Madaktari wanaotambua miili kutoka makaburi ya halaiki Syria

- Author, Tim Franks
- Nafasi, BBC Newshour
- Muda wa kusoma: Dakika 6
"Hii," anasema Dkt. Anas al-Hourani, "imetolewa kutoka kaburi la pamoja lililochanganyika."
Dkt. al-Hourani, mkuu wa Kituo Kipya cha Utambuzi wa Syria, anasimama karibu na meza mbili zilizojaa mifupa ya mapaja ya binadamu.
Kila meza imefunikwa kwa kitambaa cheupe na juu yake kuna vipande 32 vya mifupa, vimepangwa kwa umakini na kuwekewa namba.
Kupanga mifupa ni hatua ya mwanzo katika mchakato mrefu wa kutafuta haki dhidi ya uhalifu wa kivita uliofanyika nchini Syria.
Kaburi la pamoja lenye miili mchanganyiko linamaanisha kwamba maiti zilitupwa bila mpangilio, moja juu ya nyingine.
Inaaminika kuwa mifupa hii ni ya baadhi ya maelfu ya watu waliouawa na utawala wa Bashar al-Assad na baba yake Hafez, waliotawala Syria kwa zaidi ya nusu karne.
Iwapo ni hivyo, anasema Dkt. al-Hourani, basi waliuawa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita waathiriwa wa hivi karibuni.
Dkt. al-Hourani ni mtaalamu wa vinasaba vya meno.
Anasema meno yanaweza kutoa taarifa muhimu kuhusu mtu aliyekufa hasa katika kumtambua jina au historia yake.
Lakini hata kwa mfupa wa paja, wataalamu wa maabara katika jengo dogo la kijivu jijini Damascus wanaweza kuanza kazi: wanaweza kubaini urefu wa mwili, jinsia, umri, hata kazi aliyokuwa akiifanya marehemu. Wanaweza pia kutambua kama mtu huyo aliteswa kabla ya kuuawa.
Licha ya hayo, njia bora kabisa ya utambuzi ni upimaji wa vinasaba (DNA).
Hata hivyo, Syria ina kituo kimoja tu cha kupima DNA.
Vingi vimeharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha, kutokana na vikwazo vya kimataifa, kemikali muhimu zinazohitajika kwa vipimo hivyo hazipatikani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Zaidi ya hayo, baadhi ya vifaa vinavyochangia mchakato huo vinaweza kutumika pia kwa matumizi ya kijeshi, hali inayovifanya kupigwa marufuku kuingizwa nchini na mataifa mengi ya Magharibi.
Na kisha kuna gharama: dola 250 kwa kipimo kimoja.
Dkt al-Hourani anaweka wazi kuwa katika kaburi lenye miili mchanganyiko, huchukua vipimo 20 au zaidi ili kuunganisha mwili mmoja.
Maabara hiyo inaendeshwa kwa ufadhili pekee kutoka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Serikali mpya ya waasi waliogeuka kuwa watawala inasema kuwa "haki ya mpito" ni mojawapo ya vipaumbele vyake.
Lakini kwa familia nyingi za Wasyria waliopoteza wapendwa wao ambao hawajulikani waliko bila hata kaburi kunawakosesha matumaini ya haki kupatikana.
Wameiambia BBC kuwa wanataka kuona hatua thabiti kutoka kwa viongozi waliomuondoa Bashar al-Assad madarakani mwezi Desemba mwaka jana, baada ya miaka 13 ya vita vya kutisha.
Katika kipindi hicho, maelfu waliuawa, mamilioni wakalazimika kukimbia, na takribani watu 130,000 walitoweka bila maelezo.
Kwa kasi ya sasa, inaweza kuchukua miezi kadhaa kumtambua mwili mmoja kutoka kaburi la pamoja.
"Hili," asema Dkt. al-Hourani, "ni kazi ya miaka mingi, na bado ni mwanzo tu."
Miili Iliyoharibiwa na Kuteswa
Kando ya mlima mmoja wa jangwa nje ya Damascus, kuna makaburi 11 ya pamoja.
BBC imekuwa chombo cha kwanza cha habari cha kimataifa kutembelea eneo hili.
Makaburi haya sasa yanaonekana wazi, ardhi inayozunguka imeporomoka polepole kwa miaka mingi.
Tunaandamana na Hussein Alawi al-Manfi, anayejulikana pia kama Abu Ali.
Alikuwa dereva wa jeshi la Syria.
"Mizigo yangu," asema Abu Ali kwa sauti ya chini, "ilikuwa ni miili ya watu."

Mwanaume huyu mwenye ndevu za mvi alifichuliwa kupitia uchunguzi wa kina wa Mouaz Mustafa, Mkurugenzi wa Shirika la Syrian Emergency Task Force lililo Marekani.
Alimshawishi Abu Ali aungane nasi, ashuhudie kile anachokiita "uhalifu mkubwa zaidi wa karne ya 21."
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Abu Ali alisafirisha miili kwa malori hadi maeneo tofauti ya maziko ya siri.
Katika eneo hili, alifika takriban mara mbili kwa wiki, kwa kipindi cha miaka miwili mwanzoni mwa maandamano na vita (2011–2013).
Alikuwa na trela la urefu wa mita 16.
Mara nyingi halikuwa limejaa kabisa, lakini kila safari, alibeba miili 150 hadi 200. Anasema aliamini wengi wao walikuwa raia, waliouawa kikatili. Miili ilikuwa imeharibiwa vibaya, mingine ikiwa na alama za mateso.
Utambulisho wao ulikuwa ni namba tu zikiandikwa mwilini au kupachikwa usoni au kifuani zikionyesha sehemu walikokufa.
Kituo kilichotajwa mara kwa mara ni "Branch 215", jela ya siri ya idara ya ujasusi wa kijeshi mjini Damascus. Eneo hili tutalizungumzia katika makala haya.
Ni mojawapo ya maeneo yaliyotajwa kutoa maiti nyingi zilizochukuliwa na Abu Ali.
Malori hayakuwa na kifaa cha kushusha mizigo.
Abu Ali alipowasili kwenye shimo kubwa, askari walivuta miili na kuitumbukiza moja baada ya nyingine.
Baadaye trekta la mbele lilikandamiza na kufukia mashimo hayo.
Wanakijiji watatu wenye nyuso zilizochoka walifika na kuthibitisha kuwa waliona malori yakifika hapo mara kwa mara, miaka yote hiyo.
Lakini dereva huyu angewezaje kufanya hili wiki baada ya nyingine na kila mwaka?
Je, Abu Ali aliwezaje kuishi na hali hiyo? Aliwaza nini kila aliposhika usukani?
Anasema alijifunza kuwa mfanyikazi wa serikali wakunyamaza na kutii.
"Huwezi kusema jambo lolote zuri au baya."
Wakati askari wanatupa miili na kufukia makaburini, "mimi ningeenda pembeni, nikatazama nyota au mji wa Damascus kwa mbali."
"Walimvunja mikono na kumpiga mgongoni"
Damascus pia ndiyo mji ambao Malak Aoude amerudi baada ya miaka mingi kama mkimbizi nchini Uturuki.
Ingawa Syria sasa ipo mikononi mwa watawala wapya, Malak bado anaishi kifungo cha maisha.
Kwa zaidi ya miaka 13, amekuwa akijifungia kila uchao akisononeka.
Tangu 2012, alipowapoteza wanawe wawili Mohammed na Maher hajawahi kupata jibu.
Hii ni baada ya maandamano dhidi ya Rais, ambapo wanawe wawili walipotea.

Mohammed, aliyekuwa kijana mdogo wakati huo, alilazimishwa kujiunga na jeshi.
Alikerwa na aliyoyaona, akaanza kukwepa na kujiunga na waandamanaji mamake anasema.
Alikamatwa, akateswa vibaya. "Walimvunja mikono na kumpiga mgongoni," asema mama yake. "Alikaa hospitalini kwa siku tatu bila fahamu."
Baadaye alijificha, lakini alikamatwa tena mwezi Mei 2012,mtoto wake wa miaka 19 akiwa na marafiki zake wote wakapigwa risasi.
Hakukuwa na taarifa rasmi, lakini Malak anaamini mtoto wake aliuawa.
Miezi sita baadaye, Maher, mdogo wake, alikamatwa akiwa shuleni.
Alikuwa na umri wa miaka 14 wakati alipoanza kushiriki maandamano mwaka 2011.
Mara ya kwanza alipotoka mahabusu, mwili wake ulikuwa umejaa majeraha na alama za kuchomwa zikidhihirisha mateso aliyopitia.
Aliogopa sana," asema Malak.
Aliporudi shuleni kutafuta taarifa, walimu walimpa daftari la zamani lililo na jina la Maher.
Ilionyesha alifukuzwa kwa kutohudhuria shule kwa wiki mbili.
Hakukuwa na maelezo kuwa alikamatwa na vyombo vya dola.
Pia walimpatIa faili la shule la Maher lenye picha ya Bashar al-Assad kwenye jalada.
Malak alichukua kalamu na kufuta picha hiyo kitendo ambacho miaka sita iliyopita kingeweza kumgharimu maisha.
Kwa miaka yote hiyo, tumaini lake lilitegemea simulizi za watu wawili waliodai kumuona Maher katika "Branch 215".
Mmoja wao alimweleza jambo ambalo, anasema Malak, ni Maher pekee ambaye angeweza kulisema.
''Maher alimtuma kumjulisha mamake kuwa yuko salama alipo'' akielezea haya machozi yalimtiririka kwa uchungu.
Kwa Malak kama ilivyo kwa maelfu ya Wasyria wengine kuondoka kwa Assad kulikuwa ni siku ya matumaini.
"Nilijua kwa asilimia tisini kwamba Maher angefunguliwa na kuachiliwa huru.''
Lakini hajaweza hata kupata jina la mwanawe kwenye orodha ya magereza.
Na hivyo pigo la maumivu linaendelea kumkosesha usingizi.
"Ninahisi kupotea na kuchanganyikiwa," anasema.
Kaka yake mdogo, Mahmoud, aliuawa kwa kupigwa risasi na gari la jeshi lililokuwa likimiminia raia risasi mnamo 2013.
"Angalau alikuwa na mazishi."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












