Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kipchoge: Atapambana na joto na vilima ili kuweka historia katika Olimpiki
- Author, Celestine Karoney
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Author, Rob Stevens
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Eliud Kipchoge, Mkenya anayetaka kuweka jina lake katika vitabu vya historia ya michezo ya kukimbia kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris.
Tarehe 10 Agosti mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 39, atatafuta nafasi ya kuwa mtu wa kwanza kushinda mara matatu mfululizo katika mbio za marathoni katika michezo ya Olimpiki.
Atapambana na wakimbiaji wachanga, lakini pia atakuwa na changamoto nyingine ya kupambana na hali ya hewa. Joto katika mji mkuu wa Ufaransa ni kali, na huongezeka hadi nyuzi joto 30.
"Mashindano yatakuwa magumu sana - karibu 40% ni milima - na nadhani joto litachangia ugumu," aliiambia BBC Sport Africa.
"Hata saa mbili, tatu, nne asubuhi, nadhani joto litapanda hadi digirii 30. Ni vigumu kukimbia marathoni kamili katika digrii 30.
Kutoka mwinuko wa kuanzia wa mita 36 kutoka usawa wa bahari katikati mwa jiji, njia hiyo itapanda hadi mita 183 kwenye barabara ya Versailles, kuelekea mwinuko wa pili mkali wa mita 172 kabla ya kuifikia alama ya kilomita 30 wakati wakimbiaji wanaporejea Paris. .
Mashindano yataanza saa 02:00 asubuhi kwa saa za Ufaransa, na Kipchoge amebadilisha mfumo wake wa mazoezi katika kituo chake cha Kaptagat katika jitihada za kuongeza medali nyingine ya dhahabu, mbali na zile za Rio, Brazil 2016 na Tokyo, Japan 2020.
"Nitaweka akilini mwangu kuhusu ukimbiaji wa milimani na katika joto kali ili kuufanya mwili wangu umudu kuelekea mashindano ya Paris," alielezea katika mahojiano wakati wa maandalizi yake.
"Wakati mwingine hufanya mazoezi saa nne asubuhi, tano ili kuhisi joto hilo. Lakini katika Olimpiki hatuzingatii muda."
Anapambana kuweka historia
Kipchoge alipovuka mstari wa kumaliza huko Sapporo, Japan, miaka mitatu iliyopita alilingana na mafanikio ya mabingwa mfululizo wa Olimpiki ya marathoni, Abebe Bikila (1960 na 1964) na Waldemar Cierpinski (1976 na 1980).
Mkenya huyo hashikilii tena rekodi ya dunia ya zaidi ya maili 26.2 (kilomita 42.195), rikodi yake ilivunjwa na marehemu Kelvin Kiptum, mwezi Oktoba mwaka jana, lakini anapambana kuweka historia huku akitarajia kuwapita wanaume kutoka Ethiopia na Ujerumani Mashariki.
"Nataka kuingia katika vitabu vya historia, kuwa binadamu wa kwanza kushinda mara tatu mfululizo," alisema.
Mwezi Aprili, Kipchoge alisema matarajio yake ni kushinda mjini Paris licha ya kumaliza katika nafasi ya 10 kwenye mbio za Tokyo Marathon za Machi - nafasi yake ya chini kabisa kuwahi kutokea.
“Ikiwa nitapoteza marathoni hii, nitaumia. Lakini nitarudi na kuanza safari tena.”
Kumbukumbu za Paris
Kipchoge atakimbia katika jiji ambalo mbio zake za kuwa mkimbiaji wa kimataifa zilianza, baada ya kushinda dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwenye Mashindano ya Dunia ya 2003, akiwa na umri wa miaka 18 tu.
"Michezo hii ya Olimpiki ni maalumu kwangu, inafanyika Paris ambapo nilianza maisha yangu katika michezo," anasema.
"Ulikuwa mwanzo wa mimi kwenda kwenye uwanja wa kimataifa kukimbia, kuwa kwenye mstari wa kuanzia na watu wenye uzoefu na kutambulika. Nilifurahi sana. Iliathiri maisha yangu kwa njia chanya.”
Kipchoge anatazamiwa kupangwa pamoja na nguli wa Ethiopia, Kenenisa Bekele, mwanaume aliyemzidi umri kwa miaka miwili ambaye alimaliza wa tatu katika fainali hiyo jijini Paris miaka 21 iliyopita.
Mkenya huyo anasema "kuwa na nidhamu, msimamo na kuheshimu michezo" yamekuwa mambo muhimu kwa maisha yake ya muda mrefu michezoni.
Kipi kifuatacho kwa Kipchoge?
Kipchoge hataki kuthibitisha ikiwa atastaafu baada ya michezo hiyo, lengo lake ni kuhamasisha watu wengi zaidi kuanza kukimbia.
"Ikiwa utaniambia ulimwengu umekuwa ulimwengu wa kukimbia, nitastaafu," alisema.
"Nataka familia zote zifanye kukimbia kuwa ni mtindo wa maisha; kuamka asubuhi, kuvaa viatu, kutoka nje na kukimbia na kurudi. Hilo ndilo ninalohitaji.
Nyota huyo wa Afrika Mashariki amekiri huenda Paris ikawa mashindano yake ya mwisho kwenye michezo hiyo.
"Nadhani nitakuwa kwenye benchi nikitazama watu, ikiwa kila kitu kitaenda sawa, huko Los Angeles [mwaka 2028]," alisema.
“Kukimbia Olimpiki ya mwisho haimaanishi kuwa nitaacha kukimbia. Napenda michezo.”
Mbio za marathoni za Paris 2024 zitafikia mwisho huko Esplanade des Invalides, mbele ya eneo la mapumziko la Napoleon.
Jina la mfalme wa zamani wa Ufaransa, imepita zaidi ya miaka 200 tangu kifo chake,
"Naamini nitakuwa mtu mwenye furaha moyoni nitakaposhinda medali ya dhahabu. Hilo linamaanisha kuwa historia itaandikwa."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla