‘Nitapiga kura lakini sitarajii kipya’

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili

th

Chanzo cha picha, MANNY ANYANGO

Tarehe 9 Agosti mwaka huu sasa inaonekana kuwa karibu sana .Ngoja ngoja ya miaka mitano sasa imesalia kuwa ya siku chache tu .

Taswira ya hali itakavyokuwa katika siku hiyo ya Wakenya kupiga kura imeanza kujitokeza wazi wazi katika fikra za wengi .

Mojawapo ya makundi ambayo yana mchango mkubwa sana katika mchakato sio tu wa kuamua uongozi wa nchi bali pia mwelekeo wa demokrasia ya Kenya ni vijana .

Pia ndio kundi kubwa zaidi la wapiga kura lakini wamejipata na hisia kinzani kuhusu kinachofaa kuwa mchango wao.

Kuna hofu ya wengi kutojitokeza kupiga kura na hilo limedhihirika wazi hasa wapiga kura wanapojitayarisha kufanya uamuzi wao.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,IEBC ilikosa kuafikia lengo lake la usajili wa wapiga kura na vijana wengi wenye umri wa kupiga kura hawakujiandikisha.

'Viongozi wajao' wasiojali kuhusu kura

th

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema ripoti ya ukaguzi ya kampuni ya KPMG iliyotolewa mwezi Juni mwaka huu ilionyesha kwamba idadi ya vijana waliosajiliwa wenye umri wa miaka 18-34 inafikia asilimia 39.84, ikiwa ni asilimia 5.27 ikilinganishwa na 2017.

Alisema ripoti hiyo ilionyesha usajili wa vijana wa kiume umepungua kwa asilimia 2.89 katika kipindi cha miaka mitano.

Uchambuzi zaidi wa takwimu za usajili wa vijana unaonyesha kupungua kwa idadi ya wapiga kura wa kike waliojiandikisha kwa asilimia 7.75 kati ya 2017 na 2022,”

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Licha ya kutajwa kama ‘viongozi wa siku zijazo’ yamkini vijana wameonekana kuwa kama hadhira tu katika mchezo wa kina kirefu wa siasa za Kenya .

Wanatumiwa na wanasiasa kujaza viwanja vya mikutano ya kisiasa na wakati mwingine wanachochewa kufanya ghasia ilhali wao ndio nguzo muhimu sana katika kuleta unadhifu katika uongozi ili kusuluhisha baadhi ya kero zao kubwa kama vile ukosefu wa ajira .

th

 Miaka mingi ya ahadi ambazo vijana wamepewa na wanasiasa na ambazo hazijatimizwa huenda imechangia wengi kukosa matumaini kwamba wanaweza kuleta mageuzi kupitia kura .

Kunao hata walioamua kwamba mchakato mzima wa kupiga kura hauwafai na huo ndio mwanzo wa njia panda kwa vijana nchini Kenya .

Ili kufahamu uchaguzi huu ujao una maana gani kwao,BBC Swahili imezungumza na baadhi yao ambao misimamo na kauli zao zinaweza kutupa taswira ndani ya fikra za kundi hili muhimu katika uchaguzi wa Kenya .

Manny Anyango,27

th

Chanzo cha picha, MANNY ANYANGO

Maelezo ya picha, ‘Kinachonichochea sana kupiga kura ni imani yangu kwamba kutakuwa na mabadiliko'
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Itakuwa mara ya kwanza kwa Manny Anyango kupiga kura katika uchaguzi huu mkuu.

Kuna mamilioni ya wengi kama yeye ambao watapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka huu na wao ndio waliobeba matumaini makubwa kwamba uchaguzi huu utaleta mabadiliko .Watalenga kuona haki yao ya kupiga kura ikiwapa matunda baada ya uchaguzi .

‘Kinachonichochea sana kupiga kura ni imani yangu kwamba kutakuwa na mabadiliko,pia nina uchu wa kujua mtu anahisi vipi anapopiga kura-ni haki ambayo natamani sana kuitekeleza’ anasema mwandishi huyo wa habari .

Katika jitihada za kuwavutia vijana wengi na hasa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza, wagombeaji wametosa mbinu mbali mbali na ahadi zimekuwa nyingi kupindukia ambazo wanawalimbikizia wapiga kura .

Utekelezaji wa ahadi hizi hata hivyo unasalia kuwa ngano za kale iwapo historia ya siasa za ahadi nchini Kenya ni jambo la kutegemewa hapa .

Wengi wa wagombeaji tayari wameshatoa manifesto zao zenye mipango,mikakati na wanachoamini ni ufumbuzi wa kero za vijana .

Anyango anaamini ameweza kuwatambua wagombeaji ambao watanufaika na kura yake .

‘Kama mwanahabari,nimefanikiwa kusoma na kupitia manifesto zote za wagombeaji ,kuanzia kwa wale wa urais hadi kwa mwakilishi wadi-nimewatambua wagombeaji ambao nimevutiwa na walichoandika-ila sina uhakika iwapo watayatekeleza yote’ anasema .

