George Weah: Kitabu cha wasifu wa Rais wa Liberia chazua utata, mmoja wa wandishi wake akamatwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Makundi ya wanawake nchini Liberia yameghadhabishwa na sehemu ya chapisho katika kitabu cha wasifu wa Rais wa nchi hiyo George Weah.
Wanawake hao wamekasirishwa na sura ambapo rais amenukuliwa akifichua mambo machafu na ya kudhalilisha kuhusu tabia za ngono za mke wake.
Hayo yanajiri huku ripoti zikiashiria kuwa mwandishi mwenza wa kitabu cha wasifu wa Rais wa Liberia George Weah amezuiliwa kuondoka nchini huku kukiwa na utata kuhusu sehemu za kitabu hicho.
Rais alielezea kwa kina katika kitabu hicho sababu iliyomfanya kuchagua kumuoa mke wake badala ya wanawake wengine, ikiwa ni pamoja na uwezo wake chumbani.
Mama taifa Clar Marie Weah, hajatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo tata.
Tukio la hivi punde linakuja baada ya sehemu za kitabu hicho kusambazwa mtandaoni na mtangazaji wa kipindi cha mazungumzo cha Liberia mwenye makazi yake nchini Marekani Henry Costa.
Isaac Vah Tukpah alilazimika kuacha kazi yake - kama msaidizi wa mwanasiasa wa upinzani - na kuomba msamaha kwa kujumuisha mahojiano kuhusu mke wa rais.
Serikali imepinga madai ya upinzani kwamba mwandishi wa kitabu hicho alikamatwa kwa kuchapisha sehemu hiyo ya mahojiano iliyozua utata.
Katika taarifa wizara ya mawasiliano ilisema alizuiliwa kutoka nchini siku ya Jumanne usiku kwa kuhofia usalama wake na mpaka pia ulikuwa umefungwa.
Rais Weah katika taarifa alisema kuwa hakuna "anayemtafuta" Bw. Tukpah na kwamba yuko "huru kusafiri nje ya Liberia".
Makundi ya wanawake yaliyoghadhabika yamesema yanapanga maandamano ya kupinga kitabu hicho.
Lakini watu wengi wanataka rais wa Liberia awe wazi na akubali kama waandishi walidanganya au la kuhusu alichowaambia kwenye wasifu.
Pia unaweza kutazama:
Fahamu jinsi mshindi huyo wa kombe la klabu bingwa Ulaya alivyoibuka na kuwa rais wa Liberia













