Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je unawezaje kufurahia msimu huu wa likizo licha ya gharama ya juu ya maisha?
Na Dinah Gahamanyi
BBC news Swahili
Je umewahi kujiuliza ni jinsi gani utaadhimisha na kuburudika katika msimu huu wa sherehe za sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya bila kujipata katika mzigo wa madeni mwaka ujao katika nyakati hizi ngumu kiuchumi ?
Kwa kawaida mwezi Disemba ni msimu wa sherehe, wa kufurahi na kujumuika na marafiki…msimu ambao ni wa matumizi.
Msimu huu huambatana na mapambo, kununua zawadi kwa wapendwa, kusafiri na kununua vyakula tuvipendavyo.
Inashauriwa na wataalamu wa mipango ya misimu ya sherehe kuweka akiba maalumu ya pesa kwa ajili ya msimu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka kwa ajili ya kupumzika na kuburudika, baada ya shughuli nyingi za mwaka mzima.
Hatahivyo usipokuwa na mpango unaofaa kwa msimu huu wa likizo uliojaa shughuli za sherehe, huenda ukajikuta unatumia pesa nyingi bila kutambua. Hii ina maana kwamba baadhi ya watu wataanza mwaka mpya kwa madeni.
Hatahivyo iwapo haujafanikiwa kufanya hivyo kutokana na hali ngumu ya uchumi usife moyo kwani kuna njia nyingi za kuburudika binafsi na familia.
Katika kipindi hiki watu wengi hufanya makosa kama vile kununua bidhaa kwa msukumo na sio kuweka vipaumbele vyako kwa utaratibu. Kuwa mwangalifu katika kutumia mfuko wako kwa pupa na kujikuta katika hali ngumu zaidi kifedha katika mwezi wa Januari.
Ni vyema kujipanga iwe unapanga kwenda likizo fupi kijijini, kupanga safari katika maeneo ya utalii au uamue kuwatembelea wapendwa wako nyumbani, haya ndio mambo yanayoweza kukusaidia hasa unapopanga bajeti katika kipindi hiki kigumu kiuchumi:
Nakili gharama zako za msimu huu
Hatua ya kwanza katika kupanga likizo ni kuandika kila kitu unachotaka kufanya. Kwa mfano iwapo ungependa kusafiri kwenda maeneo ya kujivinjari unatakiwa kuangalia bajeti ya pesa ulizonazo kwa ajili ya safari unayotarajia kuifanya. Jiulize maswali kama …itakugarimu kiasi gani? je pesa hizi ni ninazo? Na ni lazima nisafiri? Kuna maeneo mengine ninayoweza kujivinjari kwa gharama ndogo?.
Inapokuja katika suala la kupanga safari, wataalamu wa mipango ya safari za mapumziko (Hollyday planners) wanashauri kuwa ni vyema kusafiri katika makundi, kwa mfano familia au marafiki kuliko kusafiri ukiwa peke yako, mke na mume au wenza. ‘’Mnapokuwa kundi mnaweza kuchangia gharama mfano za mafuta ya gari na wanasema hoteli na maeneo ya starehe hupunguza gharama zake kwa wateja wanapokuwa katika makundi kuliko mtu binafsi au watu wawili’’, anasema Brenda Gatonye mtaalamu wa safari za utalii nchini Kenya.
Amua kuhusu kikomo chako cha matumizi
Ni vema kuamua ni kiasi gani cha pesa za matumizi ambacho uko tayari kukitumia wakati wa msimu huu.
Kumbuka iwapo unategemea mshahara wa kila mwezi, mshahara utakaolipwa Disemba ndio unaoutegemea ukutunze hadi mwisho wa Januari. Hivyo basi kama haukuweka akiba maalumu kwa ajili ya msimu huu ,huenda ikawa vigumu kwako kukidhi matakwa yako yote ya sherehe za msimu huu.
