Uraibu wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na wanawake nchini Somalia

Baada ya kupatikana kwa mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 22 katika mitaa ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, mwaka jana ndio kulichangia kuliweka wazi tatizo la uraibu wa dawa za kulevya kwa wanawake katika mji huo. Wafanyakazi wa afya walisema alikufa kutokana na kuzidisha kwa dawa ya opioids.

Marafiki wa mshawishi huyo wa mitandao ya kijamii walisema amekuwa akijidunga dawa kwa muda mrefu. Walisema alikuwa amewelewa wakati alirekodi baadhi ya video zake maarufu za TikTok.

Polisi wameandikisha ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya mjini Mogadishu na kwingineko nchini Somalia, wakiwemo wanawake. Wanasema watu wanageukia aina mpya za dawa.

Ingawa walikuwa wakitafuna mirungi ya majani - ambayo si haramu - wanakunywa pombe, kunusa gundi au au kuvuta moshi wa hashishi, watu zaidi wanatumia vibaya opiods ambazo wanazidunga moja kwa moja kwenye mishipa yao. Hizi ni pamoja na morphine, tramadol, pethidine na codeine.

Mapema mwezi wa Desemba, polisi walikamata shehena kubwa ya dawa zilizoagizwa na daktari, hasa dawa za kulevya, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu ambapo pia waagizaji walikamatwa.

"Nilianza kulala kwenye gari"

Dawa nyingine maarufu inayotumiwa na wanawake vijana ni aina ya tumbaku ya kutafuna inayojulikana kama "tabbuu", ambayo inaweza kusababisha saratani ya mdomo na koo.

Amino Abdi, 23, amekuwa akitumia dawa za kulevya kwa miaka mitano iliyopita. Ingawa uraibu wa dawa za kulevya kwa wanawake ni jambo la mwiko nchini Somalia, ameamua kulizungumzia kwa uwazi na BBC kwa matumaini kwamba anaweza kusaidia kuvunja ukimya na kupunguza chuki.

"Nilianza kutafuna tabuu na wasichana nilioishi nao," anasema.

"Walikuwa na ushawishi mbaya kwangu. Nilipata uraibu wa tumbaku kisha nikahamia kwenye dawa kali zaidi, hasa zile ambazo ningeweza kuzidunga kwa njia ya mishipa, hasa tramadol na pethidine."

Bi Abdi anasema matumizi yake ya dawa za kulevya yaliongezeka baada ya kuanza kuwa na matatizo na mumewe. Sasa ametalikiwa na anaishi na binti yake mdogo.

"Mpenzi wangu wa zamani ndio sababu ya mimi kuwa mraibu wa dawa za kulevya. Uraibu wangu ulizidi kuwa mbaya hadi nikapoteza akili. Nilianza kulala kwenye magari na mitaani."

Bi Abdi anajaribu kuachana na dawa za kulevya lakini anasema ni vigumu sana kufanya hivyo kwa sababu hakuna vituo vya kurekebisha tabia nchini Somalia kukabiliana na tatizo hili..

Anasema haiwezekani kuacha dawa zote kwa wakati mmoja. Ameweza kupunguza tabia yake ya kujidunga opioid lakini bado anatafuna tumbaku na kuvuta shisha.

Wazazi, hasa akina mama, wana wasiwasi mwingi kuhusu tatizo la dawa za kulevya linaloongezeka miongoni mwa binti zao, ambao baadhi yao bado wako shuleni.

Khadijo Adan aliona binti yake mwenye umri wa miaka 14 alikuwa na tabia isiyo ya kawaida.

"Alikuwa akilala nyakati zisizotrajiwa na kuonyesha tabia za ajabu," anasema.

"Siku moja nilipata vidonge vya tramadol na tumbaku ya kutafuna kwenye begi lake. Nilimkabili na akaniambia ameanza kutumia dawa za kulevya kwa sababu ya shinikizo la rika."

Bi Adan alimtuma mtoto wake kuishi katika kituo kinachosimamiwa na mashekhe wa Kiislamu. Hatumii tena dawa za kulevya kwa sababu ni vigumu kwake kuzipata huko.

Wazazi wengi huwapeleka watoto wao “wanaowaletea shida” kwenye taasisi hizo, hasa wale wenye magonjwa ya akili, wanaojihusisha na uhalifu au dawa za kulevya na wale wanaoshukiwa kuwa mashoga.

Unyanyasaji mkubwa umefanyika katika baadhi ya vituo, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa minyororo na kupigwa kwa wafungwa.

