Moja kwa moja, Marekani yakataa msamaha wa Jenerali Muhoozi wa Uganda
Kwa mujibu wa Seneta Risch, mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.
Mtangazaji wa zamani wa CNN ashtakiwa juu ya maandamano ya kupinga maafisa wa uhamiaji Minnesota
Chanzo cha picha, Kevin Mazur/Getty Images
Mtangazaji
wa zamani wa CNN, Don Lemon, amefikishwa mbele ya jaji baada ya kukamatwa kwa
kuingia kanisani huko Minnesota na kupiga picha za waandamanaji wanaopinga
uhamiaji walipokuwa wakivuruga ibada.
Baada ya
kufikishwa mahakamani, Lemon aliachiliwa kutoka kizuizini. Aliwaambia waandishi
wa habari nje kwamba alikamatwa kwa kuripoti habari hizo, akiongeza kuwa:
"Sitanyamazishwa."
Idara ya
Usalama wa Nchi (DHS) ilisema alishtakiwa kwa "njama ya kunyima wengine haki"
na "ukiukaji wa Sheria ya FACE", kwa madai ya kuingilia haki za wengine
kwa kutumia nguvu.
Lemon
aliingia Cities Church huko St Paul mnamo tarehe 18 Januari akiwa na
waandamanaji waliosema mmoja wa wachungaji alikuwa afisa wa utekelezaji wa
sheria za uhamiaji.
Trump asema Iran inataka kufikia makubaliano badala ya kukabiliwa na hatua za kijeshi
Chanzo cha picha, EPA
Rais Donald
Trump amesema Iran inataka kufikia makubaliano badala ya kukabiliana na hatua
za kijeshi za Marekani, licha ya Tehran kusisitiza kwamba mifumo yake ya
makombora na ulinzi "haitawahi" kujadiliwa.
"Naweza
kusema hivi, wanataka kufanya makubaliano," Trump aliwaambia waandishi wa
habari katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa alipoulizwa kuhusu mkusanyiko
wa vikosi vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba, bila kutoa maelezo
zaidi.
Alikuwa
ameionya Tehran siku ya Jumatano kwamba muda ulikuwa "unayoyoma"
kujadili makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia baada ya meli kubwa za
majini za Marekani kukusanyika karibu na nchi hiyo.
Waziri wa
mambo ya nje wa Iran alisema hakuna mazungumzo yaliyopangwa na Marekani kwa
sasa lakini kwamba Iran iko wazi kwa mazungumzo yanayotegemea "heshima ya
pande zote" na uaminifu.
Pia siku ya
Ijumaa, Kremlin ilisema mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran Ali
Larijani alikuwa amekutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Walijadili
"masuala ya Mashariki ya Kati na kimataifa" miongoni mwa mambo
mengine, shirika la habari la serikali Ria-Novosoti liliripoti.
Iran
inasisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani kabisa na imekanusha mara
kwa mara shutuma kutoka kwa Marekani na washirika wake kwamba inatafuta
kutengeneza silaha za nyuklia.
Alipoulizwa
Ijumaa kama alikuwa ameipa Tehran tarehe ya mwisho ya kufikia makubaliano,
Trump alisema kwamba "hakika ni wao tu wanaojua".
Aliwaambia
waandishi wa habari: "Natumaini tutafanya makubaliano. Tukifanya
makubaliano, hilo ni jambo zuri. Tusipofanya makubaliano, tutaona
kitakachotokea."
Marekani yakataa msamaha wa Jenerali Muhoozi wa Uganda
Chanzo cha picha, X
Seneta wa Marekani Jim Risch, ambaye pia ni mwenyekiti wa
Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, amekataa msamaha wa umma uliotolewa na
Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Uganda, akiutaja kuwa usio na maana na
usiojitosheleza huku akitoa wito wa kutaka vikwazo vikali zaidi dhidi ya
Uganda.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Januari 30, Risch
alisema Muhoozi, mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amevuka mstari mwekundu licha
ya kufuta ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii na kuomba msamaha kwa
Marekani.
Kwa mujibu wa mwenyekiti, Marekani itatathmini upya
ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi
na Uganda.
Seneta wa Marekani aliongeza kuwa nchi yake
"haitavumilia hali ya mashaka kiwango hiki na uzembe".
Jenerali
Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu
za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda
ulihusika kumsaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya
Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026.
Katika
ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi
alisema:
"Wananchi wenzangu wa Uganda, kutokana na hali ya sasa ambapo kiongozi wa
upinzani amejiteka mwenyewe na kutoweka, na kwa mujibu wa taarifa zetu bora za
kijasusi, vitendo hivi vilifanyika kwa ushirikiano na uongozi wa sasa wa
Ubalozi wa Marekani nchini mwetu. Kwa sababu hiyo, UPDF imesitisha ushirikiano
wote na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani jijini Kampala. Hii inajumuisha
pia ushirikiano wetu nchini Somalia. Ushirikiano wa kiusalama uliokuwa wa
thamani kubwa kati ya Uganda na Marekani umeathiriwa vibaya tangu mwaka 2015 na
watendaji wa urasimu wasio na ubunifu katika ubalozi huo".
