Mapacha walioibuka na lugha yao wenyewe

dfv

Chanzo cha picha, Matthew and Michael Youlden/ Superpolyglotbros

Maelezo ya picha, Matthew na Michael Youlden
    • Author, Ahmed Nour na Erwan Rivault
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mapacha Matthew na Michael Youlden kila mmoja anazungumza lugha 25, na ya 26 ni Umeri, hawaijumuishi katika hesabu yao.

Ikiwa hujawahi kusikia kuhusu Umeri, kuna sababu ya hilo. Mathew na Michael ndio watu wawili pekee wanaozungumza lugha hiyo, kusoma na kuandika, baada ya kuiunda wenyewe wakiwa watoto.

Ndugu hao wanasisitiza kuwa Umeri si lugha ya siri.

"Kwa hakika ina thamani kubwa sana kwetu, kwani inaonyesha uhusiano mkubwa tulionao kama mapacha wanaofanana,” wanaeleza katika barua pepe.

Inakadiriwa kuwa 30-50% ya mapacha huibuka na lugha ya mawasiliano au muundo fulani wa mawasiliano wanaouelewa wao tu.

Roy Johannink, kutoka Uholanzi, ni baba wa mapacha wawili, Merle na Stijn. Miaka kumi na tatu iliyopita, walipokuwa watoto, alirekodi mazungumzo yao na kuyaweka kwenye YouTube. Kufikia sasa, mazungumzo hayo yametazamwa zaidi ya mara milioni 30.

Nancy Segal, Mkurugenzi wa masomo ya mapacha katika Chuo Kikuu cha California anasema, kama ilivyo kwa Merle na Stijn (ambao wameipoteza lugha yao walipojifunza Kiholanzi), mapacha wengi pia hupoteza lugha zao kadiri wanavyokuwa na kusikia lugha nyingine nyumbani.”

Lakini kwa mapacha wa Youlden, haikuwa hivyo. Hawajapoteza lugha yao. Kinyume chake, wameiboresha na kuikamilisha kwa miaka mingi.

Pia unaweza kusoma

Kuibuka kwa Umeri

fd

Chanzo cha picha, Matthew and Michael Youlden/ Superpolyglotbros

Maelezo ya picha, Mapacha Matthew na Michael Youlden walikuza lugha yao wenyewe wakiwa watoto, ambayo bado wanazungumza hadi leo.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Walizaliwa na kukulia Manchester nchini Uingereza, mapacha hao wa Youlden walizungukwa na jamii na tamaduni tofauti, na hilo likawafanya wapende lugha.

Kumbukumbu za maisha ya utotoni kuhusu lugha ya Umeri hazieleweki, lakini wanakumbuka babu yao alichanganyikiwa, wawili hao walipomwambia mzaha ambao hakuelewa, wakati huo wakiwa wanafunzi wa shule ya awali.

Wakiwa na umri wa miaka minane, wakaenda likizo ya na familia nje ya nchi. Walikwenda Uhispania na kuamua kujifunza Kihispania, wakiamini wasipofanya hivyo, watapata shida kuagiza malai.

Wakiwa na kamusi na bila kujua sarufi nyingi, wakaanza kutafsiri sentensi kutoka Kiingereza hadi Kihispania neno kwa neno. Baadaye, wakajifunza Kiitaliano, kisha wakageukia lugha za Skandinavia.

Kwa kuleta pamoja vipengele tofauti vya kisarufi vya lugha zote walizosoma, ndugu hao waligundua kwamba Umeri inaweza kuwa lugha yake yenyewe.

Youlden walianza kusanifisha na kuiboresha lugha ya Umeri. Hata walijaribu kuunda alfabeti zao wenyewe, lakini waligundua (walipopata kompyuta yao ya kwanza), hilo halitakuwa na manufaa kwao kwa vile hakuna alfabeti za Umeri. Umeri sasa inaandikwa kwa kutumia alfabeti za Kilatini.

Changamoto ya lugha hizi

gfcv

Chanzo cha picha, Mike Simons/Getty Images)

Maelezo ya picha, Mapacha wanaofanana daima wameamsha udadisi.

Kuhifadhi lugha inayozungumzwa na watu wachache kuna changamoto zake. Yeyote anayezungumza lugha ya watu wachache, isiyozungumzwa na sehemu kubwa ya jamii - anaweza kusita kuitumia.

Karen Thorpe ni mtaalamu wa maendeleo ya malezi ya watoto, elimu na utafiti katika Taasisi ya Queensland katika Chuo Kikuu cha Queensland, anasema:

“Badala ya kufikiria jambo hilo kuwa jambo la ajabu na lisilo la kawaida, lugha ngeni ni jambo zuri ambalo hutokea kwa wanadamu wanapokuwa karibu.”

Pia anachukulia hili kuwa jambo la kawaida la ukuaji. Kama alivyoeleza katika makala ya utafiti ya 2010: "Watoto wadogo wanaoanza kuzungumza huwa wanajielewa vizuri zaidi kuliko wazazi wao au watu wazima wengine."

Kwa Youlden, lugha hizi ni mchanganyiko wa ukaribu na udadisi wa kiakili, ingawa Thorpe anasema ukuzaji huu wa lugha binafsi kwa muda mrefu ni nadra sana.

Juni na Jennifer Gibbons ni mfano wa changamoto hizo. Mapacha hao kutoka Barbados walikulia Wales katika miaka ya 1970, wanasema walikabiliwa na tatizo la kunyanyaswa shuleni kutokana na lugha yao. Kwa sababu hiyo, waliacha kuzungumza na wengine na kuzungumza wao kwa wao tu.

Wakiwa na umri wa miaka 19, baada ya kukamatwa kwa makosa ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kuchoma moto na wizi, walipelekwa katika hospitali ya Broadmoor, yenye ulinzi mkali ya magonjwa ya akili nchini Uingereza kwa sababu ya lugha yao.

Lugha inakuwa

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Inakadiriwa kuwa 40% ya mapacha wachanga hutumia aina fulani ya "lugha pacha"

Kwa mapacha wa Youlden, kuunda Umeri ni jambo muhimu na uzoefu mzuri. Lugha inazidi kubadilika, na wao hufikiria maneno mapya ambayo yameibuka katika maisha ya kisasa. "Iwe ni kebo ya iPad au ya Umeme, maneno hayo yote hayakuwepo miaka 20 au 30 iliyopita," anasema Matthew.

Sasa wanaendesha biashara yao ya kufundisha lugha kwa watu binafsi, taasisi za elimu na makampuni binafsi. Michael anaishi Gran Canaria na Matthew, Basque. Wanapozungumza wao kwa wao hadi leo hutumia lugha ya Umeri.

Hawakusudii kuifundisha lugha hiyo kwa watoto wao wa baadaye, na wanaona ni jambo la ajabu kuisomesha lugha hiyo kwa mtu mwingine.

“Ni lugha moja inayozungumzwa na watu wawili,” Michael anaeleza. "Ni moja ya lugha ambayo, kwa bahati mbaya, itakuwa na tarehe yake ya kumaliza muda wake.”

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah