Vita vya Ukraine: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni nini na linafanya kazi vipi?

Chanzo cha picha, Reuters
Umoja wa Mataifa ulianzia kutoka kwenye majivu ya Vita vya Pili vya Dunia kuleta nchi kote ulimwenguni Pamoja kusuluhisha maswala ya ulimwengu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lilikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1946, ni chombo muhimu kilichopewa jukumu la kuhakikisha amani na usalama duniani kote.
Kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Rais Volodymyr Zelensky ametoa hotuba yenye hisia kali kwa baraza hilo akiitaka "kuchukua hatua mara moja" kukomesha hatua za kijeshi za Urusi.
Lakini jinsi shirika linavyofanya kazi imefanya iwe vigumu kwake kuchukua hatua wakati wa matukio ya kimataifa.
Wanachama wake 15 - watano wa kudumu na kumi wasio wa kudumu - wana uwezo wa kuweka vikwazo au kuidhinisha matumizi ya nguvu kudumisha au kurejesha amani na usalama wa kimataifa.
Lakini mara nyingi, maamuzi madhubuti hayawezi kuchukuliwa kwa sababu yanapigiwa kura ya turufu na wanachama wa kudumu ambao wana maoni yanayoshindana kuhusu masuala ya kimataifa.
Kwa hivyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya kazi vipi?
Wanachama wa kudumu
Mataifa matano yanawakilishwa kwa kudumu kwenye Baraza la Usalama: Marekani, Uingereza, Uchina, Urusi na Ufaransa.
Haya ndiyo mamlaka yaliyokuwa yakitawala katika kipindi kilichofuatia kushindwa kwa Ujerumani na Japan katika Vita vya Pili vya Dunia, wakati baraza hilo lilipoundwa.
Utunzi huu haujabadilika tangu mwaka 1946, ingawa ulijirekebisha kwa hali halisi mpya ya kijiografia.
Kiti cha China hapo awali kilishikiliwa na serikali ya kitaifa inayoongozwa na Chiang Kai-shek.
Baada ya mapinduzi ya mwaka 1949, serikali yake ilirejea kisiwa cha Taiwan lakini ilikuwa hadi mwaka 1971 ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kubadili umiliki wa kiti hicho kwa Jamhuri ya Watu wa Kikomunisti wa China (PRC).
Kiti cha Urusi hapo awali kilishikiliwa na Umoja wa Kisovieti hadi kufutwa kwake mnamo mwaka 1991.
Haki ya kura ya turufu
Jambo muhimu kuhusu wanachama hawa watano wa kudumu ni kwamba wanaweza kupinga uamuzi wowote unaojadiliwa na baraza.
Ina maana kwamba ikiwa mmoja wao atapiga kura dhidi ya azimio hilo, haliwezi kupitishwa.
Hata hivyo, azimio linaweza kupitishwa ikiwa mwanachama wa kudumu hatapiga kura.
Hili ni muhimu hasa wakati nchi zilizo na mamlaka ya kura ya turufu zinahusika moja kwa moja au isivyo moja kwa moja katika mzozo, kama vile vita vya sasa vya Ukrainia.
Hakuna kanuni ya kuzuia aina hii ya mgongano wa kimaslahi.

Chanzo cha picha, Reuters
Mnamo mwaka 2020, zaidi ya nchi 100 ziliunga mkono pendekezo la Franco-Mexican la kudhibiti matumizi ya mamlaka ya kura ya turufu.
Kulingana na pendekezo hili, wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama wangejitolea kwa hiari na kwa pamoja kuacha kutumia kura ya turufu pale ambapo "unyama mkubwa" ulifanyika.
Nchi zingine, kama Uhispania, zimetoa wito wa kuondoa mamlaka ya kura ya turufu kabisa.
Wanachama wasio wa kudumu
Nchi kumi huchaguliwa kila baada ya miaka miwili kuwa wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinazowakilishwa katika Baraza Kuu zinaweza kupiga kura.
Lengo ni kufikia usawa wa kikanda, na wanachama watano wa Asia au Afrika, wanachama wawili wa Amerika ya Kusini, mmoja wa Ulaya mashariki, na wanachama wawili kutoka Ulaya magharibi au mikoa mingine inayounda mchanganyiko wa wanachama wasio wa kudumu.
Kufikia Aprili 2022, wanachama wasio wa kudumu ni India, Ireland, Kenya, Mexico na Norway, ambao mamlaka yao yanamalizika tarehe 31 Desemba mwaka huu, na Albania, Brazil, Gabon, Ghana, na UAE, ambao mamlaka yao yanaisha 2023.
Mataifa yanashindana kwa hamu kubwa ya uanachama wa baraza, pengine kwa sababu ya heshima iliyoambatanishwa, au nafasi ya kuibua suala ambalo ni la manufaa ya taifa.
Baadhi ya nchi hutangaza kugombea kwao miaka mingi mapema na kujitokeza kutafuta kura.
Kila mwanachama wa Baraza la Usalama - wa kudumu au vinginevyo - anashikilia urais wa baraza hilo kwa muda wa mwezi mmoja, kwa msingi wa zamu.
Kupanuka
Lakini nchi ambazo nguvu zao zimeongezeka katika miaka 75 iliyopita zimekuwa wakosoaji vikali wa muundo wa Baraza la Usalama, wakisema kuwa sio mwakilishi tena wa ulimwengu wa nchi nyingi.
Kikundi cha kazi kuhusu mageuzi kilichoanzishwa chini ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1993 kimefanya maendeleo kidogo kuhusu suala hilo, na kukosekana kwa maafikiano kuhusu wagombea wanaotarajiwa.
India, Ujerumani, Japan na Brazil - inayojulikana kama G4 - na Umoja wa Afrika ni miongoni mwa wale ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishawishi kwa kutamaniwa kuwa mwanachama wa kudumu.

Wakati wa mijadala katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka jana, wawakilishi wa G4 walitoa wito wa kufanya kazi ili "kuweka maisha mapya katika majadiliano".
Walikubaliana kwamba baraza "lazima liakisi vyema hali halisi ya kijiografia na siasa za kisasa, na uwakilishi mkubwa kwa Asia, Afrika na Amerika Kusini".
Kile kinachoitwa Msimamo wa Pamoja wa Afrika, unaotaka kuwepo kwa Baraza la Usalama la "uwakilishi zaidi na wa kidemokrasia", uliwekwa katika matamko mawili mwaka 2005: Makubaliano ya Ezulwini na Azimio la Sirte.
Marehemu ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan alionya kutokuwepo kwa mageuzi kunaweza kudhoofisha msimamo wa baraza hilo duniani.
Kuchukua hatua
Baraza la Usalama linatilia maanani umuhimu mkubwa kuzuia migogoro ya kivita kwanza.
Lakini mara tu mzozo unapopamba moto, lengo lake la kwanza ni kutafuta suluhu la kidiplomasia.
Ikiwa mzozo utaendelea, Baraza la Usalama linaweza kufanyia kazi usitishaji mapigano na kupeleka walinda amani.
Inaweza kuamuru mataifa ya Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo na, kama hatua ya mwisho, inaweza kuidhinisha hatua za kijeshi dhidi ya mvamizi.
Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatakiwa kuzingatia maamuzi ya Baraza la Usalama.

Chanzo cha picha, Reuters
Ukosoaji
Baraza la Usalama limekosolewa kwa kutochukua hatua hadi janga litokee - hata wakati lingetarajiwa, kama vile mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994.
Kuchelewa kwa mchakato wa kufanya maamuzi na nguvu ya kura ya turufu ina maana kwamba mataifa na miungano wakati mwingine huchukua kile wanachodai kuwa ni hatua halali za kijeshi bila kibali.
Kampeni ya kulipua mabomu ya Nato dhidi ya Yugoslavia mwaka 1999 ilifanyika bila idhini ya baraza.
Nchi za Nato - na hasa Marekani chini ya rais Bill Clinton - zilidai hatua hiyo ya upande mmoja ilikuwa ya haki katika kujibu tuhuma za mauaji ya halaiki ya wakazi wa Kosovo wa Albania na vikosi vya Yugoslavia.
Urusi ilisema kuwa shambulio hilo la bomu bila idhini ya Baraza la Usalama badala yake lilichangia mzozo huo.
Uvamizi wa Marekani na Uingereza nchini Iraq mwaka 2003 pia uliendelea bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio nambari 1441, lililopitishwa na baraza hilo, liliitaka Iraq kunyanganya silaha na kushirikiana na wakaguzi wa silaha.
Lakini baadhi ya wanachama wa kudumu, ikiwa ni pamoja na Ufaransa na Urusi, hawakukubaliana na madai ya Marekani-Uingereza kwamba 1441 iliruhusu hatua za kijeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika hali nyingine, Baraza la Usalama limechukua hatua madhubuti zaidi.
Kati ya mwaka 2006 na 2015, iliweka vikwazo vya teknolojia ya nyuklia vinavyohusiana na silaha kwa Iran juu ya mpango wake wa nyuklia.
Tangu mwaka 2006, pia ilipitisha takriban maazimio kadhaa dhidi ya Korea Kaskazini kuhusu mpango wake wa silaha za nyuklia.
Wanalenga uuzaji wa silaha na zana za kijeshi, kuzuia ushirikiano wa kisayansi na kuwawekea vikwazo watu wanaohusika katika mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.
Mnamo mwaka 2001, iliidhinisha eneo lisilo na ndege juu ya Libya ambayo ilisaidia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuangusha serikali ya Gaddafi.
Hata hivyo, makosa ya Vita Baridi yanavumiliwa.
Mwaka 2012, Urusi na China zilipiga kura ya turufu mfululizo wa maazimio ya Baraza la Usalama yenye lengo la kuweka shinikizo kwa utawala wa Syria wa Rais Bashar al-Assad - mshirika mkuu wa Urusi katika Mashariki ya Kati.
Na sasa azimio lolote lililopendekezwa lililowekwa mbele ya Baraza la Usalama dhidi ya Urusi juu ya uvamizi wake Ukraine ni lazima kupigiwa kura ya turufu na Urusi yenyewe.












