Moja kwa moja, Marekani yakataa msamaha wa Jenerali Muhoozi wa Uganda

Kwa mujibu wa Seneta Risch, mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Marekani yakataa msamaha wa Jenerali Muhoozi wa Uganda

    .

    Chanzo cha picha, X

    Seneta wa Marekani Jim Risch, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, amekataa msamaha wa umma uliotolewa na Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Uganda, akiutaja kuwa usio na maana na usiojitosheleza huku akitoa wito wa kutaka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Uganda.

    Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Januari 30, Risch alisema Muhoozi, mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amevuka mstari mwekundu licha ya kufuta ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii na kuomba msamaha kwa Marekani.

    Kwa mujibu wa mwenyekiti, Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.

    Seneta wa Marekani aliongeza kuwa nchi yake "haitavumilia hali ya mashaka kiwango hiki na uzembe".

    Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda ulihusika kumsaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi alisema:

    "Wananchi wenzangu wa Uganda, kutokana na hali ya sasa ambapo kiongozi wa upinzani amejiteka mwenyewe na kutoweka, na kwa mujibu wa taarifa zetu bora za kijasusi, vitendo hivi vilifanyika kwa ushirikiano na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini mwetu. Kwa sababu hiyo, UPDF imesitisha ushirikiano wote na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani jijini Kampala. Hii inajumuisha pia ushirikiano wetu nchini Somalia. Ushirikiano wa kiusalama uliokuwa wa thamani kubwa kati ya Uganda na Marekani umeathiriwa vibaya tangu mwaka 2015 na watendaji wa urasimu wasio na ubunifu katika ubalozi huo".

    Baadaye, Jenerali Muhoozi alifuta ujumbe huo na kutoa radhi kwa kauli zake.

    Soma zaidi:

  2. Jenerali Muhoozi wa Uganda aomba msamaha kwa kuilaumu Marekani kwa kusaidia upinzani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, ameomba msamaha kwa Marekani kwa matamshi yake ya awali kwenye mitandao ya kijamii ambayo yalikuwa yametilia shaka ushirikiano wa kijeshi unaoendelea kati ya Kampala na Marekani.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X Ijumaa asubuhi, Jenerali Kainerugaba alisema alikuwa amefuta machapisho yake ya awali baada ya kubaini kuwa taarifa alizotegemea hazikuwa sahihi.

    Aliongeza kwamba amezungumza moja kwa moja na Balozi wa Marekani nchini Uganda na kuthibitisha kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili bado uko sawa.

    "Nataka kuomba msamaha kwa marafiki zetu wakubwa Marekani kwa ujumbe wangu wa Twitter wa awali ambao sasa nimeufuta," Kainerugaba aliandika.

    "Nilipewa taarifa zisizo sahihi. Nimezungumza na Balozi wa Marekani nchini mwetu na kila kitu kiko sawa. Tutaendelea na ushirikiano wetu wa kijeshi kama kawaida."

    Ujumbe wa Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mwana wa Rais Yoweri Museveni na Kiongozi wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Uganda (UPDF), ulilaumu Ubalozi wa Marekani nchini Uganda kwa madai ya kumficha kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine.

    Kyagulanyi alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa Januari 15, baada ya Rais Museveni, baba yake Jenerali Muhoozi, kutangazwa mshindi kwa ushindi mkubwa.

    Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda ulihusika kumsaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026.

    Soma zaidi:

  3. UN ipo katika hatari ya 'kuporomoka kifedha' - Guterres

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la Umoja wa Mataifa linakabiliwa na tishio la 'kuporomoka kiuchumi' kutokana na mataifa wanachama kukosa kulipa ada zao kwa shirika hilo.

    Katibu Mkuu wa Mmoja wa Mataifa António Guterres, amesema shirika hilo linakumbwa na uhaba wa fedha, hali ambayo inahatarisha utoaji wa huduma, na fedha walizonazo huenda zikaisha ifikiapo mwezi Julai.

    Guterres aliwaandikia mabalozi wa mataifa wanachama 193 akiwataka kuheshimu wajibu wao wa kutoa malipo kwa shirika hilo, ili kuizuia kuporomoka kwake.

    Tangazo hili linakuja baada ya taifa la Marekani ambalo lililokuwa mfadhili mkubwa wa shirika hilo kukataa kufadhili miradi ya kudumisha amani inayoendeshwa na umoja wa mataifa na kujiondoa kwa mashirika mengine kwa madai ya "kuharibu pesa za walipa kodi".

    Wanachama wengine kadhaa pia wana madeni au wanakataa tu kulipa.

    Guterres amesema umoja wa mataifa awali imekumbwa na uhaba wa fedha ila kwa sasa hali imekuwa mbaya zaidi.

    Ingawa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mabadiliko ya sehemu katika mfumo wake wa kifedha mwishoni mwa mwaka 2025, shirika hilo bado linakabiliwa na upungufu mkubwa wa kifedha unaozidishwa na sheria inayomaanisha kuwa linarejesha pesa ambazo halijawahi kupokea.

    Katika makao makuu yake mjini Geneva, mabango ya onyo kuhusu hali hiyo yamewekwa kila mahali.

    Katibu huyo aliongezea kuwa ufanisi wa mfumo wa UN, unatokana na mataifa wanachama kuheshimu wajibu wao wa kisheria chini ya mkataba wa umoja wa mataifa, na kuongeza kuwa mwisho wa mwaka 2025, 77% ya malipo hayakuwa yametolewa na mataifa wanachama kwa shirika hilo.

    "Siwezi kusisitiza vya kutosha kuhusu dharura ya hali tuliyonayo kwa sasa. Hatuwezi tekeleza bajeti zetu bila fedha kutoka mataifa wanachama, na hatuwezi rudisha fedha ambazo hatujawahi kupokea."

    "Sijui nielezee vipi dharura ya hali tuliyonayo kwa sasa. Hatuwezi kutekeleza bajeti zetu bila fedha, wala kurudisha fedha ambazo hatujawahi kupokea kamwe".

    Mwezi Januari, Marekani ilijiondoa kutoka mashirika tofauti ikiwemo 31 ya umoja wa mataifa.

    Soma zaidi:

  4. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 31/01/2026.