Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Simuamini mtu yeyote' - Jinsi unyanyasaji mitandaoni ulivyomuumiza Kipchoge
- Author, Celestine Karoney
- Nafasi, BBC Michezo Afrika, Eldoret
Mshindi mara mbili wa mbio za marathon katika mashindano ya Olimpiki Eliud Kipchoge anasema alihofia maisha ya familia yake wakati wa kampeni ya unyanyasaji mtandaoni dhidi yake ambayo ilimhusisha kimakosa na kifo cha mwanariadha mwenzake wa Kenya wa mbio za marathon Kelvin Kiptum.
Kiptum, mshikilizi wa rekodi ya dunia ambaye alionekana kumaliza ushindi wa Kipchoge zaidi ya maili 26.2, alifariki katika ajali ya barabarani mnamo Februari akiwa na umri wa miaka 24.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walianza kukisia kwamba Kipchoge alikuwa sehemu ya njama ya kumuua Kiptum, ambaye alikuwa amepunguza kiwango bora cha dunia hadi saa mbili, sekunde 35 Oktoba iliyopita huko Chicago.
"Nilishtuka kwamba watu [kwenye] mitandao ya kijamii wanasema 'Eliud anahusika katika kifo cha kijana huyu'," mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 39 aliiambia BBC Michezo Afrika.
"Hiyo ilikuwa taarifa mbaya zaidi kunihusu maishani mwangu.
"Niliambiwa mambo mengi mabaya; kwamba watachoma kambi ya (mazoezi), watachoma mali yangu mjini, watachoma nyumba yang, watachoma familia yangu.
"Haikufanyika lakini hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo."
Maoni ya awali ya Kipchoge alipoona uvumi wa uwongo ukisambaa mitandaoni jambo ala kwanza alilofanya ni kuangalia ikiwa familia yake ilikuwa salama.
"Sina uwezo wa kwenda kwa polisi na kuwaambia maisha yangu yako hatarini. Kwa hiyo wasiwasi wangu ulikuwa ni kuiambia familia yangu kuwa makini zaidi na waangalifu," alisema.
"Nilianza kuwapigia simu watu wengi.
"Niliogopa sana watoto wangu kwenda shule na kurudi.
"Wakati mwingine wanaendesha baiskeli, lakini tulilazimika kuwazuia kwa sababu huwezi kujua nini kitatokea. Tulianza kuwaacha na kuwachukua jioni.
"Msichana wangu alikuwa katika shule ya bweni - hiyo ilikuwa ahueni kwamba hakuwa na ufikiaji wa mitandao ya kijamii, lakini ni ngumu kwa wavulana wangu kusikia 'Baba yako ameua mtu'."
Kupoteza marafiki na uaminifu
Kipchoge alitekwa na hisia wakati wa mahojiano nyumbani kwake mjini Eldoret alipokuwa akielezea jinsi unyanyasaji mtandaoni ulivyomuathiri mama yake mzazi.
"Wakati wangu mbaya zaidi ulikuwa (wakati) nilipojaribu kumpigia simu mama yangu," alisema.
"Aliniambia 'Jihadhari' na 'Mengi yamekuwa yakiendelea'.
"Kwetu nyumbani ni vijijini. Na kwa umri wa mama yangu, niligundua kuwa mitandao ya kijamii umefika kila mahali.
"Lakini alinipa ujasiri. Ulikuwa mwezi mgumu sana."
Hata hivyo, Kipchoge, ambaye alikua mtu wa tatu kushinda mbio za Olimpiki mfululizo alipotetea taji lake mjini Tokyo mwaka wa 2021, aliamua kutochukua tahadhari kuhusu usalama wake.
“Sikuona haja ya kubadili sehemu za kufanyia mazoezi kwa sababu maisha yangu yako wazi,” alieleza.
"Mchezo wetu hatufanyi mazoezi katika ukumbi wa kufanyia mazoezi, ni kwenda nje kukimbia. Ninatembea mitaani kwa uhuru."
