Dhuluma za kikoloni zatanda katika ziara ya Mfalme Charles nchini Kenya

- Author, Anne Soy
- Nafasi, Mwandishi mwandamizi wa Afrika, Nairobi
Mfalme Charles na mkewe Camilla wako katika ziara ya kiserikali ya siku nne nchini Kenya, ambapo atakubali "matukio ya uchungu" ya enzi ya ukoloni wa Uingereza.
Zaidi ya watu 10,000 waliuawa na wengine kuteswa wakati wa ukandamizaji wa kikatili wa uasi wa Mau Mau katika miaka ya 1950, mojawapo ya uasi wa umwagaji damu zaidi wa Dola ya Uingereza. Mwaka wa 2013 Uingereza ilionyesha majuto na kulipa pauni milioni 20 ($24m) kwa zaidi ya watu 5,000 - lakini wengine wanahisi hiyo haikutosha.
Mmoja wao ni Agnes Muthoni mwenye umri wa miaka 90.
Kwa mwendo wa kasi licha ya kuinama, anatuongoza hadi kwenye eneo la kaburi nyumbani kwake huko Shamata, katikati mwa Kenya.
Anang'oa magugu yaliyoota karibu na kaburi la mumewe. Elijah Kinyua alifariki miaka miwili iliyopita, akiwa na umri wa miaka 93. Alijulikana pia kama Jenerali Bahati, na sawa na mke wake alikuwa mpiganaji wakati wa uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali ya kikoloni ya Dola ya Uingereza katika miaka ya 1950.
Alishikilia cheo cha meja katika Jeshi la Ardhi na Uhuru wa Kenya - linalojulikana zaidi kama Mau Mau.
Bi Muthoni anaanza kutabasamu huku akituonyesha pete yake ya ndoa. Walikutana tu baada tu ya uasi kuisha na akaachiliwa kutoka kizuizini.
"Alisema kama kungekuwa na wapiganaji wanawake walionusurika, angependa kuoa mmoja wao kwa sababu ataelewa matatizo yake na hatamwita Mau Mau."

