Kamanda mkuu wa Hezbollah aliyeuawa alikuwa nani?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi la Hezbollah ameuawa katika shambulio la kombora la Israeli katika mji mkuu wa Lebanon - Beirut siku ya Ijumaa, katika uhasama unaoongeza hofu ya vita kamili.

Hezbollah limethibitisha kifo cha Ibrahim Aqil baada ya Israeli kusema kuwa alikuwa mmojawapo ya viongozi kadhaa wakuu wa kundi hilo aliyeuawa katika shambulio.

Hapo awali maafisa wa Lebanon walisema kuwa takriban watu 14 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio hilo lililotekelezwa katika eneo la Dahieh lenye watu wengi na ambalo ni ngome ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Afisa mkuu wa Umoja wa mataifa ameonya kuwa eneo la mashariki ya kati limo katika hatari ya mzozo ambao utakuwa mkubwa zaidi ya uharibifu ambao tayari umeshuhudiwa katika eneo hilo mpaka sasa.

Huko Beirut, kulikuwa na matukio ya mshikemshike timu za dharura zikikimbilia eneo la shambulizi, kuwaokoa waliojeruhiwa na kuwatafuta watu wanaoaminika kuwa wamenasa chini ya vifusi.

Jengo moja la makazi liliporomoka na mengine kuharibiwa sana.

Wanachama wa Hezbollah walisimamisha shughuli za mitaani, wengine wakionekana kutokuamini huku shambulio hilo likiwakilisha pigo lingine la kufedhehesha ndani ya wiki moja ambalo lilishuhudia vifaa na redio za mawasiliano vya kundi hilo zikilipuka.

Makumi ya watu waliuawa na maelfu kujeruhiwa katika mashambulizi hayo yanayoaminika kuratibiwa na Israel.

Shambulio hilo la Ijumaa ni la kwanza kuilenga Beirut tangu Julai, wakati mkuu wa jeshi la Hezbollah Fuad Shukr alipouawa.

Soma zaidi:

Katika taarifa yake, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Daniel Hagari alisema Aqil, kamanda mkuu katika vikosi vya wasomi vya Hezbollah vya Radwan, aliuawa pamoja na watendaji wakuu wakiwa kwenye mkutano.

Hagari alisema "walikuwa wamekusanyika kwenye jengo moja la makazi eneo la chini ya ardhi katikati mwa kitongoji cha Dahiyah [kusini mwa Beirut], wakijificha miongoni mwa raia wa Lebanon, wakiwatumia kama ngao".

Msemaji wa IDF aliongeza kuwa watu waliouawa walikuwa "wanapanga mashambulizi, ambapo Hezbollah ilinuia kujipenyeza katika jamii za Israel na kuua raia wasio na hatia."

Mnamo mwezi Aprili, Washington ilisema ilikuwa ikimtafuta Aqil, ambaye pia anajulikana kama Tahsin, na ilitoa zawadi ya kifedha kwa mtu yeyote mwenye "taarifa zitakazopelekea kutambuliwa kwake, mahali, kukamatwa na/au kutiwa hatiani".

Alikuwa akitafutwa na Marekani kutokana na kuhusika kwake na cheo alichonacho ndani ya kundi la Hezbollah, ambalo limetangazwa kuwa shirika la kigaidi na Israel, Uingereza, Marekani na nchi nyinginezo.

Mnamo 1980, alikuwa mwanachama wa kikundi kilichopanga shambulio la Ubalozi wa Marekani huko Beirut na kambi ya wanamaji.

Mashambulizi hayo yaliua watu 63 na 307 mtawalia.

Mnamo mwaka wa 2019, Marekani ilimtaja Aqil kama gaidi na tovuti Wizara ya Sheria inasema anahudumu katika baraza kuu la kijeshi la Hezbollah - Baraza la Jihad.

Ikithibitisha kifo cha Aqil katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, Hezbollah ilimtaja kama mmoja wa "viongozi wakuu wa kijihadi".

Kundi hilo lilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na katika eneo lililotawaliwa na Washia, Iran, ili kuipinga Israel.

Wakati huo, wanajeshi wa Israel walikuwa wameikalia kwa mabavu kusini mwa Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mapema siku ya Ijumaa, Hezbollah ilisema kuwa ilianzisha mashambulizi katika maeneo ya kijeshi kaskazini mwa Israel.

IDF ilisema roketi 140 zilirushwa kaskazini mwa nchi hiyo, huku polisi wa Israel wakitoa onyo kuhusu uharibifu wa barabara.

Hilo lilitokea baada ya Israel kufanya mashambulizi makubwa ya anga kusini mwa Lebanon, ikisema kuwa ndege zake za kivita zilishambulia zaidi ya roketi 100 za Hezbollah na "maeneo mengine ya kigaidi" ikiwa ni pamoja na kituo cha kuhifadhi silaha.

Mapigano ya kuvuka mpaka kati ya Israel na Hezbollah yaliongezeka tarehe 8 Oktoba 2023 - siku moja baada ya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israeli kutekelezwa na wapiganaji wa Hamas kutoka Gaza - wakati Hezbollah iliposhambulia maeneo ya Israeli ikionyesha kuunga mkono Wapalestina.

Tangu wakati huo mamia ya watu, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hezbollah, wameuawa katika mapigano hayo ya mpakani, huku makumi ya maelfu pia wakikimbia makazi yao katika pande zote za mpaka.

Hivi majuzi Israel iliongeza kurejea kwa watu waliokimbia makazi yao kutoka kaskazini mwa nchi hiyo kwenye orodha yake lengwa katika vita, na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant alisema siku ya Alhamisi kwamba nchi yake inaingia katika "awamu mpya ya vita", ikizingatia zaidi upande wa kaskazini.