Je, Papa Francis alifanya vya kutosha kupambana na unyanyasaji wa watoto?

    • Author, John Sudworth
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Makadinali 133 watapokutana mjini Roma ili kuamua Papa anayefuata, maswali kuhusu urathi wa Papa aliyefariki yatazuka katika majadiliano yao.

Kwa Kanisa Katoliki, eneo gumu ni jinsi Papa Francis alivyoshughulikia unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto unaofanywa na makasisi.

Ingawa inaeleweka kuwa alikwenda mbali zaidi kuliko watangulizi wake katika kuwatambua waathiriwa na kurekebisha taratibu za ndani za Kanisa, waathiriwa wengi hawafikiri kwamba alikwenda mbali vya kutosha.

Unyanyasaji wa watoto

Unyanyasaji dhidi ya Alexa MacPherson kutoka kwa kasisi wa Kikatoliki ulianza akiwa na umri wa miaka mitatu na kuendelea kwa miaka sita.

"Nilipokuwa na umri wa miaka tisa na nusu, baba yangu alimkamata akijaribu kunibaka kwenye kochi la sebuleni," aliniambia tulipokutana kwenye ukingo wa mto wa Boston.

"Kwangu mimi, lilikuwa ni tukio la kila siku."

Alipogundua unyanyasaji huo, baba yake aliita polisi. Kesi ya jinai dhidi ya kasisi Peter Kanchong, aliyeshtakiwa kwa kumyanyasa na kusababisha madhara kwa mtoto, ilipangwa tarehe 24 Agosti 1984.

Lakini bila familia hiyo kujua, jambo la ajabu lilikuwa likifanyika nyuma ya pazia. Kanisa - taasisi ambayo ina nguvu kubwa - iliamini kwamba mahakama iko upande wa kanisa.

"Mahakama inashughulikia suala hilo kwa njia ya kumsaidia Kasisi Peter na kuepusha kashfa kwa Kanisa," Askofu Mkuu wa wakati huo wa Boston, Bernard Law, aliandika katika barua ambayo ilibaki siri kwa miaka mingi.

Bi MacPherson anatambua kwamba unyanyasaji dhidi yake ulifanyika miaka mingi nyuma kabla ya Francis kuwa Papa. Lakini mfululizo wa kashfa za unyanyasaji ambazo bado zinaendelea kujitokeza, dhidi ya watoto, ni changamoto kubwa kwa Kanisa.

Ni changamoto ambayo anaamini Papa Francis alishindwa kuikabili. Kwani aliweka wazi nilipomuuliza amepokea vipi taarifa za kifo chake.

"Sitaki kuondoa mema ambayo aliyafanya, lakini kuna mengi zaidi ambayo Kanisa na Vatikani na watu wanaolisimamia wanaweza kuyafanya."

Barua ya 1984 kutoka kwa Askofu Mkuu Bernard Law iliyotumwa kwa askofu huko Thailand. Ni barua iliyoandikwa miezi miwili baada ya kusikilizwa kwa kesi hyo katika mahakama ya Boston, ambayo kwa hakika ilihitimisha kwamba hakuna kashfa yoyote kwa Kanisa.

Peter Kanchong - ambaye alikuwa anatoka Thailand - aliondolewa mashtaka rasmi ya uhalifu na kupewa muda wa kutazamwa wa mwaka mmoja kwa sharti kwamba akae mbali na familia ya MacPherson na afanyiwe matibabu ya kisaikolojia.

Licha ya tathmini ya kisaikolojia ya Kanisa ilihitimisha kuwa kasisi aliyeshtakiwa "hakusikia tiba za kisaikolojia" na kwa hiyo anapaswa "kulazimishwa kukabiliana na matokeo ya matendo yake" chini ya sheria ya kiraia na ya Kanisa.

Lakini badala ya kufanyia kazi ushauri huo, Askofu Mkuu wa Boston, alimsihi askofu wa Thailand amrejeshe mara moja Peter Kanchong katika dayosisi yake nchini Thailand, akisema kwamba "kashfa" itakuwa kubwa ikiwa atabaki Marekani.

Ingawa ripoti za vyombo vya habari wakati huo zinaonyesha kwamba viongozi wa Kanisa nchini Thailand walikubali kumrudisha, Peter Kanchong hakutaka kurudi, akatafuta kazi katika eneo la Boston kwenye kituo cha watu wazima wenye matatizo ya kusoma.

Mwaka 2002, zaidi ya miaka 18 baada ya babake Bi MacPherson kuwaita polis, barua ya askofu mkuu iliwekwa wazi.

Barua yafichuka

Katika uamuzi wa kihistoria, ilikuwa moja ya maelfu ya hati ambazo mahakama ya Boston ililiamuru Kanisa Katoliki izitoea hadharani hati hizo.

Gazeti la The Boston Globe, kwa mara ya kwanza, lilianza kuipa changamoto taasisi hiyo katika jiji hilo, kwa kuweka habari za waathiriwa kwenye kurasa zake za mbele.

Alipotafutwa wakati huo, Peter Kanchong alikanusha madai hayo. "Una ushahidi? Una mashahidi?" aliiambia Boston Globe, ambayo ilimkuta bado anaishi katika eneo hilo.

Bi MacPherson, alikuwa mmoja wa waathiriwa zaidi ya 500 ambao walishinda kesi ya madai ya dola milioni 85 kwa unyanyasaji walioupitia.

Hati za Kanisa zilionyesha kwamba, mara kwa mara, Askofu Law alishughulikia kesi za unyanyasaji kwa njia ile ile aliyoshughulikia kesi ya Peter Kanchong - kwa kuwahamisha Mkasisi kwenda parokia mpya.

Baada ya kesi hizo, Kadinali, Bernard Law alijiuzulu kutoka wadhifa wake huko Boston na kuhamia Roma.

Na huko alipewa heshima kwa kupewa wadhifa wa miaka saba kama Kasisi Mkuu wa kanisa la Basilica di Santa Maria Maggiore, jengo ambalo Papa Francis amezikwa sasa.

Papa na kesi za unyanyasaji

Mwaka 2019, Papa Francis aliwaita zaidi ya maaskofu mia moja kwenda Roma kwa mkutano juu ya tatizo la unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto. Aliwaambia, "Tunaona mkono wa uovu."

Mkutano huo ulisababisha marekebisho ya sheria ya Kanisa na kuruhusu ushirikiano na mahakama za kiraia inapohitajika katika kesi za unyanyasaji.

Marekebisho hayo, hata hivyo, hayalazimishi ufichuaji wa taarifa zote zinazohusiana na unyanyasaji wa watoto. Ufichuaji wa taarifa hufanyika katika matukio maalumu pale ombi rasmi la mamlaka halali linapotumwa.

Vile vile, sheria mpya inayotaka madai yapelekwe kwenye uongozi wa ndani wa Kanisa, sheria hiyo haiamuru kesi hizo zipelekwe polisi.

Wakili wa Bi MacPherson, Mitchell Garabedian, aliniambia kuna mambo mengi ambayo Kanisa linaendelea kuficha.

"Ili kupata hati hizo, lazima kwanza tufungue kesi mahakamani, hakuna kilichobadilika," anasema.

Ushindi wake wa kisheria 2002, ukifuatiwa na wimbi la kesi kama hizo katika nchi kadhaa ni mafanikio makubwa, lakini hana shaka kwamba kesi bado hufichwa katika makanisa duniani kote.

Ms MacPherson anataka Kanisa lifichue kila kitu linachokijua. Watu wanaoificha, wanatakiwa wawajibishwe katika mahakama ya kawaida na sio kuwalainda na kuwaficha."

Hadi sasa Peter Kanchong mwenye umri wa miaka 85 hajawahi kuhukumiwa kwa kosa lolote. Wala hajavuliwa cheo chake, ingawa amezuiwa kushikilia wadhifa wowote rasmi katika Dayosisi ya Boston.

Orodha ya Kanisa iliyochapishwa kuhusu makasisi wanaoshutumiwa inayonyesha kesi yake "bado haijatatuliwa" hakuna uamuzi wa mwisho wa hatia au kutokuwa na hatia.

Ms MacPherson anasema Kanisa limebadilisha jina la parokia ya Boston ambako alinyanyaswa - anaamini hilo limefanyika, kujaribu kuanza upya baada ya kile kilichotokea.

BBC imeiuliza Dayosisi ya Boston kuhusu urathi wa Papa Francis na pia madai kwamba Kanisa Katoliki linalea utamaduni wa usiri juu ya rekodi zake za ndani.

Hatukupata majibu ya maswali hayo.

Pia tuliuliza ikiwa Askofu mkuu wa sasa anaweza kufanya lolote kusaidia waathiriwa wanaotaka kasisi kuondolewa katika wadhifa wake.

Tulielekezwa twende Vatikani.

Kanisa Katoliki linapoanza kumchagua Papa mpya, Bi MacPherson ana matumaini madogo ya mageuzi.