Chris Oyakhilome: Mchungaji wa Nigeria anayesambaza nadharia potofu dhidi ya chanjo ya malaria

Akiwa amevalia suti yake ya shingo ya kuzunguka, Mchungaji Chris Oyakhilome alitazama moja kwa moja kwenye kamera, akitangaza kwamba "hakukuwa na uthibitisho kwamba chanjo ziliwahi kufanya kazi".

Kila mtu alikuwa "amedanganywa" kuhusu chanjo, alisema katika mahubiri yaliyotangazwa kwenye chaneli ya YouTube ya kanisa lake mnamo Februari.

Anajulikana kama "Mchungaji Chris", mwanaume huyo mwenye umri wa miaka sitini ni mmoja wa wahubiri wa kiinjili wanaojulikana sana barani Afrika.

BBC imekagua makumi ya mahubiri yake kutoka 2023 na 2024 na kugundua kwamba amekuwa akieneza ujumbe wa kupinga chanjo kwa wafuasi wake, haswa akilenga chanjo mpya ya ugonjwa wa Malaria ambayo inasambazwa katika nchi za Kiafrika.

Malaria ni tatizo kubwa barani Afrika. Takriban 95% ya vifo vinavyotokana na malaria vilitokea barani humo mwaka 2022, huku watoto chini ya miaka mitano wakichangia karibu 80% ya vifo hivyo, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kampuni ya Mchungaji Oyakhilome pia imetoa takribani filamu tano za dakika 20 za kupinga chanjo zinazotangazwa katika huduma za kanisa au kushiriki kwenye jukwaa lake la utiririshaji wa video, kukwepa sera za kampuni za mitandao ya kijamii dhidi ya maudhui ya kupinga chanjo.

Tangazo la mwaka jana la kutolewa kwa chanjo dhidi ya malaria, baada ya miongo kadhaa ya kujaribu, lilipongezwa na wataalamu kama mafanikio makubwa ambayo yanaweza kuokoa makumi ya maelfu ya maisha.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, kampeni za majaribio za chanjo ya tangu 2019 nchini Kenya, Ghana na Malawi zilisababisha kupungua kwa 13% kwa vifo vya watoto wa umri unaostahili.

Lakini wataalamu wa tiba wanahofia mahubiri ya mchungaji huyo mwenye ushawishi mkubwa yanaweza kuathiri vibaya uchukuaji wa chanjo barani Afrika.

Mnamo Agosti mwaka jana, alionya katika mahubiri ya "ajenda ya uovu ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu''.

Kisha akaeneza nadharia ya njama maarufu katika jumuiya ya kupinga chanjo, kwamba chanjo ni njia ya "kuondoa idadi ya watu duniani".

Pia alisema kwa uwongo kwamba "malaria haikuwa tatizo kwa wale wa Afrika".

"Kueneza habari za uwongo kuhusu chanjo, haswa kutoka kwa watu mashuhuri kama viongozi wa kidini, kunaweza kuchangia kuendeleza hadithi na imani potofu, na hivyo kuchochea kukwama kwa mchakato wa utoaji chanjo.

"Hii inaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya umma, hasa katika kanda ya Afrika ya WHO ambapo magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hutokea mara kwa mara," msemaji wa WHO alisema.

Matamshi ya Mchungaji Oyakhilome yalijumuishwa kama mojawapo ya mwelekeo wa kutoa taarifa potofu "ya kutazamwa" kabla ya utolewaji wa chanjo ya malaria katika ripoti iliyotolewa mwezi Machi na Muungano unaoungwa mkono na WHO wa The Africa Infodemic Response Alliance.

Tulimuuliza mchungaji kuhusu kauli zake dhidi ya chanjo kupitia barua pepe za kampuni yake na kanisa. Hatukupokea jibu.

Alianzisha kanisa la Christ Embassy katika jiji kuu la Nigeria, Lagos, katika miaka ya 1990 na kuendelea kukusanya mamia ya maelfu ya wafuasi duniani kote.

Mnamo 2011, alioneshwa kwenye jarida la Forbes kama mmoja wa wachungaji tajiri zaidi wa Nigeria na wastani wa utajiri wa $30m hadi $50m (£24m hadi £40m).

Kwa mujibu wa jarida hilo, mambo mbalimbali ya kibiashara ya mchungaji huyo yalijumuisha magazeti, majarida, kituo cha televisheni cha ndani, lebo ya rekodi, TV ya satelaiti na hoteli.

Himaya yake, inayoitwa LoveWorld Inc, umekua. Sasa inajumuisha huduma ya utiririshaji, programu ya kutuma ujumbe yenye vipakuliwa zaidi ya milioni moja kwenye duka la programu la Google na benki ndogo ya fedha.

Mara moja kwa wiki, Mchungaji Oyakhilome anahubiri katika uwanja mkubwa wa kambi ya kanisa huko Asese, kando ya Barabara ya Lagos-Ibadan Expressway.

BBC ilipotembelea kanisa hilo mwezi Novemba mwaka jana, mamia ya wachungaji kutoka mataifa mbalimbali walijaza ukumbi wake kwa ajili ya kongamano la kila mwaka. Bendera za nchi kadhaa zilioneshwa ndani.

"Mafundisho yake makubwa ya mtandaoni na huduma za uponyaji" yana mahudhurio ya kimataifa ya "watu bilioni 7", kulingana na tovuti ya Christ Embassy, hii ni kutokana na kwamba idadi ya watu inakadiriwa kuwa bilioni nane.