Kipchoge anadai "alipoteza takriban 90%" ya marafiki zake huku kukiwa na kiungo kisicho sahihi cha ajali ya Kiptum na unyanyasaji mtandaoni.
"Ilikuwa uchungu sana kwangu kujifunza hata kutoka kwa watu wangu, wale tunaofanya mafunzo pamoja, wale ambao nina mawasiliano nao, na maneno mabaya yanatoka kwao," aliongeza.
"Nilisikitika sana kuona hivyo."
Athari kwenye utendaji wake
Timu ya Kipchoge iliamua kumtenganisha na mitandao ya kijamii kufuatia dhuluma hiyo, lakini alisema hakuwahi kufikiria kufuta akaunti zake.
“Nikifuta akaunti zangu basi inaonyesha kuna kitu naficha,” alisema.
"Nitasalia na akaunti zangu. Sikufanya lolote."
Hata hivyo, anaamini matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yaliathiri utendaji wake katika mashindano.
Kipchoge aliibuka wa 10 katika mbio za Tokyo Marathon tarehe 3 Machi, matokeo ya chini zaidi tangu aanze mchezo wa riadha mwaka wa 2013, akivuka mstari kwa dakika mbili na nusu nyuma ya mshindi Benson Kipruto.
"Nilipokuwa Tokyo sikulala kwa siku tatu," alifichua.
"Ilikuwa matokeo yangu mabaya zaidi kuwahi kutokea."
Licha ya kushindwa huko aliteuliwa katika timu ya Kenya ya mbio za marathon kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 wiki iliyopita, na sasa anaangazia kuandikisha historia zaidi katika Michezo hiyo huku akilenga kushinda medali ya tatu mfululizo ya dhahabu.
"Inamaanisha kujizoazoa kuamka na kwenda moja kwa moja tena, kwa lengo lako," aliongeza Kipchoge, ambaye mwaka wa 2019 alikuwa mtu wa kwanza kukimbia mbio za marathon chini ya saa mbili, ingawa katika hali zilizodhibitiwa mjini Vienna.
"Nataka kuingia katika vitabu vya historia, kuwa binadamu wa kwanza kushinda-mataji mtawalio."
Kukabiliana na unyanyasaji Paris 2024
Baada ya kukabiliwa na vitisho na unyanyasaji mitandaoni, Kipchoge anaamini kuwa kampuni za mitandao ya kijamii "hazijachukua hatua" kuzuia unyanyasaji kwenye majukwaa yao.
“Hawa watu wasio na uso wanachapisha mambo mabaya na ni hatari sana,” alisema.
“Ukiripoti baadhi ya akaunti zinachukua muda kuzifungia akaunti hizo.
"Wanapaswa kuchukua hatua haraka, kupata ukweli, kufuta akaunti. Watu [wanapaswa] kujua kwamba ikiwa unasema kitu ambacho si kizuri basi akaunti yako itafungiwa."
Hata hivyo, Kipchoge amekaribisha tangazo kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), kwamba inapanga "kuchukua hatua kikamilifu" ili kuwalinda wanariadha dhidi ya unyanyasaji mtandaoni wakati wa Paris 2024.
IOC inakusudia kutumia akili bandia kusaidia kutambua machapisho yenye matusi na kuyaripoti kwa makampuni ya mitandao ya kijamii.
"Nadhani ni mwelekeo sahihi," alisema.
"Sasa wanapiga muhuri mamlaka yao na kazi yao kama shirika linaloshughulikia wanariadha ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji."
Lakini, kwa Kipchoge, tayari wamechelewa sana kuepusha majeraha ya kihisia ambayo amekumbana nayo.
"Nilijifunza kwamba urafiki hauwezi kudumu milele," alisema.
"Nadhani ni bahati mbaya kwamba ilitokea wakati ninasherehekea zaidi ya miaka 20 katika mchezo wa riadha.
"Kilichotokea kimenifanya nisimuamini mtu yeyote. Hata kivuli changu mwenyewe, sitakiamini."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi