Ziara ya kifalme DRC: Mfalme Phillipe arejesha mali zilizoporwa enzi za ukoloni

DRC

Chanzo cha picha, AFP

Mfalme Philippe amekabidhi kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mali ya kwanza kati ya vitu 84,000 vilizoporwa wakati wa ukoloni ambavyo Ubelgiji imekubali kurejea. Ni barakoa, iitwayo Kakungu, ambayo ilionyeshwa hapo awali katika Jumba la Makumbusho la Kifalme la Ubelgiji la Afrika ya Kati.

Mfalme Philippe na Malkia Mathilde wako katika ziara nchini DR Congo kwa mwaliko wa Rais Félix Tshisekedi. Inaelezwa rekodi ya ukoloni wa Ubelgiji nchini DR Congo ilikuwa moja ya rekodi katili zaidi barani Afrika. Kinyago kipya kilichorejeshwa kilitumiwa wakati wa sherehe za uponyaji na jamii ya Suku, kutoka kusini-magharibi mwa nchi.

Belgium

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kinyago hiki awali kiliweka huko Brussels Ubelgiji

Mali na vitu vingi vya sanaa vinarejeshwa kutoka Makumbusho ya Kifalme ya Afrika ya Kati, ambapo karibu 70% ya vitu vyake vya sanaa viliporwa wakati wa ukoloni.

Baada ya makabidhiano hayo makubaliano yalitiwa saini kufungua ushirikiano wa kitamaduni kati ya Makumbusho ya Kitaifa ya DR Congo na Jumba la Makumbusho la Kifalme la Afrika ya Kati, lakini maelezo hayo hayajawekwa wazi.

Shangazi wa Mfalme Philippe, Princess Esmerelda aliambia BBC kuwa ni jambo sahihi kurejesha vitu vilivyoporwa.

"Wakoloni wa zamani wa Ulaya wanapaswa kusahau ya zamani," aliambia kipindi cha BBC World Tonight.

"Ninaamini sana kwamba vitu vya kale vilivyoibiwa kutoka nchi nyingi sana barani Afrika na kwingineko vinapaswa kurejea vilikotoka."

Mamilioni ya Wakongo waliteswa na vitendo vya ukatili chini ya ukoloni, haswa wakati wa utawala wa Mfalme Leopold II, ambaye alimiliki Jimbo Huru la Kongo kama mali yake binafsi.

Belgium

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfalme Leopold II alitawala Ugelgiji kati ya mwaka 1865-1909

Mnamo 2020, Mfalme Phillipe alimwandikia Rais Tshisekedi katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa nchi hiyo akielezea "majuto yake makubwa" kwa unyanyasaji wa kikoloni uliofanywa chini ya mababu zake.

Lakini Princess Esmerelda alisema hatua zaidi inahitajika: "Ninahisi kwamba labda msamaha unapaswa kuja hivi karibuni, msamaha rasmi kwa siku za nyuma na kwa ukatili wa kikoloni ambao ulifanywa".

Kwa nini utawala wa kikoloni wa Ubelgiji unatajwa kuwa wa kikatili sana?

Ubelgiji ilitawala nchi hiyo ya Afrika ya kati kuanzia Karne ya 19 hadi ilipopata uhuru wake mwaka 1960.Zaidi ya Waafrika milioni 10 wanadhaniwa walikufa wakati wa utawala wa Mfalme Leopold wa Pili kutokana na magonjwa, unyanyasaji wa wakoloni, na walipokuwa wakimfanyia kazi mashambani.

Wenye mamlaka wangekata miguu na mikono ya watu waliokuwa watumwa wakati hawakufikia kiwango cha kufaa kutumika.

Ziara ya juma moja ya Mfalme Phillipe, ambayo ni ya kwanza tangu kutwaa kiti cha ufalme mwaka wa 2013, imepata mapokezi tofauti kutoka kwa watu ambao BBC ilizungumza nao mjini Kinshasa."Nimefurahishwa sana na ziara hii, kwa sababu nchi imekuwa ikienda vibaya tangu Wabelgiji kuondoka," mtu mmoja alisema.

Wakati mwingine alikuwa na shauku kidogo: "Rais anaamua kumwalika mfalme wa Ubelgiji, kufanya nini, kutupora tena?"

Kama sehemu ya safari, Mfalme Phillipe pia alikutana na Koplo Albert Kunyuku, mkongwe wa mwisho wa Vita vya Kidunia vya pili vya Kongo ambaye alipigana pamoja na Wabelgiji. Katika ukumbusho wa wapiganaji wa zamani, shada la maua liliwekwa, na Mfalme Phillipe akamkabidhi Koplo Kunyuku medali.

Corporal Albert Kunyuku was honoured at an elaborate ceremony

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kopolo Albert Kunyuku alitunukiwa medali maalumu na mfalme Phillipe