Jamii Zanzibar inavyopambania mustakabali wa maisha kwenye matumbawe

    • Author, Na Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Zanzibar

Unapofika katika kisiwa cha Mnemba, Kaskazini Mashariki mwa Zanzibar utaona fukwe safi, mchanga mweupe lakini zaidi kwa umakini utaona matumbawe ‘coral reefs’ kwa chini, hatua chache tu pembezoni mwa kisiwa hicho.

Miamba katika kisiwa hicho, ni ya kuvutia, yenye maumbo mbalimbali na muonekano wa kipekee.

Visiwani Zanzibar, hufahamika zaidi kama ‘Coral Reef’ lakini waswahili huita matumbawe. Haya hupatikana katika sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Zanzibar.

Matumbawe ni muhimu katika ukuaji wa viumbe hai majini kwani ni sehemu ya asilia ya mazalia ya samaki na viumbe hai wengine wa baharini.

Matumbawe yanapotunzwa, wananchi hupata samaki kwa wingi. Pia shughuli za utalii hushamiri katika eneo hilo yaani ‘house reef’ na kuchangia katika kukua kwa uchumi wa bahari (uchumi wa bluu).

Kwa sasa, wataalamu wanasema mabadiliko ya tabia nchi, uvuvi usio endelevu, na shughuli za utalii ni miongoni mwa vitu vinavyoathiri miamba ya matumbawe.

Kuimarisha hali, uhifadhi unafanywa na jamii, wanasayansi, wasimamizi, watunga sera, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), na wafadhili wahisani.

Kwa Zanzibar haswa eneo la Mnemba, mradi huu unakarabati miamba ya matumbawe katika maeneo yaliyoharibiwa kando ya fukwe. Mradi pia unalenga kushughulikia changamoto zinazokabili miamba ya matumbawe, zikiwemo shughuli zisizo endelevu za binadamu.

Matumbawe hatarini

Mabadiliko ya tabia nchin, uvuvi usiofaa ukiwemo wa kutumia baruti na mikuki, pamoja na boti za kitalii huchangia katika uharibifu.

Juma Mshindani, mfanyabiashara wa ndani wa Samaki anasema, "Upatikanaji wa samaki siku za nyuma ikilinganishwa na sasa una tofauti kubwa…

“Zamani kulikuwa na samaki wengi. Lakini sasa idadi ya watu ni kubwa na mbinu zisizofaa za uvuvi zimeongezeka kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mitego mbalimbali kama vile nyavu na nyaya,” anasema Mshindani

Mshindani anasema baadhi ya wavuvi wanatumia vifaa hatarishi kwa Samaki na matumbawe kama vile nyavu zisizokuwa za viwango.

Uharibifu wa mwamba wa Mnemba umekithiri kiasi cha jamii kutambua kama wasipofanya kazi ya kuuhifadhi, si tu kwamba ungetoweka, bali pia watalazimika kuhama kutokana na ukosefu wa kipato.

Urejeshwaji matumbawe

Septemba 2021, jamii ilianza kushirikiana na shirika la & Beyond naAfrican Foundation katika kurekebisha miamba hiyo, kulinda eneo la hifadhi ya baharini, na kusaidia katika uvuvi endelevu.

Kwa mujibu wa Africa Foundation, wanafanya hivyo kwa kujenga bustani za majini ambapo ndipo wanapotengeneza matumbawe ya kisasa.

Matumbawe mapya hupandikizwa kwenye maeneo ya miamba iliyopo ambayo imeharibiwa.

Hija Uledi ambaye ni mhifadhi kwenye kisiwa hicho anasema miaka mitatu tangu kuanza kwa mradi huu, matokeo yanatia moyo huku asilimia 80 ya matumbawe yakiwa yamerudishwa.

Haji anasema, "Tumerudisha uhai kwenye miamba, na huwezi kutofautisha miamba ya kisasa na ile ya asili. Sasa samaki wameanza kuongezeka katika eneo hili lenye matumbawe.”

Naye Dkt. Camilla Floros, Meneja Programu na Mwanasayansi katika Bahari wa Oceans Without Borders, anasema mpango wa urejeshaji ni mzuri iwapo utafanyika kwa ustadi mkubwa.

"Kutumia nyenzo zisizo sahihi kwa miamba bandia kunaweza kuwa na matokeo mabaya. Wakati miamba ya bandia ilipokuwa changa, watu walitumia nyenzo zisizo sahihi kama vile kutumia matairi kujaribu kuunda miamba ya bandia, ambayo sio njia sahihi…

"…tulichofanya ni kwamba tumetumia miamba ya asili ya matumbawe katika uundaji wa matumbawe ya kisasa," anasema Camilla.

