'Nimeshindwa kuwashawishi wazazi wangu kuondoka nyumbani kwao': Hofu ya mwandishi wa BBC mjini Tehran

Parham Ghobadi wa Idhaa ya Kiajemi ya BBC ameshindwa kuwashawishi wazazi wake kuondoka Tehran; nyuso zao zimekuwa na ukungu ili kulinda utambulisho wao endapo watalipizwa kisasi na taifa la Iran.

Chanzo cha picha, Parham Ghobadi

Muda wa kusoma: Dakika 4

''Sijaweza kuwashawishi wazazi wangu kuondoka nyumbani mwao, achilia mbali Tehran, baada ya Donald Trump kuwataka wakazi "kuondoka mara moja" katika mji mkuu wa Iran.

Baba yangu aliniambia, "Katika umri wetu, na kila aina ya masuala ya kiafya, hatuwezi kuvumilia msongamano wa magari kwa saa kadhaa na kisha kukabiliwa na uhaba wa mahitaji ya kimsingi katika miji iliyojaa watu baada ya kuondoka Tehran. Heri tusalie nyumbani kwetu."

Wazazi wangu wana kisukari. Kwa mwezi mmoja uliopita, mama yangu amekuwa nyumbani kwa sababu ya kizunguzungu kikali na anaweza tu kutembea kwa usaidizi.

Baba yangu anaugua mfululizo wa magonjwa sugu na anatembea kwa shida na kulazimika kusimama na kupumzika.

Unaweza kusoma
Wanaume kadhaa wamesimama juu ya mlima wakitazama moshi ukitoka kwenye jengo la shirika la utangazaji la taifa la Iran baada ya kulipuliwa na Israel.

Chanzo cha picha, Reuters

Kuondoka si rahisi kwa kila mtu

Lakini si wazazi wangu pekee wanaosalia.

Mwanamke mmoja kutoka Iran ananieleza kwamba wazazi wake hawataki kuondoka Tehran: "Wanaamini ni bora kufa kwa heshima nyumbani kwao kuliko kuhamishwa."

Anasema aliambiwa, "Ikiwa nyumba yetu itaharibiwa, ni afadhali tushuke nayo."

Mwanamke mwingine kutoka Tehran anaelezea kwa nini, kwa wengi, kuondoka ni vigumu: "Hata tuna majirani ambao wanaugua ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu. Tuna majirani kwenye viti vya magurudumu."

Kwa wale ambao wameamua kukaa, au hawawezi kuondoka, maisha si rahisi.

Chakula na mafuta ni haba

Magari yamesongamana wakati watu wakijaribu kuondoka Tehran.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Magari yamesongamana wakati watu wakijaribu kuondoka Tehran.

Mashine za kutoa fedha (ATM) nyingi ni tupu. Ni duka moja tu kati ya kumi ambalo limefunguliwa, kulingana na mwanamke mwingine huko Tehran.

Mkazi mmoja ananiambia kuwa jengo lake halina maji baada ya bomba kupasuka mwanzoni mwa mzozo, na kwamba hakuna fundi bomba wa kulirekebisha.

"Tumewapeleka watoto sehemu salama, lakini tumekaa, kwa ajili ya paka katika jiji letu, kwa usalama wa majengo yetu. Mungu akipenda, yataisha," mtu mmoja aliniambia.

Alikuwa akizungumzia paka wengi wanaoishi katika mitaa ya jiji hilo na wanatunzwa na wakazi wengi.

Tehran ina jumba la kumbukumbu la paka na mkahawa wabinafsi, Meowseum, na ni maarufu kwa kuwa na paka wengi wa mitaani.

Chanzo cha picha, Atta Kenare / AFP via Getty Images

Kizuizi

Tehran ina watu wengi kama Israel yote. Hebu waza kujaribu kuhamisha jiji hili kuu lenye shughuli nyingi na barabara zilizosongamana na mafuta yaliyogawiwa.

Kila dereva anaruhusiwa tu lita 25 za petroli kwa siku, na wale wanaojaribu kuondoka hukumbana na foleni zinazowaka barabarani kwaa saa nyingi

Wengine waliniambia kuwa waliishiwa na mafuta wakiwa nusu safari.

Wengi wanakimbilia majimbo tulivu ya kaskazini ya Mazandaran na Gilan.

Safari ambayo kwa kawaida huchukua saa tatu hadi nne kutoka Tehran imechukua baadhi ya madereva zaidi ya saa kumi na mbili katika siku za hivi karibuni.

Watu wakitazama moto kutoka bohari ya mafuta ya Shahran mjini Tehran siku ya Jumatatu baada ya Israel kuishambulia.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Siku hizi tumekuwa tukiangalia foleni ya magari, tukitumai kuondoka wakati wa mapumziko. Lakini mwishowe, bado tumekwama kwenye trafiki," anasema mkazi mwingine.

"Ni moto usiovumilika, na kutokana na uhaba wa mafuta, hakuna mtu anayeweza kutumia kiyoyozi. Baadhi ya magari yaliharibika au kukosa mafuta njiani. Kuna njia za urefu wa maili katika kila kituo cha mafuta."

Na wale wanaofika wanakoenda wanakabiliwa na changamoto mpya: hakuna maeneo ya kutosha ya kukodi.

Bei ya vyakula imepanda sana. Teksi hutoza nauli kubwa kusafirisha watu.

Moshi ukifuka kutoka kwenye vifusi vya jengo la vyombo vya habari vya serikali ya Iran mjini Tehran kufuatia shambulizi la anga la Israel.

Chanzo cha picha, MINA / Getty Images

Unataka tu kusema "tuliwaambia" mara watakapotuua?

Wairani wengi wanahisi kutumbukia katika vita ambavyo hawakuwahi kuchagua, baada ya miongo kadhaa ya ukandamizaji.

"Si Benjamin Netanyahu (waziri mkuu wa Israel) wala Israel wala Jamhuri ya Kiislamu wanaotujali," mwanaume mmoja kutoka Tehran ambaye aliamua kusalia aliiambia BBC.

"Tumenaswa kati ya utawala katili ambao haujali watu wake na wale wanaoturushia makombora," mwanamke mwingine alituambia.

Anaamini kuwa amri ya rais wa Marekani ya kuhama ilikuwa ni kisingizio tu cha kuhalalisha mauaji ya raia.

Nilikuwa na ujumbe kwa Donald Trump:

"Unamaanisha nini kwa kuhama Tehran, huku ukiwa umekaa nusu ya dunia? Unataka tu kusema 'tulikuambia hivyo' mara tu watakapotuua?"

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi