Eliud Kipchoge: Hayakuwa mashindano bali nilikuwa natuma ujumbe

Bingwa wa Olimpiki mbio za marathon Eliud Kipchoge Ijumaa wiki hii ametangazwa mwanamichezo bora katika hafla ya kufana iliyofanyika katika uwanja wa Mombasa Sports Club.

Kipchoge pia alichaguliwa kuwa mwanamichezo bora wa kitengo cha wanaume naye bingwa wa dunia, Hellen Obiri akatwaa tuzo la wanawake.

Baadhi ya wanamichezo ambao Obiri aliwabwaga ni Brigid Kosgei ambaye anashikilia rekodi ya dunia na bingwa wa dunia wa marathon Ruth Chpngetich.

Miongoni mwa wanamichezo Kipchoge aliwaangusha ni bingwa wa dunia mbio za mita 1,500, bingwa wa Olimpiki na wa dunia mbio za mita 3000 kuruka vizuizi na maji, Conseslus Kipruto.

"Nafurahia sana kushinda tuzo hii, inamaanisha watu wametambua niliyofanya Vienna kwa kukimbi chini ya saa mbili katika marathon. Napenda kuwaambia watu kuwa hazikua mbio ya ushindi ila kutuma ujumbe ya kwamba hakuna lisilowezekana dunia," anasema Kipchoge.

Timu bora kwa wanaume ilikua ni klabu ya mpira ya Bandari na Malkia Strikers kwa wanawake.

Malkia Strikers ilishinda taji la voliboli katika michezo ya mataifa ya Afrika nchini Morocco na hatimaye ikashiriki kombe la dunia nchini Japan.

"Ushindi huu wa tuzo la timu bora umetuongezea motisha sana. Tunajiandaa sasa kwa michezo ya Olimpiki.

Huko tunaenda kubeba kombe," anasema nahodha wa Malkia Strikers Mercy Moim ambaye anafanya kazi na idara ya Magereza.

Mkufunzi wa Malkia Strikers Paul Bitok alishinda tuzo la kocha bora.