Watoto wa mitaani wamo hatarini

Wakati inajitahidi kukabiliana na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 40 na zaidi ya miongo mitatu ya vita, rasilimali chache za Somalia haziwezi kukidhi mahitaji ya kimsingi ya binadamu, kando na kukabiliana na matatizo kama vile uraibu wa madawa ya kulevya.

Mashirika machache madogo yanajaribu kujaza pengo kwa kueneza ufahamu kuhusu hatari za dawa za kulevya.

Shirika la Green Crescent hutembelea shule na vyuo vikuu ili kuwaonya wanafunzi kuhusu aina tofauti za uraibu, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, kamari, michezo ya kubahatisha na mitandao ya kijamii.

Sirad Mohamed Nur anaendesha Wakfu wa Mama Ugaaso unaojikita katika utumiaji wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana wakiwemo wasichana.

"Tunafanya kila tuwezalo kuwazuia vijana kutumia dawa za kulevya kwa kufanya mipango ya uhamasishaji ambayo inaangazia hatari za kiafya zinazohusiana na utumiaji wa dawa za kulevya.

"Pia tunashawishi serikali kuingilia kati na kufanya kitu. Lakini hii haitoshi. Hatua kali zinahitajika ili kuzuia janga hili kuvuka mipaka, hasa miongoni mwa watoto wa mitaani."

Kulingana na Wizara ya Maendeleo ya Wanawake na Haki za Binadamu, zaidi ya 40% ya watoto wa mitaani hutumia dawa za kulevya.

Takriban thuluthi moja ya watoto wa mitaani nchini Somalia ni wasichana. Baadhi ya 10% wana umri wa chini ya miaka sita, wengine wakiwa na umri wa miaka mitatu.

Ingawa miraa, gundi na tumbaku ya kutafuna ni vitu vinavyotumiwa sana na watoto wa mitaani, utafiti uliofanywa na wizara uligundua kuwa karibu 10% wanatumia opioids na karibu 17% wanatumia tembe za usingizi.

Kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana waliotengwa kumesababisha ongezeko la uhalifu, ikiwa ni pamoja na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Kulingana na shirika la utafiti, Ajenda ya Umma ya Somali, pia imesababisha hali ya hivi karibuni ya magenge ya mitaani, yanayojulikana kama "Ciyal Weero", ambayo yamekuwa yakizua ugaidi kote Mogadishu.

Katika baadhi ya matukio, dawa za kulevya hutumika kuwadhuru wanawake kama vile katika mji wa kusini-magharibi wa Baidoa, ambapo mwanamke aliripotiwa kubakwa baada ya kupewa dawa ya afyuni.

Kuna hatari kwamba kuongezeka kwa matumizi ya dawa kwa njia ya mishipa kutabadilisha kiwango cha chini cha maambukizi ya VVU na Ukimwi nchini Somalia.

"Kuongezeka hivi karibuni wa watu wanaojidunga dawa za kulevya, hasa opioids, unaweka kundi jipya kabisa la Wasomali katika hatari ya kupata virusi," anasema Dk Sadia Abdisamad Abdulahi, meneja wa programu ya VVU katika wizara ya afya ya Somalia.

Kuyalenga maduka ya kuuza madawa

Wataalamu wa afya wanasema mojawapo ya njia mwafaka zaidi za kukabiliana na tatizo la opioid ni kuwalenga watu wanaouza dawa hizo, ambao wengi wao ni wenye maduka ya kuuza madawa.

Polisi wameanza kuwachukulia hatua kali.

Mmiliki mmoja ya duka la dawa ambaye hakutaka kutaja jina lake anasema yeye na wenzake hawajafurahishwa hata kidogo na hatua hiyo ya polisi.

"Nimeendesha duka la dawa huko Mogadishu kwa miaka mingi. Ilikuwa rahisi sana kuuza dawa kwa vijana, ikiwa ni pamoja na wasichana, kwa kiasi fulani kwa sababu hakuna mtu aliyejua ni aina gani ya athari za dawa hizo," alisema.

"Tulikuwa tukiuza kwa kila mtu na tulipata pesa nzuri.

"Lakini wazazi sasa wanashirikiana na polisi ambao wameanza kufuatilia na wakati mwingine wanatukamata. Sasa tunaogopa kuwauzia vijana dawa za kulevya na matokeo yake tunapoteza."

Kwa kuzungumzia matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake, wanawake vijana jasiri kama Amino Abdi na akina mama kama Khadijo Adan wamechukua hatua muhimu ya kwanza ya kuweka suala hilo hadharani.

Uingiliaji kati wa polisi na mipango ya uhamasishaji wa madawa ya kulevya pia itasaidia, lakini bila rasilimali zaidi na tahadhari, haiwezekani kuwa tatizo hili litaondoka hivi karibuni.