Kulingana na Dkt. Camilla, aina hii ya mradi ni muhimu kuungwa mkono na jamii inayozunguka pamoja na serikali kwani ni kwa faida yao.

"Kila tunapokuwa na mpango mpya, tunaujadili pamoja nao, na tunapata nafasi yao ya kushiriki na ndiyo maana mengi wanayafanya ikiwemo utoaji elimu," anasema.

Atuwa Omar, 24 ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye anajihusisha na ukarabati wa matumbawe. Kabla ya mhifadhi, alikuwa nyumbani akimtunza mwanae.

“Kuwa mhifadhi katika mradi huu katika kisiwa cha Mnemba si tu kunaniwezesha kulisha familia yangu bali pia kunasaidia elimu ya mwanangu ambaye angali ameanza shule ya msingi,” anasema.

Kwa sasa Atuwa ndiye mwanamke pekee anayefanya kazi katika mradi huo, ambapo anasema alipata changamoto awali tena zinazohusu jinsi yake.

“Nilikumbana na kukatishwa tamaa, hasa kutoka kwa wanaume, ambao walitilia shaka uamuzi wangu wa kutafuta kazi inayoonekana kuwa ya wanaume. Hata hivyo, ninaamini kabisa kuwa kazi haipaswi kuwa ya jinsi moja,” anasema.

Mfumo utalii, uvuvi wabadilika

Kurejesha uhai kwa matumbawe si tu kurekebisha hali ya miamba hiyo bali pia kuzuia au kupunguza shughuli za utalii na uvuvi katika eneo husika.

"Hapo awali, eneo hilo lilikabiliwa na msongamano mkubwa kutokana na shughuli za utalii, na boti 200 zilizobeba wageni wasiopungua 400 zikiingia eneo la mita za mraba 200 tu," anasema Bakari Jaha, Mratibu wa Africa Foundation Zanzibar huku akieleza kuwa wingi wa watalii wanaotembelea miamba hiyo ni hatari kwa miamba hiyo.

Bakari anasema, "Ili kuhifadhi eneo hilo, serikali pamoja na mashirika ya &Beyond na Africa Foundation iliamua kupunguza idadi ya wageni hadi 80 kwa siku…

“…hapo awali, wageni walitozwa dola za kimarekani 3 kila mmoja kutembelea miamba hiyo. Gharama hii sasa imeongezeka hadi dola 25. Njia hii si tu imeimarisha uhifadhi wa mazingira lakini pia imeongeza mapato," anasema Jaha.

Uvuvi uliokuwa ukisababisha uharibifu mkubwa umesitishwa katika maeneo ambayo miamba hiyo inarejeshwa na sasa huenda wakazi wa eneo hilo wakaneemeka.

“Tumeona mabadiliko chanya, uvuvi haramu kama vile utumiaji wa mabomu vimepungua, na wavuvi wamekuwa na uelewa zaidi kuhusu mbinu endelevu za uvuvi,” anasema Mshenga Ally ambaye amefanya kazi za uvuvi kwa zaidi ya miaka 30.

Unaweza pia kusoma

Mkakati wa Serikali

Kufuatia hali inavyoendelea katika kiswa cha Mnemba, Serikali ya Zanzibar inatazamia kuendeleza mradi wa matumbawe kwenye maeneo mengine yaliyo hatarini.

Mkurugenzi wa Idara ya Bahari Zanzibar, Dkt. Makame Omar “Serikali imebaini maeneo 14 yenye matumbawe ambapo baadhi tayari yameathirika, nao wamejipanga kuyahifadhi... Pia tumeweka maboya kwenye mpaka wa maeneo yenye matumbawe ili wananchi wawe makini ili wasifanye shughuli za uvuvi.

Je wajua?

Miamba ya matumbawe ni baadhi ya mifumo ya ikolojia yenye thamani zaidi katika sayari. Wakati inafunika takriban 0.1% ya sakafu ya bahari, na inahifadhi angalau robo ya aina zote za viumbe hai wa baharini na inasaidia takriban aina 4,000 za samaki na aina 800 za matumbawe.

Matumbawe ni nini?

Miamba ya matumbawe ni mojawapo ya vitu vya kuvutia katika maumbile ya dunia! Zamani baadhi ya watu walifikiri kuwa matumbawe yalikuwa aina ya mawe, lakini sasa wanaelewa kuwa matumbawe ni mkusanyiko wa wanyama wadogo sana wanaoitwa ‘polipu’ (polyps) ambao wana kiunzi cha mfupa mgumu kwa nje mithili ya jiwe.

Pia soma:

Imehaririwa na Florian Kaijage