Marubani wanaosaka ndege zisizo na rubani za Wahouthi katika anga ya Bahari ya Shamu

- Author, Nafiseh Kohnavard
- Nafasi, BBC Persian
Ndege moja ya kivita inanguruma kwenye giza inapovuka USS Bataan, meli kubwa ya kivita ya Marekani. Muda mfupi baadaye, ndege ya pili inafuata.
Taa zinazomulika nyekundu na kijani kwenye ncha za mbawa zao hupotea upesi mahali fulani mashariki mwa Mediterania.
Hapa ni makao ya wanajeshi na mabaharia 24,000 wa Marekani, kambi hii kubwa ya kijeshi inayoelea iliyojaa magari ya kivita, jeti na helikopta kawaida hutumwa kwa kasi kusafirisha wanajeshi hadi nchi kavu.
Lakini wakati Wahouthi wa Yemen walipoanza kurusha makombora kwa kutumia ndege zisizo na rubani dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, wafanyakazi wa USS Bataan walijikuta wakilazimika kukabiliana na mapigano ya anga, na kutuma ndege kujaribu kuziangusha.
"Sikuwahi kufikiria ningekuwa nikifanya hivi tulipozindua," anasema rubani mkuu Kapteni Earl Ehrhart.

Kwa hakika, siku chache kabla ya kuzuka kwa vita huko Gaza, Rubani Ehrhart na wafanyakazi wenzake walifikiri kwamba walikuwa wakienda nyumbani.
Baada ya miezi kadhaa ya kushika doria majini karibu na Ghuba ya Uajemi, maelfu ya wanajeshi waliokuwa kwenye meli ya USS Bataan walikuwa karibu kumaliza ziara yao ya kikazi. Lakini asubuhi ya Oktoba 7, kila kitu kilibadilika.
Ndani ya saa moja baada ya Hamas kushambulia Israel na kuua zaidi ya watu 1,200, USS Bataan ilipokea amri mpya, kupanga njia kuelekea mashariki mwa Mediterania na kujiandaa kufuatilia pwani ya Gaza.
Siku kumi na mbili baadaye, maelekezo mengine yalitolewa katik aoperesheni yao. Wakati huu, ilishirikisha kufuatilia shughuli za waasi wa Kihouthi.
Lengo lilikuwa kukabiliana na kuongezeka kwa ghasia huko Gaza, tangu katikati ya mwezi wa Disemba Wahouthi wa Yemen wameshambulia zaidi ya meli kumi na mbili. Wanadai meli zote zilikuwa zinamilikiwa na Waisraeli au yaliendeshwa na Waesraeli. Hata hivyo, baadhi ya meli hizo zilionekana kutokuwa na uhusiano na Israeli hata kidogo.
Mwezi Januari, Marekani na Uingereza pia zilianza kufanya mashambulizi ya anga kulipiza kisasi, ikiwa ni pamoja na mashambulio kutoka kwa USS Bataan.

"Wahouthi walikuwa wakitumia ndege nyingi zisizo na rubani," anasema Ehrhart. "Wao ni nguvu imara na yenye uwezo," anaongeza, akionya kwamba hawapaswi kupuuzwa.
Ili kupata ufanisi dhidi ya kundi hili la waasi, majini walihitaji kubadili mbibu zao za kivita.
"Tulichukua ndege aina ya Harrier na kuigeuza kuwa ya ulinzi wa anga," Ehrhart ananiambia. "Tuliitumia kubeba makombora na kwa njia hiyo tuliweza kujibu mashambulizi yao ya droni."
Rubani wa kivita mwenye uzoefu, Ehrhart anasema ameangusha ndege saba zisizo na rubani za Wahouthi. Lakini wakati wa kuruka karibu sana na vifaa hivi vya vilipuzi, anasema, ni hatari kubwa.
"Wanatushambulia kila wakati, kwa hivyo tunahitaji kuwa na umakini zaidi. Mifumo yetu inahitaji kurekebishwa ili tuweze kuwa salama."
Chumba cha amri
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya Safari fupi ya helikopta kutoka kwa USS Baatan unafikia Arleigh Burke, meli ya pili ya kivita ya Marekani iliyo kwenye hali ya tahadhari.
Chini yake, inang'aa na mwanga wa vichunguzi kadhaa vya kompyuta, ni Kituo cha Habari cha Kivita.
"Tunapigana kutoka hapa," anasema Luteni Kamanda Tyrchra Bowman. "Huu ndio moyo wa meli yetu."
Wakiwa na mfumo wa hali ya juu wa rada, wafanyakazi wa Arleigh Burke ni macho na masikio kwa meli zote za kivita za Marekani katika eneo hilo. Wanatuma arifa kuhusu tishio lolote linaloonekana kutoka nchi kavu au baharini.
Baadhi ya arifa hizo huenda kwa Kapteni Ehrhart ndani ya USS Bataan, na zinaonyesha ni muda gani atalazimika kujibu mashambulizi ya ndege isiyo na rubani ya Houthi inayokuja.
"Kimsingi ni hesabu. Chumba cha amri kitasema: 'Houthis wamezindua ndege isiyo na rubani ya njia moja. Tuna muda kama huu.' Kisha tunaweza kushuka kutoka wakati wa kujibu wa saa mbili, hadi chini hadi jibu la dakika tano."

Hakuna hata mwanajeshi mmoja kwenye meli ya USS Bataan anayejua ni lini watarudi nyumbani. Huku mvutano ukiongezeka katika eneo lote la mashariki ya kati, misheni ya USS Bataan sasa imepanuliwa hadi ilani nyingine itakapotolewa.
Katika kukabiliana na shambulio la ndege zisizo na rubani za wanamgambo wa Kishia wa Iraq kwenye kambi ya Marekani huko Jordon mwezi uliopita, vikosi vya Marekani vinaendelea kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya Iraq na Syria. Mashambulizi haya ni dhidi ya wale ambao Rais Biden anawaita "makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali wanaoungwa mkono na Iran".
Pamoja na Wahouthi, makundi yote haya ni sehemu ya "mhimili wa upinzani" - neno mwavuli kwa wale wanaoshirikiana na Iran na kudai kwamba mashambulizi yao ni "matokeo ya moja kwa moja ya vita vya Gaza".
Wanamgambo wa Shia Iraq hivi karibuni walitoa wito kwa washirika wake katika mhimili wa upinzani kushambulia bandari za Israeli.
Tishio kama hilo litapinga moja kwa moja operesheni ya USS Bataan.
"Sasa tunaishi katika mazingira magumu na yasiyo na uhakika ya uendeshaji," anasema Kanali Dennis Sampson, afisa mkuu wa meli hiyo. "Kuna wahusika wengi katika mzozo huu na hali inazidi kubadilika."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












