Uchaguzi Kenya 2022: Kwanini kuna wagombea huru wengi katika uchaguzi huu

Na Abdalla Seif Dzungu

BBC Swahili Nairobi

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Wafula Chebukati

Tarehe 2 Mei iliashiria siku ya mwisho ilio rasmi ambapo watu binafsi walionuia kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 bila kuegemea chama chochote walihitaji kujiandikisha ili kuwa wagombea huru.

Kifungu cha 85 cha katiba ya mwaka 2010 kinasema kwamba mtu yeyote anastahili kugombea kama mgombea binafsi kwa ajili ya uchaguzi mradi tu mwanachama huyo si mwanachama aliyesajiliwa na chama chochote cha kisiasa na pia hajawa mwanachama wa chama chochote kilichosajiliwa miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Kulingana na kalenda ya tarehe muhimu ya kipindi hiki cha kuandaa uchaguzi, vyama vya kisiasa vilihitaji kuwa vimekamilisha uteuzi wa vyama vyao kufikia tarehe 22 Aprili 2022, na baadaye kufikia tarehe 28 Aprili orodha ya wagombeaji waliopendekezwa wa vyama vya kisiasa ilihitajika kuwasilishwa kwa IEBC kwa gazeti la serikali.

 Mtu yeyote aliyeshiriki katika zoezi lolote la uteuzi wa vyama vya kisiasa alipewa fursa kama anahisi alionewa kuwania kama mgombea binafsi.

Mifumo dhaifu ya vyama vya kisiasa

Uchaguzi wa 2022 umeshuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaowania kama wagombeaji huru, idadi ya sasa ikiwa 7000 iliyoidhinishwa na IEBC. Ongezeko hili kubwa la wagombea binafsi linaweza kuchangiwa na mambo kadhaa, muhimu miongoni mwao ni ukosefu wa uwezo wa vyama vya kisiasa kuandaa uteuzi huru, wa haki na unaoaminika.

Vyama vingi vya kisiasa vina mifumo dhaifu ya kiutawala ya ndani ambayo kwa kiasi kikubwa inatawaliwa na watu walio na mwelekeo wa kisiasa, hivyo basi hakuna hakikisho la uteuzi wa haki, huru na wa kuaminika.

Katika mikoa mingi, zoezi la uteuzi huzingatiwa kama uchaguzi mdogo huku mhudumu akiwa na athari kubwa ya kulipia gharama, ilhali hakuna hakikisho lolote la zoezi huru, la haki na la kuaminika -ukweli huu kwa njia nyingi umewalazimu wagombeaji wengi kuchagua kuwa huru

Tangu kuwasili kwa siasa ya vyama vingi nchini Kenya, vyama vingi vimeanzishwa na vimekuwa vikiendeshwa kwa misingi ya hesabu za kikabila na ushawishi wa kisiasa wa "mfalme wa kabila". Vyama hivi havitofautiani kwa misingi ya itikadi yoyote inayojulikana bali eneo la kijiografia na kabila la kiongozi wa chama.

wapiga kura Kenya
Maelezo ya picha, Wapiga kura wakisubiri kushiriki katika shughuli hiyo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika hali ya sasa, Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ambacho kiongozi wake wa ni Mhe. Raila Odinga, ana ngome yake katika eneo la Nyanza ambako jamii yake ya Waluo wengi wao wanaishi; katika hali hiyo hiyo Wiper Democratic Movement, ambayo kiongozi wake wa chama anatoka eneo la Ukambani, inapata uungwaji mkono wake kutoka kwa kabila la Akamba kutoka eneo la mashariki mwa Kenya; Chama cha United Democratic Party (UDA) cha William Ruto kinatoa wafuasi wake washupavu kutoka kwa jamii ya kalenjin ambao wanaishi katika eneo kubwa la bonde la ufa nchini Kenya; hali hiyo hiyo inawahusu viongozi wengine wote wenye vyama vya siasa.

Hivyo basi, upendeleo wa mtu binafsi unaofanywa na kiongozi wa chama kuhusiana na nafasi fulani ya mgombea, mara nyingi hushinda haja ya kuandaa zoezi lolote la maana la uteuzi na hivyo kuishia kwa mgombea aliyependekezwa kupewa cheti cha uteuzi. Changamoto kubwa zaidi ni kukidhi matarajio ya kiongozi wa chama, na matarajio haya kwa kawaida huwa magumu kufikia, na hivyo kusababisha watu wengi kuamua kugombea kama wagombea binafsi.

Skip Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu Wagombeaji and continue readingUchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu Wagombeaji

End of Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu Wagombeaji

Mbinu ya 'Suti' sita

Katika uchaguzi wa awali wa vyama vingi, upigaji wa kura tatu (Rais, Mbunge na Diwani) na suti sita (Rais, Gavana, Seneta, Mbunge, Mwakilishi wa Wanawake na Mbunge wa Kaunti) zilitawala siasa za uchaguzi nchini Kenya, kwa sasa wapiga kura wamekuwa na busara zaidi hadi kusema kuwa ni mtu wanayetaka kumchagua na sio chama cha siasa.

 Mbinu hii ya "suti" ilitumika pale ambapo chama kiliweza kufanya zoezi la uteuzi la haki na la kuaminika; hata hivyo kwa miaka mingi na katika chaguzi zilizofuata, uongozi wa juu wa chama cha siasa umetumia vibaya uaminifu na utaratibu huu na kuishia kutoa vyeti vya uteuzi kwa watu wasiostahili ambao hata wanaposhinda, hawatumiki ipasavyo wapiga kura.

 Wapiga kura pia wameweza kuelewa kwamba vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi vyenye madhumuni maalum, ambavyo thamani na umuhimu wake hupungua mara tu baada ya kupiga kura.

Rais Uhuru kenyatta na naibu wake Uhuru kenyatta wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Uhuru kenyatta na naibu wake Uhuru kenyatta wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita

Je Wakenya watachagua vyama ama watu binafsi?

Hakuna kinachoonyesha vyema mfano huu wa vyama vya kisiasa jinsi vilivyotumika kuwa chombo maalum cha uchaguzi kama vile vyama vya siasa katika jimbo la kati; katika mwaka wa 1992, chama kikuu cha siasa katika jimbo la kati kilikuwa FORD-Asili cha Kenneth Matiba, katika uchaguzi wa 1997, chama cha Democratic Mwai Kibaki kilikuwa chama kikuu cha siasa, katika uchaguzi wa 2002 NARC ilikuwa sehemu kubwa, katika Uchaguzi wa 2007, Party of National Unity (PNU) ndicho kilikuwa chama kikuu, katika uchaguzi mkuu wa 2013, chama cha The National Alliance (TNA) cha Uhuru Kenyatta ndicho kilikuwa chama kikuu, huku katika uchaguzi mkuu wa 2017, chama cha Jubilee kikitawala.

Tunapoelekea uchaguzi wa Agosti 2022, wapiga kura kote nchini watachagua viongozi bila kuzingatia utendakazi wa vyama vya siasa vilivyotangulia, bali uwezo wa wagombea binafsi katika kufanya kazi, hivyo kuchangia kuongezeka kwa idadi ya wagombea binafsi.

Mipango ya kazi ya kisiasa kabla na baada ya uchaguzi pia imechangia pakubwa kupungua kwa thamani ya vyama vyaki siasa nchini. Wapiga kura wameelewa kuwa hakuna kitu cha kudumu katika siasa mbali na maslahi; kwa hivyo mipango ya awali ya kisiasa isiyoweza kutekelezeka inaweza kuwa mipango inayotekelezeka/kukubalika katika hali ya baada ya uchaguzi.

Kwa hivyo, wakati wa kumchagua kiongozi, ufuasi wa chama cha siasa au uanachama haupaswi kuchukua nafasi katika kutathmini uwezo wa mgombea. Iwapo hilo ni kinyume na mtazamo huu hali hiyo itachangia pakubwa kuongezeka kwa idadi ya wagombea binafsi katika uchaguzi ujao.

Uchaguzi
Uchaguzi