Je, unaijua familia tajiri zaidi duniani?

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari linalotoa habari za biashara, Bloomberg, utajiri jumla wa baadhi ya familia tajiri zaidi ulimwenguni umeongezeka kwa dola trilioni moja na nusu mwaka 2023.

Utajiri wa familia ya Al Nahyan inayotawala Abu Dhabi na utajiri wa nyumba ya ubunifu wa kifahari ya Hermès huko Ufaransa, umeongezeka 2023.

Familia ya kifalme ya Abu Dhabi, Al Nahyan, ndiyo iliyoongoza orodha ya familia tajiri zaidi duniani mwaka huu ikiwa na utajiri wa dola bilioni 305, ikiipiku familia ya Walton ya Marekani, wamiliki wa maduka ya Walmart kwa kiasi cha dola bilioni 45.

Familia ya Al Nahyan inadhibiti eneo lenye utajiri wa mafuta ghafi la UAE la Abu Dhabi na inamiliki Manchester United, klabu maarufu zaidi ya kandanda duniani.

Familia ya Althani ya Qatar ipo nafasi ya tano katika orodha hii.

Familia ya Bay Area imejumuishwa katika orodha ya Bloomberg zinaaminika kuwa na utajiri mwingi kuliko ilivyokadiriwa.

Kulingana na Bloomberg, ukubwa wa International Holdings, kampuni ya hisa ya biashara inayoendeshwa na familia ya kifalme ya Abu Dhabi, imekua kwa karibu asilimia elfu saba katika miaka minne iliyopita.

Familia ya taifa hilo la Ghuba sio tu imebadilisha utajiri wake, pia imebadilisha mwelekeo wa uchumi wa eneo hilo.

Historia ya Familia ya Al Nahyan

Abu Dhabi, mojawapo ya majimbo saba ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mji mkuu wa nchi hiyo na ina akiba nyingi ya mafuta.

Familia hiyo ilitawala eneo hilo kwa miongo kadhaa kabla ya kugunduliwa mafuta. Lakini wakati huo haikuwa tajiri kama ilivyo sasa.

Hadithi ya Falme za Kiarabu na familia ya Al Nahyan ilianza katika miaka ya 1960 na ugunduzi wa mafuta katika eneo hilo.

Hapo awali, idadi kubwa ya wakazi wa nchi hiyo walikosa huduma za kimsingi, lakini mara baada ya kupatikana mafuta, Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan alilibadilisha eneo hilo na kuziunganisha falme zote za eneo hilo na kuunda nchi inayoitwa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan pia anaitwa 'Baba wa Taifa' na alifanywa kuwa Rais wa nchi mwaka 1971.

Mwaka wa 2004 mwanawe Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan alimrithi baba yake kama mkuu wa UAE. Mwaka 2022 Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, aliyesoma katika Chuo cha Kijeshi cha Uingereza huko Sandhurst, akawa Rais wa tatu wa UAE.

Wengine katika familia ya Al Nahyan hutekeleza majukumu katika serikali ya UAE na sekta binafsi.

Burj Khalifa, jengo refu zaidi duniani huko Dubai, limepewa jina kwa heshima ya Rais wa zamani wa UAE, Khalifa bin Zayed Al Nahyan.

Ugunduzi wa mafuta

Akizungumza na BBC mwandishi kutoka Abu Dhabi, Mohammed Al Fahim, alisema Zaid bin Sultan, mtawala wa Abu Dhabi, alibadilisha sio tu familia yake, lakini eneo hilo.

Kabla ya kugunduliwa mafuta, wakazi wa hapa hawakuwa na huduma za kimsingi. Watu walikuwa na mahema tu na ilibidi watembee maili nyingi kupata maji safi ya kunywa.

Baada ya kupatikana mafuta, mtawala mwenye maono wa Abu Dhabi, Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan, alianza kujenga barabara, hospitali na majengo muhimu nchini humo.

Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1960, Uingereza ilikuwa imeanza kujiondoa katika makoloni yake katika nchi za Kiarabu. Karne moja iliyopita Waingereza walifika huko wakati ambapo baadhi ya makabila yalikuwa yakipora meli za mizigo zinazopita.

Waingereza walifika ili kupata udhibiti wa eneo hilo. Hata hivyo, mafuta yaligunduliwa na Waingereza waliondoka, waliona kuna hatari kubwa kuliko faida za kukaa huko.

Sababu kuu ni uamuzi uliochukuliwa na Masheikh wa falme sita (Dubai, Abu Dhabi, Sharjah, Ajman, Ummal Quain, Fujairah) kuunda baraza la maelewano na ushirikiano.

Shauku ya Sheikh Zayed ilikuwa jambo muhimu katika kuundwa kwa Umoja wa Falme za Kiarabu. Pia aliomba uungwaji mkono wa maridhiano kati ya watawala wenzake.

Hatimaye watawala wa falme sita (isipokuwa Ras Al Khaimah) kwa kauli moja walimchagua Sheikh Zayed kuwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ras Al Khaimah ilijiunga na Umoja wa Falme za Kiarabu tarehe 10 Februari 1972.

Ni vyema kutambua kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu ni nchi yenye majimbo saba huru, zikiwemo Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Umm al-Qawi, Fuzaira, Ajman na Ras Al Khaimah.

Abu Dhabi ni jimbo kubwa zaidi la Umoja wa Falme za Kiarabu, linalochukua asilimia 84 ya nchi.

Mwanahistoria Ruri Miller anasema mafanikio ya kiuchumi ya nchi hiyo ni kutokana na mgawanyo wa mapato ya mafuta na umiliki wa mali kama majengo na hisa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah