Mauaji ya siri Saudi Arabia: 'Hatujui kama walizikwa au walitupwa jangwani'

Saudi Arabia imetekeleza hukumu ya kifo kwa wafungwa bila ya kuziarifu familia zao

Saudi Arabia imetekeleza hukumu ya kifo kwa wafungwa bila kuarifu familia zao, jamaa za baadhi ya wale waliohukumiwa kifo wameambia BBC.

Kiwango cha unyongaji nchini humo kimekaribia maradufu tangu mwaka 2015, kwa mujibu wa ripoti mpya. Mfalme Salman na mwanawe Mohammed bin Salman walichukua madaraka mwaka huo.

Familia ya Mustafa al-Khayyat haikuambiwa angenyongwa.

Bado hawana miili ya kuzika, hawana makaburi ya kutembelea. Mara ya mwisho kusikia kutoka kwake ilikuwa wakati wa simu aliyowapigia kutoka gerezani. Mwanaume huyo aliagana na mama yake kwa maneno haya: "Sawa, ni lazima niende. Ninafurahi kuwa uko sawa.

Hakuna hata mmoja wao aliyeshuku kwamba hii ingekuwa mara ya mwisho wao kuzungumza wao kwa wao.

Mwezi mmoja baadaye, Mustafa alikufa. Alikuwa miongoni mwa wanaume 81 walionyongwa mnamo Machi 12, 2022, katika mauaji makubwa zaidi katika historia ya kisasa ya Saudi Arabia.

Orodha ambayo inaendelea kukua

Jina la Mustafa liko kwenye orodha ndefu na inayokua iliyoandaliwa na kundi la Reprieve ambalo, pamoja na Shirika la Haki za Kibinadamu la Euro-Saudi, liliandika kwa taarifa za kunyongwa na kutengeneza ripoti

Ingawa karibu mwaka mmoja umepita tangu kunyongwa kwa Mustafa al-Khayyat, familia yake haijapokea mwili wake kwa ajili ya mazishi.

Chanzo cha picha, CORTESÍA FAMILIA AL-KHAYYAT

Kwa kutumia data iliyokusanywa tangu 2010, utafiti uligundua kuwa:

  • Kiwango cha kunyongwa nchini Saudi Arabia kimeongezeka karibu maradufu tangu Mfalme Salman alipochukua madaraka ya nchi hiyo mwaka 2015 na kumteua mwanawe Mohammed bin Salman kushika nyadhifa kuu serikalini.
  • Adhabu ya kifo imekuwa ikitumika mara kwa mara kuwanyamazisha wapinzani na waandamanaji, kinyume na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ambayo inasema inapaswa kutumika tu kwa uhalifu mkubwa.
  • Takribani 11 kati ya walionyongwa tangu 2015 walikuwa watoto walipokamatwa, licha ya madai ya mara kwa mara ya Saudi Arabia kwamba inaweka kikomo matumizi ya hukumu ya kifo dhidi ya watoto wadogo.

Mateso ni "tabia" katika magereza ya Saudia, hata kwa washtakiwa wadogo.

Hakuna taarifa yoyote

Kama mwaka mmoja hivi baadaye, mamlaka bado haijaiambia familia ya Mustafa jinsi yeye na wengine walivyonyongwa. Kaka yake mkubwa, Yasser, alisema ni msiba kwa familia.

"Hatujui walizikwa kwa heshima au walitupwa jangwani au baharini. Hatujui," alisema.

Yasser anazungumza hadharani kuhusu kesi hiyo kwa mara ya kwanza. Sasa anaishi Ujerumani, ambako alipewa hifadhi ya kisiasa baada ya kutoroka Saudi Arabia mwaka wa 2016, akihofia hatima sawa na kaka yake.

Kaka wa mtu aliyeuawa alisema alikuwa "mcheshi, mcheshi na maarufu". Tangu mwaka 2011, Mustafa amekuwa akishiriki kila siku katika maandamano ya Washia walio wachache nchini humo dhidi ya serikali ya Saudia, hadi alipokamatwa mwaka 2014.

Yasser al-Khayyat alidai mdogo wake, Mustafa, aliteswa akiwa kizuizini kwa kushiriki katika maandamano dhidi ya serikali ya Saudia.

Chanzo cha picha, CORTESÍA FAMILIA AL-KHAYYAT

Baada ya kifo chake, mamlaka ilitoa taarifa ikisema mtu huyo, pamoja na watu wengine 30, walinyongwa kwa makosa ya uhalifu ikiwa ni pamoja na jaribio la mauaji ya walinzi, ubakaji, wizi, kutengeneza mabomu, fujo, pamoja na ulanguzi wa silaha na dawa za kulevya.

"Hawakuwahi kutoa ushahidi wowote. Uongo huu ni wa kina," alisema Yasser, ambaye alisema kaka yake alikuwa bado anajaribu kukata rufaa dhidi ya hukumu yake wakati mamlaka ilipomuua yeye na wanaume wengine 80.

"Sio tu kwamba walichukua maisha yao, lakini waliwachafua kwa makusudi na kuwashutumu kwa mambo ambayo hawakufanya," aliongeza.

Ukandamizaji wa kiwango cha juu

Baada ya kuingia madarakani, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, mtawala mkuu wa Saudi Arabia, aliahidi kufanya ufalme huo kuwa wa kisasa na alisema katika mahojiano ya 2018 kwamba nchi yake, mshirika mkuu wa Magharibi, inajaribu "kupunguza" matumizi ya hukumu ya kifo.

Hata hivyo karibu miaka mitano baadaye, Saudi Arabia inasalia kuwa miongoni mwa wanyongaji wakubwa duniani. Na hii, licha ya mapumziko ambayo yaliambatana na urais wa nchi wa G20 na kuanza kwa janga la Covid-19.

Mwana wa mfalme wa Saudia

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwana wa mfalme "amefanya kinyume kabisa na kile alichoahidi", Maya Foa, mkurugenzi wa Reprieve, alisema kutoka ofisi yake mashariki mwa London, Uingereza.

"Alisimamia idadi kubwa ya mauaji na ukandamizaji wa kikatili wa washiriki katika maandamano ya kuunga mkono demokrasia," aliongeza.

Aliongeza kuwa hukumu ya kifo imezungukwa na utawala wa usiri na kueleza kuwa katika visa vingi vilivyofanyiwa utafiti na Reprieve, wafungwa hawakujua kuwa wako kwenye hukumu ya kifo.

"Ndugu zao hawakujua. Kwa hiyo kuna watu walikamatwa, wakashitakiwa, wakahukumiwa kifo na kisha kunyongwa kwa siri," alisema.

Baadhi ya familia ziligundua tu kupitia mitandao ya kijamii kwamba wapendwa wao waliuawa, Bi Foa alisema, akielezea ukosefu wa taarifa rasmi kama mojawapo ya mambo "ya ukatili na ya kutisha".

Mfumo wa haki wa Saudia umeelezewa kuwa "wa kusikitisha" na mashirika kama vile Human Rights Watch.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kukata kichwa kwa jadi ni njia kuu ya utekelezaji nchini Saudi Arabia.

Unyongaji ulifanyika hadharani na majina ya waliouawa na mashtaka dhidi yao yalichapishwa kwenye tovuti za serikali.

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wanasema matumizi ya hukumu ya kifo yamekuwa wazi zaidi.

Hakuna hata mmoja anayejua hasa jinsi mauaji yanavyofanywa sasa, ingawa walisema vikosi vya kufyatua risasi pia vinatumika.

Adhabu ya kifo ni sehemu ya mfumo wa kisheria nchini humo ambao "asili hauko wa haki", alisema Ali Adubisi, Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Kibinadamu la Euro-Saudi lenye makao yake mjini Berlin.

"Hakuna mashirika huru ya kiraia au makundi ya haki za binadamu yanaweza kufanya kazi huko. Kama hatungetoa tahadhari kwenye mauaji, watu wangekufa kimyakimya," alisema. .

Human Rights Watch ilisema kuwa wanaume 41 kati ya 81 walionyongwa mwezi Machi walikuwa watu wachache wa Shia na kwamba "unyanyasaji mkubwa na wa kimfumo wa haki ya jinai wa Saudi Arabia unaonesha kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba yeyote kati ya watu hawa akapata kesi ya haki".

Kundi hilo pia lilisema limepokea ripoti za kuteswa.

Mashirika ya haki za binadamu yamelalamika kuwa watu wengi walionyongwa nchini Saudi Arabia hawakuambiwa hata hukumu yao hadi wakati wa kunyongwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

BBC ilituma barua pepe tatu kwa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Saudi, chombo cha serikali, ikiomba kuzungumza na afisa, lakini haikujibiwa.

Katika taarifa iliyotumwa kwa BBC na Ubalozi wa Saudia mjini London, inasemekana kuwa mataifa mengine mengi duniani yanatumia hukumu ya kifo na kwamba kila nchi ina maoni yake kuhusu hukumu zinazofaa kwa uhalifu fulani.

"Kama vile tunavyoheshimu haki ya nchi nyingine kutunga sheria zao, tunatarajia wengine kuheshimu haki yetu kuu ya kufuata chaguzi zetu za mahakama na sheria," taarifa hiyo ilieleza.

Wawakilishi hao, hata hivyo, hawakushughulikia ongezeko kubwa la mauaji wakati wa utawala wa mwana mfalme au jinsi hukumu ya kifo inavyotekelezwa kinyume na viwango vya kimataifa.