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mapambano yaliwaunganisha. Lakini hata baada ya Kenya kupata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza, wanandoa hao waliendelea kuishi kwa kujificha - kama wapiganaji wengi wa zamani wa Mau Mau.
Kundi hilo la upinzani lilisalia kuwa haramu. Lilitambuliwa kuwa shirika la kigaidi na serikali ya kikoloni na tawala zilizofuata katika Kenya huru hazikubatilisha marufuku hiyo. "Wanachama watatu wa Mau Mau hawakuweza kukutana; lilikuwa kosa," anasema wakili wa Kenya na mwanasiasa Paul Muite. "Ilikuwa ya kikatili."
Waliendelea kuishi hivyo hadi mwaka wa 2003 ambapo sheria ilibadilishwa, na wanachama wa Mau Mau hatimaye walitambuliwa kama wapigania uhuru.
Lakini hii pia ilimaanisha kuwa vizazi vya baada ya uhuru vilikuwa na ufahamu mdogo wa yale yaliyopita.
"Watoto na wajukuu wengi hawakujua kuhusu mizizi ya mateso ya nchi ambayo ilizaa uhuru," anasema mwanahistoria Caroline Elkins, ambaye alifanya mahojiano kuhusu mada hiyo katika miaka ya 1990.
Maoni yake yanaungwa mkono katika mitaa ya Nairobi hadi waleo. Vijana wengi hawajui kuhusu kuzuiliwa na kuteswa kwa Mau Mau. Wanajali zaidi kuhusu uchumi na wanashangaa ikiwa ziara ya Mfalme Charles itakuwa na athari yoyote.
Mjukuu wa Bi Muthoni mwenye umri wa miaka 36, Wachira Githui, ni mmoja wa wachache waliosikia kulihusu. Lakini pia anafurahia urithi wa kudumu wa ukoloni katika maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ya Kenya. "Nazungumza Kiingereza na ninajivunia hilo," anasema, akiongeza kuwa yeye ni shabiki wa klabu ya soka ya Chelsea.
Mitandao ya kijamii ya Kenya huwa hai wakati mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya Uingereza unapowashwa. Mashabiki wanataniana kwa saa kadhaa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutoka mitaani hadi maofisini, urithi wa himaya hiyo bado unaonekana Nairobi.
Gauni jeusi lililofungwa vizuri na mikanda nyeupe shingoni yaning'inia nyuma ya meza ya Paul Muite katika ofisi yake katika mtaa wa Kilimani. Yeye huvaa wigi pia wakati akifika mahakamani. Sehemu kubwa ya miundo ya sheria, utawala na elimu ya Uingereza ilirithiwa sio tu nchini Kenya bali katika sehemu kubwa ya himaya ya zamani.
Lakini ujuzi wa mambo mengi ya "zamani chungu zaidi" ambayo Mfalme anatarajiwa kukiri haukupitishwa kwa vizazi, na hubaki kufichwa kutoka kwa umma.
Bw Muite anatoa wito kwa tume ya uchunguzi iundwe na serikali za Kenya na Uingereza kwenda kila sehemu ya Kenya na kuandika kwa kina kipindi cha ukoloni. Alikuwa sehemu ya timu ya wanasheria iliyowasilisha kesi katika mahakama za Uingereza mwaka wa 2009, ambayo ilimalizika kwa suluhu nje ya mahakama miaka minne baadaye.
Serikali ya Uingereza ilionyesha majuto na kulipa fidia kwa maveterani wa Mau Mau.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini Bw Muite anasema ni wapiganaji ambao bado wako hai tu ndio waliochunguzwa na madaktari na kuthibitishwa kuwa waathiriwa wa mateso walipokea malipo. Wale waliotoa huduma na kudumisha laini za usambazaji kwa wapiganaji, pamoja na Wakenya nje ya katikati mwa nchi ambao walipigana dhidi ya ukoloni, hawakujumuishwa, anasema.
Miongoni mwao ni watu wa ukoo wa Talai, ambao hivi majuzi wametoa wito kwa serikali ya Uingereza kurejesha fuvu la kiongozi wao Koitalel arap Samoei. Aliongoza upinzani wa jamii ya Nandi dhidi ya makazi ya wakoloni, na kutatiza mipango ya kukalia nyanda za juu za Bonde la Ufa kwa zaidi ya muongo mmoja. Hatimaye, alialikwa kilaghai kwenye mkutano wa amani ambapo aliuawa mwaka wa 1905.
Bw Muite anasema kuwa kutambua "wale waliouawa, waliotoa huduma ikiwa ni pamoja na chakula kwa wapiganaji wa Mau Mau na wale waliobakwa, na kuwapa fidia kidogo" kutawasaidia kupata faraja.
Mwanahistoria Caroline Elkins anasema tangazo linalotarajiwa la mfalme litakuwa "wakati wa ajabu" lakini anaongeza kuwa jambo sahihi litakuwa "kusisitiza uchunguzi sahihi, unaofanywa na serikali, kubadilisha vitabu vya historia, kubadilisha makumbusho nchini Uingereza na kutoa ufadhili nchini Kenya kuanzisha majumba yake ya makumbusho na sanaa za kitamaduni".
Anasema ukatili uliofanywa wakati wa hali ya hatari - uliotangazwa na serikali ya kikoloni mnamo Oktoba 1952 kukabiliana na uasi wa Mau Mau - ulifanywa kwa jina la mfalme. Malkia Elizabeth II alikalia kiti cha ufalme miezi minane tu iliyopita alipokuwa ziarani katikati mwa Kenya ambako uasi ulikuwa umeanza.
"Ni Malkia ambaye picha yake ilitundikwa katika kambi za kizuizini, [na] walipokuwa wakiteswa na kulazimishwa kufanya kazi, ilibidi waimbe Mungu Mlinde Malkia."
Mashambulizi dhidi ya Mau Mau yanaweza kuwa ya kikatili, na mara nyingi yangetokea usiku. Picha za Michael Ruck mwenye umri wa miaka sita - aliyekatwakatwa hadi kufa pamoja na wazazi wake na mkulima - na dubu wake teddy waliokuwa wamemwaga damu, zilichapishwa kwenye magazeti nje ya nchi, na hazikuonyesha huruma kwa wapiganaji.
Serikali ya kikoloni ilitumia nguvu zake za anga na vikosi vya ardhini ambavyo vilijumuisha Wakenya wengi - wanaojulikana kama walinzi wa nyumbani - kuandaa ukandamizaji wa kikatili dhidi ya Mau Mau.
Bi Elkins anakadiria kuwa takriban watu 320,000 waliwekwa kizuizini au kambi za mateso. Wafungwa waliripotiwa kuhasiwa, kuchapwa viboko hadi kufa, na hata kuchomwa moto.

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya 1,000 waliuawa kwa kunyongwa wakati wa kipindi cha dharura. Idadi ya waliofariki inakadiriwa kuwa maelfu. Wanahistoria wameelezea oparesheni za kumaliza uasi huo kama vita vya umwagaji damu zaidi vya baada ya vita ambavyo Uingereza ilihusika katika karne iliyopita.
"Hatukuwa na nyumba za kuishi," anasema mkongwe Agnes Muthoni kuhusu mazingira walioishi katika msitu wakati wa dharura. "Kulikuwa na fisi, njaa na mvua."
Sasa anaishi katika eneo la milima ya Aberdare.
Ardhi kubwa yenye rutuba inayoenea katikati mwa Kenya hadi Bonde la Ufa ilijulikana kama "White Highlands". Ilikuwa Inamilikiwa na wakulima walowezi pekee. Wenyeji, kama Bi Muthoni, walisukumwa pembeni ili kuwatengenezea njia wakulima wa Uropa kumiliki ardhi bora zaidi.
Baada ya uhuru sehemu kubwa ilienda kwa walinzi wa nyumbani, kwani Mau Mau iliendelea kuchukuliwa kuwa shirika la kigaidi.
Lakini Bi Muthoni yuko tayari kuachana na yaliyopita. "Hatuna uchungu mioyoni mwetu kwa sababu ya kale yamepita," anasema.
"Binadamu tusameheane na tuendelee kuishi pamoja, lakini ningependa nipewe ardhi."












