Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu miamba ya angani iliyo karibu na dunia, na tishio linalowasumbua Wanasayansi
- Author, Sue Nelson
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kulingana na NASA, kila mwaka, kipande cha mwamba chenye ukubwa wa gari hupita angani katika mwelekeo wa kugongana na sayari yetu. Kwa bahati nzuri, angahewa ya dunia kufanya kazi kama ngao ya asili, badala ya kuanguka duniani, miamba hiyo huwaka na kutoa mwanga angani kama kimondo au mpira wa moto.
Kwa bahati mbaya, miamba mengine mikubwa hutishia kugonga dunia, anasema Michael Küppers, mwanasayansi wa sayari wa Shirika la Anga la Ulaya (ESA). "Miamba mikubwa, yenye ukubwa wa kama kilomita 10 (maili 6.21) [upana] au zaidi ambayo kama iliyosababisha kutoweka kwa dinosaria, hiyo hutokea labda mara moja kila baada ya miaka milioni 100."
Mwamba uliopewa jina la Asteroid 2024 YR4, ambao iligunduliwa Desemba 2024, umekuwa ukigonga vichwa vya habari kote ulimwenguni. Hapo awali ulikadiriwa kuwa na upana wa mita 40-90 (131-295ft), zaidi ya jengo la ghorofa 12.
Januari mwaka huu, ESA ilikokotoa mwelekeo wa mwamba huo na kutabiri kuwa kuna uwezekano wa 1.2% kuathiri dunia tarehe 22 Desemba 2032.
Kwa bahati nzuri, mwamba YR4 si mkubwa sana wa kuwa na uwezo wa kutokomeza spishi zetu lakini bado unaweza kuleta "mauaji katika jiji," ikiwa utatua katika eneo lenye watu wengi.
Februari 2025, hatari ya mwamba huo kugonga dunia ilipanda kwa muda mfupi hadi 3.1%. Lakini hatari hiyo kisha ikapungua hadi 0.001%.
Kisha Aprili 2025, Nasa ilitoa maelezo ya uchunguzi mpya wa mwamba wa YR4 kutoka Darubini ya Nafasi ya James Webb, ikikadiria mwamba huo ni mdogo kidogo kuliko ilivyofikiriwa awali, una ukubwa wa karibu jengo moja la ghorofa 10.
Lakini Kituo cha Nasa kilieleza uwezekano wa YR4 kugonga Mwezi - tarehe 22 Desemba 2032 – na kuweka 3.8%, kutoka 1.7% ambayo ilitabiriwa mwishoni mwa Februari 2025. Ingawa asilimia hiyo ya kugongana na mwezi, haitoshi kubadilisha mwelekeo wa mwezi.
Miamba hutokea wapi?
Linapokuja suala la kuelewa miamba, Wataalamu wa anga na wanasayansi bado wanatafiti ili kuelewa mawe haya makubwa ambayo ni hatari.
Alan Fitzsimmons, mtaalamu wa anga katika Chuo Kikuu cha Queens Belfast na mwanachama wa kitengo cha uchunguzi wa anga cha Nasa ambacho hutafuta na kufuatilia Vitu vya Karibu na Dunia (NEOs).
"Mwamba wowote tunaougundua ni kipande ambacho kilitokea wakati wa kuzaliwa kwa Mfumo wetu wa Jua - zaidi ya miaka bilioni kadhaa iliyopita," anasema Fitzsimmons.
Mabaki haya ya kale ya miamba wakati mwingine hujulikana kama sayari ndogo. Mara nyingi hayana maumbo maalumu lakini wakati mwingine huwa mviringo. Huzunguka haraka haraka, polepole au hubiringia. Kwa kawaida huwa mwamba mmoja, wakati mwingine inaweza kuwa zaidi.
Tovuti ya Nasa's Jet Propulsion Laboratory hufuatilia miamba hii, na katika hesabu ya mwisho kuna zaidi ya miamba milioni 1.4 katika Mfumo wetu wa Jua. Mingi iko katika Ukanda kati ya sayari ya Mirihi na Jupita.
Mara nyingi miamba hii husalia kuzuiliwa ndani ya ukanda huo wa sayari na mvuto wa graviti ya Jupita, haiwezi kugonga sayari kubwa.
Lakini katika baadhi ya matukio, mwamba mwingine au nguvu za graviti ya Jupita, inaweza kuusukuma mwamba kuingia katika obiti ya sayari nyingine.
Miamba hugunduliwaje?
Pindi miamba inapoondoka kwenye ukanda huo kuna uwezekano wa kuelekea kwenye dunia, changamoto ya kwanza ni kuugundua mwamba huo.
"Mwamba wowote huonekana kwenye darubini kama nukta zingine za mwanga ambazo ni nyota, isipokuwa mwamba huwa unasogea," anasema Kelly Fast, kaimu afisa wa ulinzi wa sayari wa NASA, "na mwamba huakisi mwanga wa jua."
Kadiri mwamba unavyong'aa zaidi ndio huonyesha ukubwa wake. Lakini rangi ya mwamba huathiri mwangaza wake pia, kwani mwamba mweupe unaweza kuakisi mwanga wa jua zaidi kuliko mwamba mweusi.
"Kuna miamba tofauti," anasema Fast. "Mengine ni ya mawe, mengine ni ya kaboni na mengine ni ya metali kulingana na eneo mwamba ulipotoka."
Kujua muundo wa mwamba ni muhimu. Miamba ya chuma, kwa mfano inaweza kufanya uharibifu zaidi kuliko ile ya kaboni kwa kuwa ni mizito zaidi, kama utagonga Mwezi au Dunia.
Ingawa hakuna uwezekano wa dunia kupata athari ya kugongwa na YR4, bado kuna uwezekano wa 1.7% kwamba mwamba huo unaweza kugonga mwezi wetu.
Kuilinda Dunia
Mwamba wa moto ulioingia kwenye angahewa ya dunia 2013 - ulilipuka takribani maili 14 (22.5km) juu ya jiji la Chelyabinsk nchini Urusi. Walioshuhudia walielezea mwanga huo kuwa unang'aa zaidi kuliko Jua, na wimbi la mlipuko huo liliharibu zaidi ya majengo 4,000 na kujeruhi watu 1,200.
"Mwamba huo ulikuwa na ukubwa wa karibu mita 20m (66ft)," anasema Küppers.
Siku ya tukio la Chelyabinsk, kamati ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ikiendelea mjini Vienna kujadili kuhusu kuilinda dunia dhidi ya athari za mimba.
Mkutano huo ulianzisha Mtandao wa Maonyo ya Kimataifa juu ya Miamba, unaoongozwa na Nasa, na Kikundi cha Ushauri juu ya Misheni za Anga – na kutaka mashirika ya anga duniani kote kushirikiana.
Mwaka 2000, chombo cha Nasa kilikuwa chombo cha kwanza cha anga kuzunguka mwamba wa Eros, na - mwaka mmoja baadaye – kilitua kwenye moja ya miamba.
Chombo cha Japan, cha Huyabusa 2 kiliutembelea mwamba aina ya C 162173 Ryugu mwaka 2018 na 2019 na kikaleta sampuli ya mwamba huo duniani kwenye bakuli lililofungwa.
Tunataka kuilinda dunia lakini pia tunataka kusoma mabaki haya ya kushangaza kutoka uundaji wa Mfumo wa Jua, ili kuelewa historia na uundwaji wa mfumo wa jua.