Maelezo ya video, Uchaguzi Kenya 2022:Kwa nini vijana wanajipata nje ya uongozi wa kisiasa nchini Kenya?

Victoria Wanjiku,Wakili

th

Chanzo cha picha, VICTORIA WANJIKU

Maelezo ya picha, Bado sijaamua iwapo nitapiga kura.Kwa upande mmoja kupiga kura kunaonekana kama kupoteza muda kwa upande mwingine nisingependa kuona baadhi ya viongozi wakiwa madarakani.

Kwa wakili chipukizi ,Victoria Wanjiku upigaji kura kwake mwaka huu utakuwa kama ‘silaha ya kinga’.

Anasema haamini wanasiasa watazitekeleza ahadi nyingi wanazozitoa na hasa kwa vijana .

Kwake,ahadi hizi zimekuwa kama nyimbo tangia zamani na wanasiasa wamejenga ustadi wakuzikariri nyimbo hizo wakati wa kampeini .

‘Bado sijaamua iwapo nitapiga kura. Kwa upande mmoja kupiga kura kunaonekana kama kupoteza muda kwa upande mwingine nisingependa kuona baadhi ya viongozi wakiwa madarakani. Nitapiga kura kama hatua ya kuzuia na natumai tu kwamba kura yangu itakuwa na usemi’ anasema .

th

Chanzo cha picha, VICTORIA WANJIKU

Maelezo ya picha, ‘Tunaweza tu kutumaini na kuomba kwamba mageuzi yaje katika miaka 20 ijayo’

 Victoria ,anashikilia kwamba mageuzi yatahitaji ukakamavu kutoka kwa vijana na mageuzi ya kweli husenda yasije Kenya katika miaka kumi ijayo.

‘Tunaweza tu kutumaini na kuomba kwamba mageuzi yaje katika miaka 20 ijayo’ anaongeza .

 Msimamo wake huo anasema umetokana na kile anachosema ni kuwepo kwa viongozi wale wale ambao licha ya kuhudumu serikalini kwa miaka ya awali,hakuna walichofanya kinachompa imani kwamba watatekeleza ahadi wanazotoa sasa .

Magdaline Kemunto Machogu ,33

th

Chanzo cha picha, MAGGY YUNA

Maelezo ya picha, ‘Ikiwa ningekuwa na pesa ningeondoka nchini kwenda likizo mahali fulani huko Caribean wakati wa uchaguzi’ 

Kwa Magdaline Kemunto,mchakato mzima wa kampeini na upigaji kura ni kipindi ambacho binafsi humpa hofu .

Haelewi kwa nini lakini anasema panda shuka na cheche za kipindi kizima cha kampeni huwa kinaleta hali ya wasi wasi katika nchi .

‘Iwapo ningekuwa na pesa ningeondoka nchini kwenda likizo mahali fulani huko Caribean wakati wa uchaguzi’ anasema huku tabasamu yake ikiishiria kwamba ni utani .

Lakini kupiga kura ni haki yako,mbona utoroke?

Anabainisha kwamba hana mpango wa kukosa kupiga kura .

‘Kwangu,ni jukumu ambalo siwezi kuliepuka ,nahisi ni wajibu wangu kumchagua kiongozi anayefaa’ anasema

 Kuhusu matumaini ya kura yake kuleta mabadiliko,anasema hilo ni kama mchezo wa kamari

‘Kama mpiga kura nchini Kenya,una mawili-ujitokeze kupiga kura,kisha uombe kwamba unayempigia kura alikuwa na nia ya kweli ya kukutumikia’.

Spencer ,31

TH

Chanzo cha picha, SPENCER

Maelezo ya picha, ‘Ndio nitapiga kura.Natanguliza kuhakikisha nimempa kura mwakilishi wa wadi anayefaa na gavana ninayemtaka’

 Kwa mhandisi wa kilimo mwenye umri wa miaka 31,Spencer-uchaguzi huu ni fursa kwake kuweka maslahi yake kwanza .

Spencer,anayetaka kutambuliwa kwa jina moja pekee anasema hajawapa fikra wagombeaji wa urais kwani ugatuzi umemfanya kuwapa uzito viongozi katika ngazi ya kaunti.

‘Ndio nitapiga kura.Nitatangulia kumpa kura mwakilishi wa wadi anayenifaa na gavana ninayemtaka’

 Spencer anasema hatarajii mabadiliko katika ngazi ya juu kwani anahisi vyama vyote vikubwa vya kisiasa vimekandamiza demokrasia kwa kiasi fulani.

‘Kuna wagombeaji ambao wangewafaa wananchi,lakini vyama viliwatema kwa njia zisizo za kidemokrasia ,hilo halinipi imani kwamba vina nia njema ama kutakuwa na mabadiliko’ anaongeza .

‘Kura yangu itakuwa ya kujiepusha na uwajibakaji wowote wa kizaazaa cha baadaye cha viongozi wasiofaa ambao raia watawachagua au watakaosaidiwa kusalia madarakani’

TH
TH