Wasyria wanaoomba uraia wa Israeli wanahisi hawako salama tena

- Author, Feras Kilani
- Nafasi, Special correspondent, BBC News Arabic
- Akiripoti kutoka, Occupied Golan Heights
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Sijihisi salama tena," anasema Laith Abu Saleh. Mbele yake, mezani sebuleni mwake, kuna mpira wa miguu ulioandikwa majina na picha za watoto 12.
Wote waliuawa katika shambulio la anga mnamo Julai 2024. Mmoja wao alikuwa mwanawe wa miaka 15, Fajr. Mwingine alikuwa mpwa wake Hazem, ambaye pia alikuwa na umri wa miaka 15.
Watoto hao walikuwa wakicheza mpira wa miguu huko Majdal Shams katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israeli wakati roketi ilipopiga uwanja.
Israel ilishutumu kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran kwa kutekeleza shambulio hilo.
Hezbollah ilikana hili, lakini karibu wakati roketi hiyo ilipotua, vyombo vya habari vyake vilitangaza kwamba ilikuwa imerusha roketi kuelekea kambi ya kijeshi ya Israeli iliyo chini ya maili mbili kutoka uwanja wa mpira wa miguu.
Israeli iliteka Milima ya Golan kusini-magharibi mwa Syria mnamo 1967 na kuinyakua kwa upande mmoja mnamo 1981, hatua ambayo haikutambuliwa kimataifa, ingawa utawala wa Trump wa Marekani ulifanya hivyo mnamo 2019.
Raia wa Syria waliozaliwa hapa hupewa hati za Israeli za ukazi wa kudumu, watu tuliozungumza nao walisema kwamba kupata hati mpya au zilizosasishwa za Syria imekuwa vigumu tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mnamo 2011.

Chanzo cha picha, Laith Abu Saleh
Mnamo Desemba 2024, miezi michache baada ya mwanawe kuuawa, Abu Saleh alichukua uamuzi mkubwa, aliomba uraia kamili wa Israeli. "Napendelea kuwa upande wenye nguvu zaidi unaoweza kunilinda," anaelezea.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Yeye ni mmoja wa watu wanaozidi kuchukua njia hii. Majdal Shams ni mojawapo ya vijiji vinne, ambavyo kwa pamoja vina wafuasi wapatao 26,000 wa kikundi cha kidini na kikabila cha Druze kinachozungumza Kiarabu. Druze wengi wanaishi Syria, Israel na Lebanon na imani yao ni tawi la Uislamu wa Shia, wenye utambulisho na imani zake za kipekee.
Takribani Waisraeli 20,000 pia wanaishi katika Milima ya Golan katika makazi ambayo yanachukuliwa kuwa kinyume cha sheria chini ya sheria ya kimataifa, ingawa Israeli inapinga hili.
Katika mwaka uliopita, idadi ya Druze wa Syria katika Milima ya Golan wanaoomba uraia wa Israeli iliongezeka sana.
Mnamo 2025, ilikuwa 2,540, juu zaidi kuliko miaka mitano iliyopita kwa pamoja, na karibu mara tano zaidi kuliko mwaka 2024 ilipokuwa 550, kulingana na takwimu kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani ya Israeli.
Hapo awali, Wadruze wengi katika Milima ya Golan walikataa kuomba uraia wa Israeli.
Israeli ilipotumia sheria zake katika Milima ya Golan mnamo 1981, hatua hiyo ilikabiliwa na maandamano ya hasira.
Wakati huo, viongozi wa jamii ya Wadruze waliandika hati inayoelezea kujitolea kwao kwa utambulisho wao wa Syria, wakiahidi kususia kidini na kijamii kwa mtu yeyote aliyekubali uraia wa Israeli.
Hayel Abu Jabal, mmoja wa watu watano walioiandika, anasema kwamba tangu wakati huo, wakazi wachache walioomba walilazimika kufanya hivyo ili kusafiri na kushirikiana na ulimwengu.
Hapo awali, maombi yalikuwa machache na kwa kiasi kikubwa yalifanywa kwa siri, lakini hii imeanza kubadilika na sasa 32% ya Wadruze katika Milima ya Golan wana uraia wa Israeli, kulingana na takwimu za Israeli.

Kwa Abu Saleh, shambulio lililomuua mwanawe lilikuwa sababu muhimu ya kufanya uamuzi wake. Baada ya kengele kuwashwa, watoto walikuwa wakihamishiwa kwenye makazi, lakini roketi ilipiga kabla hawajafika huko. Mwanawe alikuwa tayari amekufa Abu Saleh alipofika.
Abu Jabal anasema kwamba kuanguka kwa Rais wa zamani wa Syria Bashar al-Assad na matukio ya baadaye katika jiji la Syria la Suweida pia yamechangia hali ya hofu katika jamii ya Druze ya Golan, na kusababisha maombi zaidi ya "ulinzi" badala ya hamu ya "kuwa Mwisraeli".
Maryam, si jina lake halisi, anasema aliomba uraia pamoja na mumewe na watoto wake wawili mnamo Machi 2025. Alitaka kubaki bila kujulikana kwa sababu bado hajaiambia familia yake kubwa.
Anasema alikuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa kuondolewa kwa Bashar al-Assad, lakini hakuwahi kufikiria kwamba mbadala wake angekuwa "gaidi, hii ilibadilisha sana mtazamo wangu ... Siwezi kuona hii kama nchi, angalau sio kwa sasa".

Chanzo cha picha, Turkish Foreign Ministry/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Rais mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, aliwahi kuwa mkuu wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu, Hayat Tahrir al-Sham (HTS). Kundi hilo hapo awali lilijulikana kama al-Nusra Front - wakati huo lilikuwa mshirika wa al-Qaeda nchini Syria, lakini al-Sharaa ilikata uhusiano mwaka 2016.
Mnamo Desemba 2024, baada ya kujibadilisha, al-Sharaa iliongoza kukamatwa kwa mji mkuu wa Syria, Damascus na kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo.
Katika siku zilizofuata, Israeli ilihamisha vikosi vyake vya ardhini mashariki kutoka Milima ya Golan hadi eneo la ulinzi lisilo la kijeshi nchini Syria. Ilichukua udhibiti wa miji kadhaa ya Druze kando ya barabara inayoelekea kwenye kilele cha Mlima Hermon, nafasi muhimu ya kimkakati huku Damascus ikionekana kutoka kileleni.
Israel inataka kuanzisha eneo lisilo la kijeshi linalojumuisha majimbo yote ya kusini mwa Syria ya Suweida, Deraa na Quneitra mashariki mwa Milima ya Golan, ambayo Syria inapinga, ikitaka vikosi vya Israeli viondoke mara moja kwenye nafasi walizokuwa nazo kabla ya kuanguka kwa utawala wa Assad.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameahidi mara kwa mara kutetea kundi la wachache la Druze nchini Syria na Maryam anaamini Israeli itatoa ulinzi mkubwa zaidi kwa jamii yake kuliko serikali ya Syria.
Anasema kwamba matukio katika jiji la Suweida lenye wakazi wengi wa Druze katika msimu wa joto wa 2025 yanaunga mkono mtazamo huu. Mnamo Julai, mvutano wa muda mrefu kati ya makabila ya Druze na Bedouin ulizuka na kuwa mapigano makali ya kidini huko.

Chanzo cha picha, BBC/Jon Donnison
Vikosi vya serikali ya Syria vilitumwa lakini vilishutumiwa kwa kushambulia wapiganaji wa Druze na raia, jambo lililosababisha jeshi la Israeli kuingilia kati na mfululizo wa mashambulizi ya angani ambayo ilisema yalikusudiwa kuwalinda Druze.
Kwa ujumla, zaidi ya watu 1,000 waliuawa huko Suweida. Maryam anaamini kwamba "Syria si nchi ya asili tena".
Hofu ya mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa jihadi pia iko akilini mwa jamii, na hii imewafanya baadhi ya vijana wa Druze kufanya uamuzi tata wa kujiunga na jeshi la Israeli baada ya kupata uraia.
Mkuu wa baraza la mitaa la Majdal Shams, Dolan Abu Saleh, anasema ni suala la kujilinda. Imekuwa jambo la kawaida kuwaona wanaume wa Druze wakiwa doria nje kidogo ya miji katika Milima ya Golan, wakiwa wamevaa sare na kubeba silaha.
Jeshi la Israeli halifichui idadi ya Druze wa Syria wanaohudumu katika safu zake, wala idadi ya wale waliotuma maombi.
Licha ya ukweli kwamba baadhi wamejiandikisha, Hayel Abu Jabal anaamini utumishi wa wanaume wa Druze katika jeshi la Israeli "hauwanufaishi watu wa Golan na mapambano yao" na kwamba Netanyahu "anataka tu kuimarisha mgawanyiko miongoni mwa sehemu mbalimbali za jamii ya Syria".
Yeye na viongozi wengine wa Druze wanashikilia msimamo wao kwamba "Golan ni ya Kiarabu na ya Syria".

BBC iliiomba serikali ya Syria itoe maoni yake kuhusu ongezeko la maombi ya uraia wa Israeli, masuala ya usalama yaliyoibuliwa na wakazi katika Milima ya Golan na kama ilikuwa imeanzisha mawasiliano yoyote nao. Haikujibu.
Zaidi ya mwaka mmoja baada ya kifo cha mwanawe, Laith Abu Saleh anatuonesha chumba cha kijana huyo, ambapo shati la mpira la Cristiano Ronaldo lililosainiwa ambalo lilikuwa la mvulana huyo bado linaning'inia. Alikuwa mwanafunzi mzuri, na "aliishi kwa ajili ya kucheza michezo" anasema.
Anasubiri kusikia kama maombi yake ya kuwa raia wa Israeli yataidhinishwa. Anasema anaona uraia kama "suala la uhuru wa binafsi".
"Mali yetu ni ya ardhi, na uraia haubadilishi ardhi," anasema. "Lakini tunahitaji utambulisho. Tumeishi kwa miongo kadhaa bila kujua kama sisi ni Wasyria au Waisraeli, na vizazi vilivyozaliwa tangu uvamizi vinasema, 'Siwezi kuishi isipokuwa mimi ni sehemu ya jimbo hili [la Israeli].'"
Wazo lake la kuaga "kwa kila mama na baba, awe Druze, Mkristo, Mwislamu, au chochote kile", ni "kumlea mtoto wako aishi, si afe".
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












