'Je, niko hai kweli?': Operesheni tete ya kuwaokoa dada wawili waliofukiwa kwenye kifusi

Merve baada ya kutolewa nje ya kifusi aliuliza: "Niko hai kweli?"
Maelezo ya picha, Merve baada ya kutolewa nje ya kifusi aliuliza: "Niko hai kweli?"

"Merve! Irem! Merve! Irem," mfanyakazi wa uokoaji Mustafa Ozturk anapaza sauti. Kila mtu karibu nasi ameamriwa kunyamaza. Timu hiyo ya waokoaji inawasaka dada wawili ambao manusura wengine wanasema wamenaswa wakiwa hai chini ya rundo la vifusi.

Kwa kutumia vifaa maalum wanajaribu kusikiza sauti yoyote. Kila mtu anasikiza kwa makini

Na kisha, wanafanikiwa kusikia sauti kutoka chini ya vifusi. "Irem, mpenzi wangu, mimi nipo karibu na wewe, unanisikia, sio?" Mustafa anasema.

Baadhi yetu tunaofuatilia tukio hili hatusikii kinachoendelea, lakini ni wazi sasa kwamba anajibu. Kikundi kidogo cha marafiki wa wasichana hao wanasubiri kimya karibu nasi.

"Wewe ni mzuri sana! Sasa tulie na unijibu. Ah ok, huyo ni Merve. Merve mpenzi, jibu maswali yangu tu," anasema.

Merve, 24, na dada yake Irem, 19, walinaswa chini ya vifusi vya jengo lao la orofa tano huko Antakya, kusini mwa Uturuki, ambalo liliporomoshwa na tetemeko la ardhi. Ilikuwa imepita siku mbili, lakini kwao siku hizo zilihisi kama wiki.

"Ni Jumatano. Hapana! Hukunaswa kwa siku 14. Tupatie dakika tano. Utakuwa nje."

Mustafa anajua itachukua saa nyingi zaidi ufanya hivyo, lakini anatuambia: "Watapoteza matumaini huenda wasinusurike."

Waokoaji wanaweza kuwasikia Merve na Irem ambao wamenaswa kwa siku kadhaa chini ya vifusi vya jengo lao la ghorofa
Maelezo ya picha, Waokoaji wanaweza kuwasikia Merve na Irem ambao wamenaswa kwa siku kadhaa chini ya vifusi vya jengo lao la ghorofa

Merve na Irem wanaanza kutania na kucheka pamoja. Ninaweza kuona tabasamu kubwa kwenye uso wa Mustafa: "Kama wangekuwa na nafasi labda wangecheza," anasema.

Kwa hesabu za waokoaji ni mita 2 (futi 6.6) kuwafikia akina dada hao lakini Hasan Binay, kamanda wa timu ya uokoaji, anasema kuchimba handaki itakuwa operesheni nyeti sana. Hatua moja mbaya inaweza kusababisha janga.

Tingatinga yaletwa kuinua kidogo na kushikilia saruji nene ili kuzuia jengo kuporomoka wanapoanza kuchimba.

"Wasichana, hivi karibuni tutawapa blanketi." Mustafa anawaambia dada hao. "Ah hapana, usiwe na wasi wasi sisi tuko sawa."