Tenga pesa kwa kila aina ya matumizi
Andaa orodha ya matumizi yako ya likizo , gharama zake na zingatia kikomo cha matumizi yako, kisha gawa kiasi cha pesa kwa kila gharama. Amua aina ya hoteli unayoweza kumudu, gharama zako za chakula, aina gani ya usafiri itakayofaa zaidi kulingana na bajeti yako.
Tengeneza orodha ya manunuzi
Baada ya kugawa pesa kwa kila aina matumizi , unaweza kuipunguza zaidi kwa kutengeneza orodha ya manunuzi ili kukusaidia kutofautisha mahitaji yako ya lazima na ya anasa. Orodha ya ununuzi itakusaidia kuzingatia bajeti yako na kuepuka tamaa ya kununua bidhaa kiholela hasa katika msimu huu ambapo makampuni ya biashara yamepunguza bei za bidhaa ili kuwavutia wateja wengi.
Zingatia malipo yako yote
Mara nyingi, kabla ya kwenda likizo na kuanza kutumia pesa, tunafanya tu makadirio ya bajeti na wakati mwingine yanaweza kuwa ya juu au ya chini kuliko tulivyotarajia.
Iwe ni kiasi cha pesa unachotumia kununua zawadi, gharama za usafiri au kutembelea mahali ulipopanga, kila mara andika kila kiasi unachotumia ili uweze kupima ni wapi bajeti yako itapungua au utahifadhi pesa gani. Hii inaweza pia kusaidia kuboresha matumizi yako wakati ujao.
Fikiri kabla ya kununua bidhaa
Katika msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka Krismasi na Mwaka mpya makampuni mengi ya kibiashara na wafanyabiashara huwa na mtindo wa kuuza bidhaa kwa gharama za chini na mengine huongeza gharama zao.
Kwahivyo unashauriwa usinunue tu kitu cha kwanza unachokiona kwenye duka, linganisha bei na uangalie ni biashara gani zinazonadi punguzo la gharama ya bei ili kuepuka matumizi ya pesa zaidi katika kipindi hiki.
Usitoe zawadi za binafsi
Inategemea na kiwango cha pesa ulichonacho, lakini huenda ikawa gharama kubwa kumnunulia zawadi kila mmoja wa marafiki au jamaa
. Unaweza kukubaliana na marafiki zako kununua zawadi na kwa pamoja kuzawadiana badala ya kununua na kumzawadia mmoja mmoja.
Kumbuka kuwa lengo la muhimu la msimu huu ni kufurahi, kupumzika na kujumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki hasa baada ya kazi na majukumu ya mwaka mzima, na unaweza kufikia lengo hili kwa kujumuika na wapendwa wako katika shughuli ambazo sio gharama kubwa na lengo hili kutimia.
Yafuatayo ni mambo unayoweza kuyafanya na kufurahi na wapendwa wako bila kutumia gharama kubwa:
- Kutembelea maeneo ya wazi ya umma yenye shughuli za burudani
- Kutembelea matukio ya kidini yaliyoandaliwa bila malipo
- Kupanga sherehe ya kifamilia japo mpango wa awali unapaswa kuwekwa kugharamia kwa pamoja vitu kama chakula na vinywaji miongoni mwa wanafamilia
- Kupanda vilima au mlima (mfano kikundi cha marafiki au wanafamilia)
- Kufanya pikiniki ya pamoja ya kikundi cha marafiki au familia
- Kushiriki chakula (cha mchana au cha jioni) na marafiki
Watu wengi hufikiria tu kuhusu utoaji wa zawadi na kupuuza mambo mengine ambayo pia hugharimu pesa wakati wa msimu wenye shamrashamra za sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya na hali inapoanza kuwa ngumu hujiuliza ni kwa namna gani walivyopungukiwa pesa au hata kuishiwa kabisa.
Kuna mambo mengi ya kununua wakati huu wa krismasi lakini kumbuka kuna mwezi unaofuata ambao una majukumu mengi zaidi.
Januari huwa ni mwezi mgumu sana, majukumu huwa mengi. Ni vyema kuwa na kikomo katika bajeti yako. Kuwa mwangalifu unapotumia pesa msimu huu.
Imehaririwa na Yusuf Jumah