubaliano baina ya Trump, DRC na Rwanda yanaweza kuleta amani kutokana masuala mbali mbali.

Kwanza, waasi wa M23 wanaodai kudhibiti eneo la 34,000km² mashariki mwa nchi Congo ukiwemo mji muhimu wa Goma hawakushirikishwa katika mazungumzo baina ya Marekani, serikali ya DRC na Rwanda. Ikizingatiwa kuwa wao ndio wahusika wakuu wa kijeshi mashariki mwa DRC, kujitolea kwao katika mchakato wa amani wa Trump hakuna uhakika.

Tayari Kiongozi wa vuguvugu la AFC/M23 Corneille Nangaa amesema makubaliano ya hivi majuzi yaliyotiwa saini kati ya DRC na Kigali mjini Washington ni "hatua, ambayo haijakamilika, lakini muhimu".

"Kuwadanganya walio ndani na nje ya nchi kuwa hakuna tatizo DRC, kwamba ni tatizo kati ya Kigali na Kinshasa tu itakuwa ni udanganyifu usiovumilika.", alisema katika maadhinisho ya siku ya uhuru wa DRC.

Alisema wanaunga mkono mchakato wa Doha wa mazungumzo kati ya serikali ya Kinshasa na AFC/M23 "kushughulikia chanzo cha tatizo la Congo".

Licha ya M23, DRC pia ni nyumbani kwa mamia ya makundi yenye silaha yanayoendesha vitendo vya uhalifu, ukiwemo ubakaji, na mauaji vilivyopelekea maelfu ya wenyeji kuyakimbia makazi yao, kulingana ripoti za na Umoja wa Mataifa, makundi ambayo wachambuzi wamekuwa wakisema ni vigumu kuyadhibiti.

Pili, vikosi vingine vya waasi katika maeneo tofauti ya nchi vitahisi kutengwa pia. Makundi haya yangeweza kuona makubaliano haya kama fursa ya kushinikiza kupata makubaliano zaidi kutoka kwa serikali ya Congo lakini hilo halikuzingatiwa na mapatano ya Trump.

Tatu, kuna njia chache za kutekeleza makubaliano haya. Tangu Vita vya Pili vya Congo, kumekuwa na mikataba mingi, makubaliano na mipango ya kuyapokonya silaha makundi ya wapiganaji yamekuwa na mafanikio kidogo. Mkataba wa Pretoria kati ya Rwanda na DRC mwaka 2002 haukuleta amani ya muda mrefu.

Uwezo wa serikali ya DRC wa kushughulikia masuala ya miundo mbinu, na udhibiti wa makundi yenye silaha vinatiliwa shaka baada ya historia ndefu ya mizozo ya nchi hiyo.

Kwa upande mwingine wawekezaji wa Marekani wanaweza kuzuiwa na masuala ya usalama, udhibiti na ufisadi ambayo yanayoikumba DRC. Hata kama serikali ya Congo itaahidi kushughulikia masuala haya, historia inaonyesha kuwa haina uwezo unaohitajika kutimiza ahadi yake.

Serikali ya Congo, makundi ya utafiti na Umoja wa Mataifa wameishutumu Rwanda kwa kusambaza msaada wa kijeshi, wakiwemo wanajeshi, kwa vuguvugu la Machi 23 (M23), ambalo limekuwa na vita na serikali mjini Kinshasa tangu mwaka 2021. Serikali ya Rwanda inakanusha kuhusika kwa namna yoyote lakini ina huruma kwa kundi la waasi la Congo.

DRC ina utajiri mkubwa wa madini, ikiwa ni pamoja na dhahabu, almasi, tungsten, coltan, bati na lithiamu na raslimali nyingine zinazoivutia. Si Marekani pekee inayotaka mgawo wa raslimali hizi zenye thamani za DRC, bali pia mataifa mengine ya kigeni ya kikanda na kimataifa. Uchu wa maslahi haya huenda ukaendelea kuchochea uhasama kati yao na kuyumbisha usalama na utulivu wa eneo hilo.

Nini chanzo cha mgogoro?

Baada ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi, wahalifu wa zamani wa mauaji ya kimbari walitumia ukubwa wa DRC kama maficho ya kupanga mashambulizi dhidi ya Rwanda. Walikusudia kurudi Rwanda kumaliza mauaji ya kimbari.

Matokeo yake yalisababisha Vita vya Kwanza vya Congo (1996-1997) na Vita vya Pili vya Congo (1998-2003).

Ilikuwa ni wakati wa vita vya pili vya umwagaji damu ambapo DRC ilikumbwa na makundi mengi ya waasi yaliyoungana na mataifa mbalimbali na wahusika wa kisiasa.

Umoja wa Mataifa unazituhumu Rwanda na Uganda kwa kufanya biashara haramu ya madini. Mataifa yote mawili yanakataa hili .

Matokeo ya mzozo bado yanaonekana zaidi ya miaka 20 baadaye. Licha ya makubaliano mengi ya amani, na upokonyaji silaha, uondoaji watu na programu za kuwajumuisha tena, inakadiriwa vikundi 120 vya waasi vinasalia amilifu nchini Congo.

Miongoni mwa makundi hayo ni Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) , wapiganaji wanaolenga kuung'oa madarakani utawala wa kigalii. Serikali ya Rwanda inahofia mauaji ya halaiki ya kundi hilo na itikadi za chuki.

Zaidi ya hayo, FDLR na makundi mengine yenye itikadi kali kama vile Wazalendo wanawalenga Watutsi Wacongo wanaozungumza Kinyarwanda. Kabila hili, linaloishi hasa mashariki mwa DRC, lina uhusiano wa kihistoria na Rwanda.

FDLR Iimekuwa likiendesha mashambulizi, ambayo yamewalazimu makumi ya maelfu ya watu kukimbilia Rwanda.

Mashambulizi haya yalisababisha kufufuka kwa M23. Licha ya kushindwa kwake mwaka wa 2013 , M23 ilipata mafanikio makubwa mwishoni mwa 2021 katika kukabiliana na mashambulizi dhidi ya Banyarwanda. Kundi hilo la waasi liliongoza kampeni ya kijeshi yenye mafanikio ambayo iliteka maeneo makubwa mashariki mwa DRC.

Jina la M23 linaashiria hasira yao juu ya makubaliano yaliyofeli ya 2009. Mwaka 2024, Rwanda na Congo zilikuwa karibu kufikia makubaliano chini ya upatanishi wa Angola , lakini Angola ilijiondoa . Mchakato huo ulichukuliwa na Qatar na baadaye Marekani.

DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwaunga mkono wapiganaji wa vuguvugu la M23, na kupora madini ya DRC , shutuma ambazo zimekuwa zikipingwa vikali na Rwanda, ambayo pia imekuwa ikiishutumu DRC kushirikiana na wapiganaji wa FDLR wenye nia ya kuendeleza mauaji ya kimbari nchini Rwanda. DRC inapinga hilo.

Kwa kusaini makubaliano yanayosimamiwa na Marekani DRC na Rwanda zinataka kuuonyesha utawala wa Trump nia yao ya kujadiliana na kufanya makubaliano, huku Marekani ikijionyesha kama mpatanishi anayeleta amani ya DRC na jirani yake Rwanda...lakini je, hayo yote kufikiwa?

Unaweza pia kusoma:

Imehaririwa na Yusuph Mazimu