'Tuliambiwa alikufa kutokana na njaa'

Chanzo cha picha, Family Handout
- Author, Bushra Mohamed
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ni katika eneo la Yaqshid iliyoko Mogadishu, mpakani Somalia,ambalo familia ya Fathi Hussein mwenye umri wa miaka 26 imejawa na simanzi.
Familia hiyo inasimulia siku za mwisho za Fathi kwa majonzi.
“Tulijulishwa na manusura kuwa Fathi alifariki kutokana na njaa,”dada wa kambo Samira anaiambia idhaa ya BBC kupitia simu.
“Walikuwa baharini kwa takriban siku 14 na walikuwa wakila samaki wabichi na kunywa maji ya bahari ambayo inasemekana alikataa kubugia.Walitueleza alianza kuota njozi kabla kufariki.Na baadaye wakatupa mwili wake baharini.”
Mamlaka husika inaeleza kuwa Fathi alikuwa miongoni mwa raia 24 wa Somalia waliofariki baada ya boti mbili zilizokuwa zimepakia watu 70 kupinduka na kuzama katika pwani ya Madagascar.
Manusura wa ajali hiyo wanasema kuwa walikuwa wakijaribu kufikia katika kisiwa cha ufaransa eneo la Mayotte,njia ambayo ni hatarishi kwa wakimbizi wanaotafuta hifadhi wa asili ya Somalia.
Mamia ya wakimbizi wanaaminikia kufariki kila mwaka wakijaribu kufika kisiwa cha Ufaransa ,kilicho umbali wa maili 190 kaskazini magharibi kutoka Madagascar katika bahari hindi.
Mnamo Novemba mosi,Fathi alihepa kutoka Somalia hadi bandari ya Mombasa nchini Kenya na baadaye kuabiri boti aliyoamini itamfikisha Mayotte salama.
Samira anasema Fathi aliambia dadake mdogo kuwa alipata nauli ya kupanda boti hiyo baada ya kuweka akiba alipokuwa akijishughulisha na biashara ya saluni lakini aliifanya siri.
“Fathi alikuwa hapendi bahari,na sijui ni kwanini aliamua kuchukua mkondo huo ,natamani nimuone nimpe pambaja,”anasema Samira.
BBC imezungumza na wakimbizi watano kama vile Fathi ambaye alijaribu kufika kisiwa cha Mayotte.
Walieleza kuna njia mbili ambazo hufuatwa ili kufikia kisiwa hicho kutoka Somalia.
Wengine hutumia boti kutoka bandari ya Mombasa kupitia kisiwa cha Comoros, na walio na kipato zaidi kutumia ndege kutoka Ethiopia hadi Madagascar-kwasababu walio na vibali vya pasipoti huidhinishwa visa wanapofika- kisha wanachukua boti ndogo na kuwapeleka Mayotte.
Wanakimbilia Mayotte kwasababu wanaamini ukiwa katika kisiwa hicho ni rahisi kupata pasipoti ya Ufaransa na kuingia Ulaya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wageni wapya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mayotte ni sehemu ndogo ya Ufaransa katika Bahari ya Hindi, lakini miaka michache iliyopita imekuwa uwanja wa vita kuhusu sheria za uhamiaji.
Tangu 1841 Mayotte imekuwa sehemu ya Ufaransa, sasa ni idara au kaunti ya Jamhuri ambayo inamaanisha, kwa nadharia, sheria sawa za kupata pasipoti zinatumika hapo kama mahali pengine popote nchini Ufaransa.
Lakini wimbi la hivi karibuni la wahamiaji linaisukuma serikali ya Rais Emmanuel Macron kuachana na kanuni ya Ufaransa ya usawa kwa wote.
Akiwa ziarani huko Mayotte mwezi Februari mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani Gérald Darmanin alitangaza kwamba haki ya moja kwa moja ya uraia wa Ufaransa kutokana na kuzaliwa katika kisiwa hicho itafutwa.
Mabadiliko ya katiba kwa lengo la kufikia mpango huo inafuatiliwa na serikali. Mwisho wa kanuni ya "uraia wa kuzaliwa" hutumika tu kwa wakazi wa Mayotte - sio kwa Ufaransa kwa ujumla.
Lakini hii haijawazuia wahamiaji kufikia kisiwa hicho.
Familia ya Fathi inasema safari yake iliishia kwa msiba wakati boti ndogo aliyokuwa akisafiria ilipopotea baharini.
Waliambia BBC kwamba wakati hayo yakifanyika, wasafirishaji haramu waliondoa injini kutoka kwa boti na kurudi Kenya. Waliwaacha raia hao wa Wasomalia waliokwam, wakielea baharini.
Wasafirishaji haramu waliwaambia, "Mtafika Mayotte baada ya saa tatu, ambazo ziligeuka kuwa siku 14,'' Samira anasema.
Frantz Celestin, Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki, Upembe na Kusini mwa Afrika wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa anasema hali inaendelea kuwa ya kawaida kwa wahamiaji ambao wanatarisha maisha yao kujaribu kufikia kisiwa hicho cha Ufaransa.
"Hivi karibini watu 25 waliangamia wakifanya safari kama hiyo, kwa kawaida wakipitia Comoro na Madagascar, kwa ujumla mwaka huu umekuwa mwaka mbaya zaidi kwa wahamiaji," anasema.

Ahadi ya maisha mapya
Mmoja wa watu wachache waliobahatika ambao wamenusurika katika njia hii hatari ni Khadar Mohammed.
Aliwasili Mayotte miezi 11 iliyopita lakini anakumbuka masaibu aliyopitia kufika katika kisiwa hicho kidogo kutoka Madagascar.
‘’Nilipofika Madagascar, nilipelekwa nyumbani kwa mwenye boti, tukakaa huko kwa siku 14, tulikuwa mchanganyiko wa raia wa Somalia na Madagascar,” anasema.
Wale waliokuwa wakisubiri kusafiri walikua takriban watu 70. Waliwekwa kwenye botina kupelekwa kupitia mkondo wa mto hadi kwenye bahari kuu.
Khadar anasema aliondoka Somalia kwa sababu ya hali ya usalama inayoendelea. Anaamini hakuwa na budi kwani maisha yake yalikuwa hatarini kwa sababu alilengwa na kundi la kigaidi la Kiislamu la al-Shabab.
"Niliondoka nchini mwangu kwa usalama wangu. Nilikuwa mfanyabiashara, na sikuweza kufanya kazi yangu kwa sababu ya al-Shabab,” anasema.
Familia za waathiriwa zilizozungumza na BBC zilisema wapendwa wao waliahidiwa maisha mapya na walanguzi ambao waliwalipa $6000 kusafiri kutoka Mombasa hadi Mayotte. Nusu ya pesa inalipwa mbele. Kwa wengi inaweza kuchukua miaka kuweka akiba.
BBC imeona akaunti kwenye mitandao ya kijamii, TikTok, zikitangaza safari kama hizo za kuenda Mayotte na sehemu zingine za Uropa.
Matangazo hayo yanadai waendeshaji wanaweza kuwapeleka watu Mayotte kwa kutumia boti kubwa za watalii, lakini familia za waathiriwa wanasema wasafirishaji haramu wanatumia boti ndogo zaidi za uvuvi za kienyeji zinazoitwa kwassa.
Serikali ya Ufaransa haijatoa maoni lolote kuhusu mkasa huo wa hivi majuzi. Lakini Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Somalia, Ahmed Macallin Fiqi, anasema kuwa serikali ya Madagascar ilimfahamisha kwamba wahamiaji wa Somalia walizama kwenye boti mbili kwenye pwani ya nchi hiyo.
Waziri huyo aliongeza kuwa serikali yake inafanya juhudi kuwasiliana na walionusurika na kuwarejesha Somalia. Waziri wa Habari wa Somalia Daud Aweis aliiambia BBC Jumatano wiki iliyopita kwamba serikali inatuma wajumbe nchini Madagascar wiki hii.
Wakati huo huo, familia za waliofariki zinaendelea kuomboleza.
Familia ya Fathi inasema ilimripoti mlanguzi aliyemchukua binti yao, na kukamatwa. Hata hivyo, ameachiliwa kwa dhamana.
Samira anasema kutojua jinsi dadake alihisi katika dakika zake za mwisho ni maumivu ambayo atasalia nayo milele.
‘’Natamani angezungumza nami na kunieleza kuhusu uamuzi wake. Angeweza kuniambia kwaheri ... sasa, sijui jinsi ya kushughulikia kifo chake, "anasema.
Maelezo ya ziada na Marina Daras.
Imetafsiriwa Maryam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi












