Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Malkia Latifa: UN kuhoji UAE kuhusu binti wa mtawala wa Dubai
Umoja wa Mataifa umesema utaingilia kati hatua ya mamlaka ya Milki za Kiarabu (UAE) kumshikilia bila hiari Malkia Latifa, binti ya mtawala wa Dubai.
Malkia Latifa amemlaumu baba yake kwa kumzuilia mateka Dubai tangu alipojaribu kutoroka mji huo mwaka 2018.
Katika video iliyorekodiwa kisiri na kuwasilishwa kwa BBC, Malkia Latifa amesema kuwa anahofia maisha yake.
Video hiyo imezua hisia kali kote duniani huku wito ukitolewa kwa Umoja wa Mataifa kuchunguza suala hilo.
Ofisi ya Kamishena Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa imejibu wito huo na inaazimia kuhoji kuhusu hali ya Latifa, binti wa mtawala wa Dubai.
Msemaji wa kundi la Umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya watu kuzuiiliwa bila hiari yao amesema kundi hilo litaanzisha uchunguzi baada ya video ya Malkia Latifa kuhakikiwa.
Ofisi ya Maendeleao na Mambo ya nje ya Uingereza na imeelezea hofu yake kuhusiana na kisa hicho na kuongeza kuwa japo haihusiki moja kwa moja na kesi hiyo itafuatilia kwa karibu matukio hayo.
Baba yake Malkia Latifa, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum,ni mmoja wa wakuu tajiri zaidi wa nchi ulimwenguni, mtawala wa Dubai na makamu wa rais wa UAE.
Sheikh Mohammed amejenga jiji lenye mafanikio makubwa lakini wanaharakati wa haki wanasema hana uvumilivu na wapinzani na mfumo wa mahakama unaweza kuwabagua wanawake.
Kupitia msaada wa marafikimwezi Februari mwaka 2018 Malkia Latifa alijaribu kutoroka Dubai kwenda kuanza maisha mapya.
"Siruhusiwi kuendesha gari, Siruhusiwi kusafiri wala kuondoka Dubai kabisa," Malki Latifa alisema katika video aliyorekodi muda mfupi kabla ya kutoroka.
Lakini siku chache baada ya kutoroka, Malkia Latifa alikamatwa kwenye boti na makomando katika Bahari ya Hindi. Malkia huyo alisafirishwa kwa ndege hadi Dubai, ambako amesalia tangu wakati huo.
Baba yake alisema amefanya hivyo kwa maslahi ya binti yake. Dubai na UAE zimewahi kusema siku zilizopita kwamba Malkia Latifa yuko salama mikononi mwa familia yake.
Sheikh Mohammed ana biashara kubwa ya mbio za farasi na mara nyingi huhudhuria hafla kubwa kama Royal Ascot, ambapo amepigwa picha na Malkia Elizabeth II.
Lakini Sheikh Mohammed amekosolewa vikali kuhusiana na Malkia Latifa na mama yake wa kambo, Malkia Haya Bint Al Hussain, ambaye alitorokokea London mwaka 2019 na watoto wake wawili.
Video ya Malkia Latifa ilipatikana na BBC Panorama, ambayo imethibitisha maelezo ya mahali aliposhikiliwa.
Video hizo zilirekodiwa kisiri kwa miezi kadhaa kupitia simu phone kwa karibu mwaka mmoja baada ya kushikwa kwake na kurudishwa Dubai. Alizirekodia bafuni kwani dio sehemu pekee iliyokuwa na mlango ambao angeliweza kuufunga.
Katika ujumbe wake alielezea kwa kina jinsi:
- Alivyokabiliana na maaskari waliokuwa wakimtoa kwenye boti, "kurusha mateke na kupigana" na kumuuma mkono mmoja wa makomando wa Emirati
- baada ya kudungwa sindano alipoteza fahamu alipokuwa amebebwa katika ndege ya kibinafsi, na hakuamka hadi ndege ilipotua Dubai.
- alizuiliwa peke yake bila kupata huduma za afya na usaidizi wa kisheria katika nyumba ambayo milango na madirisha ilikuwa imefungwa huku ikilindwa na polisi.
Kisa cha jinsi Malkia Latifa alivyokamatwa na kuzuiliwa kilifichuliwa na rafiki wake wa karibu Tiina Jauhiainen, ndugu yake upande wa mama Marcus Essabri na mwanaharakati David Haigh, ambao wote wanaendesha kampeni ya kushinikiza kuachiwa huru kwa Latifa.
Wanasema walitoa ujumbe huo kwa kuhofia usalama wa Malkia Latifa.