Winnifred Ikhianosin, 25, ni mtu wa kawaida kanisani. Aliiambia BBC kuwa anakataa kuchukua chanjo.

"Mtu wa Mungu alituambia," alisema. "Na pia nimefanya utafiti wangu."

Kulingana na Ada Umenwaliri, mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha Mafunzo ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha North Carolina chenye makao yake Marekani, Mchungaji Oyakhilome ana "ngome kubwa kwa wafuasi wake wanaomtegemea".

"Wachungaji na viongozi wa kidini watakuwa na jukumu muhimu katika chaguzi ambazo wafuasi wao hufanya," aliongeza.

Lakini umaskini na ukosefu wa miundombinu ya afya barani Afrika vinaweza kuwezesha makanisa kuwa na uwezo mkubwa wa kuwadhibiti watu linapokuja suala la chanjo, alisema.

Katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya habari ya Nigeria, The Cable, mwaka jana, mwandishi Julius Ogunro, ambaye alihudhuria kanisa la mchungaji huyo kwa zaidi ya muongo mmoja, alisema: "Tunahitaji kupiga kengele sasa. Ajenda ambayo Mchungaji Chris anaisukuma, inaweza kuwa hatari na haina uhusiano wowote na imani ya Kikristo."

Jina moja linarudiwa mara kwa mara na Mchungaji Oyakhilome: Bill Gates. Bilionea huyo ni mmoja wa wafadhili wakuu wa chanjo ya malaria, lakini pia amekuwa chini ya nadharia za njama za chanjo kwa miaka.

Katika mahubiri ya Agosti 2023, mchungaji alirusha kipande cha video kutoka kwenye mazungumzo ya TED Bill Gates aliyotoa mwaka wa 2010 kama mfano wa "wale ambao wana ajenda ya kupunguza idadi ya watu duniani".

Alipokuwa akitoa hotuba kuhusu kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa, Bw Gates alisema: "Kwanza, tuna idadi kubwa ya watu. Dunia leo ina watu bilioni 6.8. Hiyo inaelekea kufikia takribani bilioni tisa.

Sasa, ikiwa tutafanya kazi kubwa sana kwenye chanjo mpya, huduma za afya, huduma za afya ya uzazi, tunaweza kupunguza hilo kwa pengine asilimia10 au 15.

Tamko lake lilitolewa nje ya muktadha na Mchungaji Oyakhilome. Bw. Gates hakutetea kupungua kwa watu duniani.

Amefafanua hapo awali kwamba aliona ukuaji wa idadi ya watu na uboreshaji wa afya kama nyongeza: "Afya inapoboreka, familia huchagua kuwa na watoto wachache."

Bw.Oyakhilome pia alisema kuwa kituo cha Mpango wa Dunia wa kupambana na Mbu nchini Colombia ni cha Gates Foundation, akikishutumu kwa kuzalisha mbu waliobadilishwa vinasaba kama mkakati wa kupunguza idadi ya watu.

Kiwanda cha mbu, kilichoanzishwa ili kupunguza uwezo wa mbu kusambaza virusi, ni cha kundi lisilo la faida la kampuni zinazomilikiwa na Chuo Kikuu cha Monash nchini Australia, na kimesisitiza kuwa njia yake haihusishi matumizi ya viumbe vilivyobadilishwa vinasaba.

Mchungaji Oyakhilome si mgeni katika taarifa za kutokomeza chanjo. Hivi karibuni pia amelenga chanjo ya human papillomavirus (HPV), iliyokusudiwa kuwalinda wanawake dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi.

"Wana nia nyingine, Sio kuhusu saratani," alisema wakati wa ibada iliyopeperushwa mnamo 2 Septemba 2023.

Nigeria ilianza kampeni kubwa ya chanjo kwa wasichana mnamo Oktoba 2023 katika juhudi za kupunguza viwango vya saratani ya shingo ya kizazi.

Ugonjwa huo unagharimu maisha ya zaidi ya wanawake 8,000 nchini Nigeria kila mwaka. Mnamo 2021, utafiti mkubwa uliofadhiliwa na Utafiti wa Saratani Uingereza uligundua chanjo ya HPV ilikuwa kupunguza visa vya saratani ya shingo ya kizazi kwa karibu 90%.

Hapo awali, Mchungaji Oyakhilome alitoa madai mengi yasiyo na msingi kuhusu sindano za kuzuia pepopunda, chanjo ya polio, na chanjo nyingine za utotoni.

Mchungaji pia alisema kwa uwongo kwamba chanjo ya RNA ya mjumbe inabadilisha DNA.

Lakini chanjo haibadilishi DNA za watu. Inachukua sehemu ya nyenzo za kijeni za virusi au messenger RNA, kufanya mfumo wa kinga kujifunza kuitambua na kutoa kingamwili.

Wakati wa janga la Covid, kanisa la Mchungaji Oyakhilome lilipigwa faini ya £125,000 ($155,000) kutoka kwa mdhibiti wa vyombo vya habari wa Uingereza Ofcom.

Ilisema mtandao wake wa Loveworld, unaotangazwa nchini Uingereza, ulionesha "taarifa za kupotosha na zinazoweza kudhuru kuhusu janga la corona na chanjo".

Bw Ogunro, mwandishi aliyeacha kuabudu katka kanisa hilo, alisema ana wasiwasi kuhusu ushawishi wa mchungaji huyo.

"Madai yake kuhusu chanjo yananitisha. Tunahitaji kutafuta njia ya kuwadhibiti wahubiri kama yeye."