Baadaye,
Jenerali Muhoozi alifuta ujumbe huo na kutoa radhi kwa kauli zake.
Jenerali Muhoozi wa Uganda aomba msamaha kwa kuilaumu Marekani kwa kusaidia upinzani
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, ameomba msamaha kwa Marekani kwa
matamshi yake ya awali kwenye mitandao ya kijamii ambayo yalikuwa yametilia
shaka ushirikiano wa kijeshi unaoendelea kati ya Kampala na Marekani.
Katika
taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X Ijumaa asubuhi, Jenerali Kainerugaba
alisema alikuwa amefuta machapisho yake ya awali baada ya kubaini kuwa taarifa
alizotegemea hazikuwa sahihi.
Aliongeza
kwamba amezungumza moja kwa moja na Balozi wa Marekani nchini Uganda na
kuthibitisha kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili bado uko sawa.
"Nataka
kuomba msamaha kwa marafiki zetu wakubwa Marekani kwa ujumbe wangu wa Twitter
wa awali ambao sasa nimeufuta," Kainerugaba aliandika.
"Nilipewa
taarifa zisizo sahihi. Nimezungumza na Balozi wa Marekani nchini mwetu na kila
kitu kiko sawa. Tutaendelea na ushirikiano wetu wa kijeshi kama kawaida."
Ujumbe wa Jenerali
Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mwana wa Rais Yoweri Museveni na Kiongozi wa
Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Uganda (UPDF), ulilaumu Ubalozi wa
Marekani nchini Uganda kwa madai ya kumficha kiongozi wa upinzani, Robert
Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine.
Kyagulanyi
alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa Januari 15, baada ya Rais
Museveni, baba yake Jenerali Muhoozi, kutangazwa mshindi kwa ushindi mkubwa.
Jenerali
Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu
za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda
ulihusika kumsaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya
Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026.
UN ipo katika hatari ya 'kuporomoka kifedha' - Guterres
Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la
Umoja wa Mataifa linakabiliwa na tishio la 'kuporomoka kiuchumi' kutokana na
mataifa wanachama kukosa kulipa ada zao kwa shirika hilo.
Katibu Mkuu
wa Mmoja wa Mataifa António Guterres, amesema shirika hilo linakumbwa na uhaba
wa fedha, hali ambayo inahatarisha utoaji wa huduma, na fedha walizonazo huenda
zikaisha ifikiapo mwezi Julai.
Guterres
aliwaandikia mabalozi wa mataifa wanachama 193 akiwataka kuheshimu wajibu wao
wa kutoa malipo kwa shirika hilo, ili kuizuia kuporomoka kwake.
Tangazo hili
linakuja baada ya taifa la Marekani ambalo lililokuwa mfadhili mkubwa wa
shirika hilo kukataa kufadhili miradi ya kudumisha amani inayoendeshwa na umoja
wa mataifa na kujiondoa kwa mashirika mengine kwa madai ya "kuharibu pesa
za walipa kodi".
Wanachama wengine kadhaa pia wana madeni au wanakataa tu
kulipa.
Guterres
amesema umoja wa mataifa awali imekumbwa na uhaba wa fedha ila kwa sasa hali
imekuwa mbaya zaidi.
Ingawa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mabadiliko ya sehemu katika mfumo
wake wa kifedha mwishoni mwa mwaka 2025, shirika hilo bado linakabiliwa na upungufu
mkubwa wa kifedha unaozidishwa na sheria inayomaanisha kuwa linarejesha pesa
ambazo halijawahi kupokea.
Katika makao
makuu yake mjini Geneva, mabango ya onyo kuhusu hali hiyo yamewekwa kila
mahali.
Katibu huyo
aliongezea kuwa ufanisi wa mfumo wa UN, unatokana na mataifa wanachama
kuheshimu wajibu wao wa kisheria chini ya mkataba wa umoja wa mataifa, na
kuongeza kuwa mwisho wa mwaka 2025, 77% ya malipo hayakuwa yametolewa na
mataifa wanachama kwa shirika hilo.
"Siwezi
kusisitiza vya kutosha kuhusu dharura ya hali tuliyonayo kwa sasa. Hatuwezi
tekeleza bajeti zetu bila fedha kutoka mataifa wanachama, na hatuwezi rudisha
fedha ambazo hatujawahi kupokea."
"Sijui
nielezee vipi dharura ya hali tuliyonayo kwa sasa. Hatuwezi kutekeleza bajeti zetu
bila fedha, wala kurudisha fedha ambazo hatujawahi kupokea kamwe".
Mwezi
Januari, Marekani ilijiondoa kutoka mashirika tofauti ikiwemo 31 ya umoja wa
mataifa.