Kombe la Dunia 2022: Mashabiki wahesabu saa chache kuelekea fainali

Mashabiki waliojawa na furaha nchini Ufaransa na Argentina wanasubiri kwa hamu fainali ya Kombe la Dunia itakayochezwa huko Doha Qatar baadaye hii leo jioni.

Tumu zote mbili zinatarajia kuandikisha histori. Ufaransa inalenga kuwa timu ya tatu kuhifadhi kombe hilo katika historia yake ya miaka 92, ikifuata nyayo za Italia na Brazil.

Kocha wao mkuu Didier Deschamps - ambaye aliongoza Ufaransa kwa ushindi mwaka 1998 - pia anapigania kuwa meneja wa kwanza tangu Vittorio Pozzo wa Italia mwaka 1938 kushinda mataji mfululizo.

Kwa Argentina, matumaini na ndoto za taifa zipo kwenye mabega ya Lionel Messi. Bila shaka ndiye mchezaji bora zaidi kwa muda mrefu, anatumai kutwaa ushindi wa Kombe la Dunia katika kile ambacho mchezaji huyo wa miaka 35 anasema utakuwa mchezo wake wa mwisho kwa nchi yake.

Kombe la Dunia ni usumbufu unaokaribishwa Buenos Aires

Mjini Buenos Aires utadhani furaha ya siku za usoni ya taifa inategemea matokeo ya fainali hii ya Kombe la Dunia.

Argentina ni nchi iliyo katika mzozo mkubwa wa kiuchumi. Kupanda kwa mfumuko wa bei kunamaanisha mamilioni ya watu wannahangaika kustahimili kila mwezi - lakini baada ya Lionel Messi na timu ya Argentina kufika fainali ya Kombe la Dunia kila mmoja hapa sasa ameweka kando wasiwasi wake na badala yake wanaangazia soka.

"Nchi hii imepitia kipindi kigumu sana, kombe linatuunganisha, tunajivunia kuwa na mwanasoka bora wa dunia na anapendwa kila mahali," anasema mmiliki wa baa Luis Sarni.

Zaidi ya Messi, timu nzima inajivunia nchi yake. "Wanasema viwanja vya soka haviteteleki, vina mapigo ya moyo," Luis anasema. "Kila Muargentina anajiona kama kocha, kila mtu ana maoni tofauti, lakini wakati tunaposherehekea, tunalia, tunalia sana - na kukumbatiana!"

Kwa kijana Martin Rojas, Muajentina anayeishi Ufaransa lakini amerejea kwenye likizo ya kutembelea familia, mechi ya Jumapili ina maana kubwa.

"Ni ndoto yangu - tangu nilipozaliwa katika miaka ya 90 sijaona Argentina ikichukua bingwa wa dunia," anasema.

"Bila shaka kwa Messi ni Kombe lake la mwisho la Dunia - ni nafasi nzuri ya mwisho kwake." Na ni nafasi ya Argentina kujivunia nchi yao nzuri, licha ya matatizo yanayowakabili.

Paris yajiamini kuelekea fainali

Mjini Paris msisimko unaelekea kufikia kilele chake. Kwa rekodi hii ni fainali ya nne kwa Ufaransa katika michuano saba ya Kombe la Dunia.

Miongoni mwa takwimu zinazojadiliwa na mashabiki ni kwamba Ufaransa haijashindwa katika mechi zake 10 zilizopita za Kombe la Dunia dhidi ya timu za Amerika Kusini. Kipigo cha mwisho kilikuwa mnamo 1978 - na Argentina.

Hali hii inazua kukumbuka ya maoni yaliyotolewa na mchezaji maarufu Killian Mbappe mapema mwaka huu kuhusu soka ya Amerika Kusini kutokuwa "mbele" kama Ulaya, kwa sababu ya kiwango cha "chini" cha ushindani huko.

Alikuwa akiashiria ukweli kwamba timu ya mwisho ya Amerika Kusini kushinda kombe hilo ilikuwa Brazil mnamo 2002 - na kwamba Argentina haijashinda tangu 1986.

Na pengine pia alikuwa anakumbuka pambano la mwisho la Ufaransa na Argentina - katika hatua ya 16 bora nchini Urusi 2018 - ambayo Ufaransa ilishinda 4-3, Mbappe mwenyewe akifunga mara mbili.

Hoja zotehizi zinafanya Ufaransa kujiamini. Ingawa bila shaka kutoka kwa mtazamo wa Argentina sababu hizo pia zinaweza kuwa chachu yao ya kulipiza kisasi!

Rais Emmanuel Macron na mkewe Brigitte wako njiani kuelekea Qatar kushabikia timu ya taifa ya Ufaransa.

Wataandamana na ujumbe wa wanaspoti, akiwemo mwamuzi Stephanie Frapport ambaye mapema mwezi huu alikua mwanamke wa kwanza kusimamia mechi ya Kombe la Dunia kwa wanaume.

Ni safari ya pili ya rais nchini Qatar katika muda wa siku nne. Akitimiza ahadi aliyotoa mwanzoni mwa shindano hilo, aliungana nao kwa nusu fainali dhidi ya Morocco Jumatano.

Rais Macron amekosolewa na watu wanaojali kuhusu rekodi ya Qatar juu ya haki za binadamu, lakini kwa ujumla inaonekana kwamba jinsi Ufaransa inavyopiga hatua katika michuano hiyo, ndivyo miito ya kususia inavyozidi kufifia.