Mambo sita ambayo Trump anapaswa kuyajua kuhusu Liberia

fv

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump aliwaalika viongozi wa Afrika kutoka Gabon, Guinea-Bissau, Liberia, Mauritania na Senegal katika Ikulu ya White House huko Washington
    • Author, Moses Kollie Garzeawu & Wycliffe Muia
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Donald Trump amempongeza Rais wa Liberia, Joseph Boakai kwa kuzungumza “Kiingereza kizuri” na kumuuliza shule alisoma wapi.

Kitu ambacho Trump hakijui ni kwamba Liberia ina uhusiano wa kipekee na wa muda mrefu na Marekani.

Kiingereza ndiyo lugha rasmi ya nchi hiyo na wengi huzungumza kwa lafudhi ya Kimarekani kwa sababu ya uhusiano huo.

Huenda ni lafudhi hii ndio ambayo imemvutia Trump.

Pia unaweza kusoma

Watumwa walioachwa huru

dx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Liberia ina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria na Marekani na marais kadhaa wa Marekani, akiwemo George W Bush, wameitembelea nchi hiyo.

Liberia ilianzishwa na watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika walioachiliwa huru mwaka 1822 kabla ya kujitangazia uhuru 1847.

Maelfu ya Wamarekani weusi na Waafrika waliokombolewa – na kuokolewa kutoka kwenye meli za watumwa zilizopita Atlantiki - walikaa Liberia wakati wa ukoloni.

Rais wa zamani wa Marekani Abraham Lincoln alitangaza rasmi uhuru wa Liberia mwaka 1862, lakini nchi hiyo ilikuwa na urathi mwingi wa Marekani na ilibakia chini ya “ushawishi" wa Marekani wakati wa ukoloni.

Kutokana na ushirikiano huu, utamaduni na taasisi za Liberia zina uhusiano mkubwa na Wamarekani wenye asili ya Afrika. Marais kumi kati ya 26 wa Liberia walizaliwa Marekani.

Vizazi vya watumwa hawa walioachiliwa huru, waliojulikana kama Americo-Liberians, waliitawala nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 100.

Hilo liliwachukiza baadhi ya Waliberia wazawa na rais wa mwisho kutoka jumuiya hiyo, William Tolbert, alipinduliwa na kuuawa katika mapinduzi mwaka 1980.

Wazawa ni takriban robo ya wakazi, kulingana na tovuti ya Britannica, ambayo inasema kuna lugha dazeni mbili zinazozungumzwa nchini humo.

Rais Boakai anatoka katika kabila la Kissi na hiyo ndio lugha yake ya mama, kabla ya kujifunza Kiingereza shuleni.

Jina la Mji mkuu

ed

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Baadhi ya mitaa huko Monrovia imepewa majina ya wakoloni wa Kimarekani

Mji mkuu wa Liberia, Monrovia, ulipewa jina hilo kwa heshima ya Rais wa tano wa Marekani, James Monroe, ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa Jumuiya ya Kikoloni ya Marekani (ACS).

ACS lilikuwa shiŕika lenye jukumu la kuwatafutia makazi Wamrekani walioachiliwa huru huko Afrika Magharibi, na shirika hilo lilichangia pakubwa kuanzishwa kwa Liberia.

Haishangazi usanifu wa awali wa jiji uliathiriwa sana na majengo ya mtindo wa Marekani.

Barabara nyingi huko Monrovia zimepewa majina ya wakoloni wa Kimarekani, ikionyesha uhusiano wa kihistoria wa jiji hilo na Marekani.

Hospitali kuu ya jiji hilo inaitwa John F Kennedy Medical Center (JFKMC), jina la rais wa zamani wa Marekani.

Bendera zinazoshabihiana

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna mfanano wa kushangaza kati ya bendera za nchi hizo mbili

Bendera ya Liberia inafanana kwa kiasi kikubwa na bendera ya Marekani. Ina mistari 11 mekundu na meupe na mraba wa bluu wenye nyota moja nyeupe.

Nyota nyeupe inaashiria Liberia kama jamhuri ya kwanza huru barani Afrika.

Bendera ya Marekani ina mistari 13 meupe na mekundu, inayowakilisha makoloni 13 ya awali na nyota 50, kwa kila jimbo.

Bendera ya Liberia ilibuniwa na wanawake saba weusi - wote walizaliwa Marekani.

Mtoto wa rais wa zamani

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Timothy Weah, anayeonekana hapa akipeana mkono na Rais Donald Trump mwezi uliopita, anaichezea Juventus nchini Italia

Timothy Weah, mtoto wa Rais wa zamani wa Liberia George Weah, ni mchezaji wa kulipwa wa Marekani anayechezea klabu ya Juventus ya Italia na pia timu ya taifa ya Marekani.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 25 alizaliwa Marekani lakini alianza soka la kulipwa katika klabu ya Paris St-Germain ya Ufaransa, ambapo alishinda taji la Ligue 1 kabla ya kuhamia kwa mkopo katika timu ya Scotland, Celtic.

Baba yake, George, ni gwiji wa soka wa Liberia ambaye alishinda Ballon d'Or mwaka 1995 alipokuwa akiichezea klabu ya Juventus ya Italia, AC Milan. Yeye ndiye Mwafrika pekee mshindi wa tuzo hii - na alichaguliwa kuwa rais mwaka 2018.

Tuzo ya Amani ya Nobel

d

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ellen Johnson Sirleaf aliwahi kuwa rais wa 24 wa Liberia kutoka 2006 hadi 2018.

Liberia ilitoa rais wa kwanza wa kuchaguliwa mwanamke barani Afrika, Ellen Johnson Sirleaf.

Alichaguliwa 2005, miaka miwili baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya umwagaji damu kumalizika, na alihudumu kama rais hadi 2018.

Johnson Sirleaf ana aliishi Marekani kwani alisoma katika Chuo cha Biashara cha Madison na baadaye akaenda Chuo Kikuu cha Harvard ambako alihitimu kama mchumi.

Amepata kutambuliwa duniani kote na kupongezwa kwa kudumisha amani wakati wa utawala wake.

Mwaka 2011, pamoja na Leymah Gbowee na Tawakkul Karmān, alishinda Tuzo ya Nobel ya Amani kwa juhudi zake za kuendeleza haki za wanawake.

2016, Forbes ilimuorodhesha kati ya wanawake wenye nguvu zaidi ulimwenguni.

Shamba kubwa la mpira

k
Maelezo ya picha, Mpira hupatikana kwa kukata gome la mti na kisha kukinga utonvu unapodondoka
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shamba kubwa zaidi la mpira duniani, ambalo lina ukubwa wa maili za mraba 185, (kilomita za mraba 479), linamilikiwa na Firestone Liberia, kampuni tanzu ya kampuni ya kutengeneza matairi ya Marekani.

Lilianzishwa 1926 ili kuipa Marekani bidhaa ya mpira wakati bidhaa hiyo ikidhibitiwa na Uingereza.

Firestone ni moja ya kampuni binafsi inayotoa ajira nyingi zaidi Libeŕia, ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 4,000.

Kampuni hiyo imekuwa ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Mwaka 2006, ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu viwanda vya mpira nchini Libeŕia ilisema: "Wafanyakazi wa mashamba wanakabiliana na hali ya hatari ya kufanya kazi bila mafunzo ya kutosha au vifaa vya usalama.

"Wafanyakazi wengi... hawapati mishahara mizuri au malipo sawa, na hawana haki ya kugoma. Ajira za kuwaajiri watoto hufanyika mara kwa mara kwenye mashamba," ilisema.

Firestone imekuwa ikikanusha madai hayo, na mwaka 2011 haikupatikana na hatia ya kuajiri watoto na mahakama ya Marekani.

Mpira unasalia kuwa mojawapo ya mauzo makubwa ya nje ya Liberia na Marekani ndio soko lake kubwa zaidi.

Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu Henrietta Peters Magbollah, anasema mshangao wa rais wa Marekani kwa ufasaha wa Boakai katika kuzungumza Kiengereza, unaonyesha tatizo pana kuhusu ujinga wa kimataifa kuhusu mataifa ya Afrika na watu wake.

"Raia wengi wa mataifa mengine nje ya Afrika hawajui mengi kuhusu nchi za Afrika," anasema. "Akili zao zimegubikwa na masimulizi ya vita, umaskini na ukosefu wa elimu."