India yapiga marufuku dawa zinazolevya zenye soko kubwa Afrika

Muda wa kusoma: Dakika 3

Mamlaka ya India imepiga marufuku dawa mbili za kulevya zenye uraibu kwa kujibu uchunguzi wa BBC ambao uligundua kuwa zilikuwa zikichochea mzozo wa afya ya umma katika baadhi ya maeneo ya Afrika Magharibi.

Katika barua iliyoonekana na BBC kutoka kwa Mdhibiti Mkuu wa Dawa za Kulevya nchini India, Dkt Rajeev Singh Raghuvanshi alisema ruhusa ya kutengeneza na kuuza nje ya nchi dawa hizo imeondolewa.

BBC Eye iligundua kampuni moja ya dawa, Aveo, imekuwa ikisafirisha kinyume cha sheria mchanganyiko hatari wa tapentadol na carisoprodol katika nchi kama Ghana, Nigeria, na Ivory Coast.

Utawala wa Taasisi ya udhibiti wa Chakula na Dawa nchini India ulisema kuwa kiwanda cha kampuni hiyo huko Mumbai kilivamiwa na kukamatwa kwa hisa zake zote.

Unaweza kusoma

Waraka huo wa Ijumaa kutoka kwa Dk Raghuvanshi, ulitaja uchunguzi wa BBC katika uamuzi wake wa kupiga marufuku michanganyiko yote ya tapentadol na carisoprodol, ambayo ilitekelezwa mara moja.

Alisema hii pia ilikuja baada ya maafisa kuangalia "uwezo wa matumizi mabaya ya dawa na athari zake mbaya kwa idadi ya watu".

Tapentadol ni dawa yenye nguvu, na carisoprodol ni dawa ya kutuliza misuli kwa hivyo inalevya pia imepigwa marufuku Ulaya.

Carisoprodol imeidhinishwa kutumika nchini Marekani, lakini kwa muda mfupi tu wa hadi wiki tatu. Dalili za kujiondoa ni pamoja na wasiwasi, usingizi na kuweweseka.

Mchanganyiko wa dawa hizo mbili hauna leseni ya kutumika popote duniani kwani zinaweza kusababisha matatizo ya kupumua na kifafa na zinaweza kuua.

Licha ya hatari, opioid hizi ni dawa maarufu za mitaani katika nchi nyingi za Afrika Magharibi, kwa sababu ni za bei nafuu na zinapatikana kirahisi sana.

Data ya mauzo ya nje inayopatikana kwa umma inaonesha kuwa Aveo Pharmaceuticals, pamoja na kampuni dada inayoitwa Westfin International, imesafirisha mamilioni ya vidonge hivi hadi Ghana na nchi nyingine za Afrika Magharibi.

BBC pia ilipata pakiti za tembe hizi zenye nembo ya Aveo zinazouzwa katika mitaa ya Nigeria, na katika miji ya Ivory Coast.

Nigeria, yenye idadi ya watu milioni 225, imekuwa soko kubwa zaidi la tembe hizi.

Imekadiriwa kuwa takribani Wanigeria milioni nne wanatumia aina fulani ya opioid, kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya taifa hilo.

Kama sehemu ya uchunguzi, BBC pia ilituma mfanyakazi wa siri, aliyejifanya kama mfanyabiashara Mwafrika anayetaka kusambaza dawa nchini Nigeria, ndani ya moja ya viwanda vya Aveo nchini India, ambapo walimrekodi mmoja wa wakurugenzi wa Aveo, Vinod Sharma, akionesha bidhaa hatari na BBC iligundua kuuzwa kwake kote Afrika Magharibi.

Katika picha iliyorekodiwa kwa siri, mhudumu huyo anamwambia Sharma kwamba mpango wake ni kuuza tembe hizo kwa vijana nchini Nigeria "ambao wote wanapenda bidhaa hii".

Sharma akijibu "Sawa," kabla ya kueleza kwamba ikiwa watumiaji watachukua vidonge viwili au vitatu kwa wakati mmoja, wanaweza "kupumzika" na kukubaliana wanaweza kupata "juu".

Kufikia mwisho wa mazungumzo hayo, Sharma anasema: "Hii ni hatari sana kwa afya," na kuongeza kuwa "siku hizi, hii ni biashara".

Sharma na Aveo Pharmaceuticals hawakujibu ombi la maoni wakati uchunguzi wa awali wa BBC ulipochapishwa.

Mamlaka ya Chakula na Dawa ya India ilisema operesheni kali ilishuhudia hisa nzima ya Aveo ikikamatwa na uzalishaji zaidi kusimamishwa katika taarifa yake Ijumaa.

Hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni hiyo, iliongeza.

Shirika hilo lilisema "limejiandaa kikamilifu" kuchukua hatua dhidi ya yeyote anayejihusisha na "vitendo haramu vinavyoharibu sifa ya nchi".

FDA imeagizwa kufanya ukaguzi zaidi ili kuzuia usambazaji wa dawa hizo, ilisema.

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga