Nani na nani wapo katika Familia ya Kifalme ya Uingereza na majukumu ya Mfalme ni yapi?

Mfalme Charles III amemrithi mama yake, Malkia Elizabeth II, baada ya kifo chake kilichotokea katika Kasri la Balmoral akiwa na umri wa miaka 96.

Mapema mwaka huu, Malkia alisherehekea Jubilee yake ya Platinum, na kuwa Malkia wa Uingereza aliyetumikia muda mrefu zaidi.

Nini kinatokea sasa?

Wakati Malkia alipofariki, kiti cha enzi kilipitishwa mara moja kwa mrithi wake, Charles, Mkuu wa zamani wa Wales (Prince of Wales)

Inatarajiwa kwamba Charles atatangazwa rasmi kuwa Mfalme siku ya Jumamosi katika Jumba la St James's huko London, mbele ya baraza maalumu la kupitisha mrithi (Accession Council)

Mfalme anafanya nini?

Mfalme ndiye mkuu wa serikali ya Uingereza. Walakini, mamlaka yake ni ya kiishara na matukio ya kitaifa na anakuwa hana upande wowote kisiasa.

Atapokea barua za kila siku kutoka serikalini katika kisanduku chekundu cha ngozi, kama vile muhtasari kabla ya mikutano muhimu au hati zinazohitaji saini yake.

Waziri mkuu kwa kawaida atakutana na Mfalme siku ya Jumatano katika Jumba la Buckingham ili kumjulisha kuhusu maswala ya serikali.

Mikutano hii ni ya faragha kabisa na hakuna rekodi rasmi ya kile kinachosemwa.

Mfalme pia ana kazi kadhaa za Bunge:

  • Kuteua serikali - kiongozi wa chama kilichoshinda uchaguzi mkuu kwa kawaida huitwa kwenye kasri ya Buckingham, ambako wanaalikwa rasmi kuunda serikali. Mfalme pia anavunja rasmi serikali kabla ya uchaguzi mkuu
  • Ufunguzi wa kitaifa na Hotuba ya Mfalme - Mfalme ataanza mwaka wa Bunge na sherehe ya kitaifa ya Ufunguzi. Ataweka wazi mipango ya serikali, katika hotuba inatolewa kutoka katika kiti cha enzi katika nyumba ya Wafalme (House of Lords)
  • Idhini ya Kifalme - wakati kifungu cha sheria kinapitishwa kupitia Bunge, lazima kiidhinishwe rasmi na Mfalme ili iwe sheria. Mara ya mwisho Uidhinishaji wa kiifalme ulikataliwa mnamo 1708

Aidha, Mfalme atakuwa mwenyeji wa wakuu wa nchi wageni na kukutana na mabalozi wa kigeni na makamishna wakuu walioko Uingereza. Kwa kawaida ataongoza hafla ya Ukumbusho ya kila mwaka ya Novemba katika Cenotaph huko London.

Mfalme mpya ni mkuu wa Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya wanachama wa nchi huru 56 na watu bilioni 2.4. Nchi 14 kati ya hizi, zinazojulikana kama mikoa ya Jumuiya ya Madola, yeye pia ni mkuu wa nchi.

Ingawa, tangu Barbados iwe jamhuri mnamo 2021, mataifa kadhaa ya Jumuiya ya Madola ya Karibean yamependekeza wanaweza kufanya vivyo hivyo.

Picha ya Mfalme Charles III itachukua nafasi ya ile ya mama yake kwenye stempu mpya za Royal Mail na noti za Benki Kuu ya Uingereza na maneno ndani ya Pasipoti mpya za Uingereza yatabadilshwa ili kusomeka Ukuu wake.

Wimbo wa taifa utakuwa "Mungu Mwokoe Mfalme".

Namna urithi unavyofanya kazi?

Mpangilio wa urithi unaweka wazi ni nani katika Familia ya Kifalme atachukua kiti kama aliyepo atafariki au kujiuzulu. Wa kwanza katika mstari, mrithi wa kiti cha enzi ni mtoto mkubwa wa mfalme.

Kama mtoto wa kwanza wa Malkia Elizabeth, Charles alivyokuwa Mfalme baada ya kifo cha mama yake, na mkewe, Camilla, atakuwa Malkia.

Sheria za urithi wa kifalme zilirekebishwa mwaka wa 2013 ili kuhakikisha kwamba wanaume hawatachukua tena nafasi ya kwanza mbela ya dada zao wakubwa.

Mrithi wa Mfalme Charles ni mtoto wake mkubwa, Prince William, ambaye anarithi cheo cha baba yeke la Duke wa Cornwall. Ingawa hatakuwa Mkuu wa Wales moja kwa moja

Mtoto mkubwa wa Prince William, Prince George, ni wa pili katika mstari wa kiti cha enzi, na binti yake mkubwa Princess Charlotte ni wa tatu.

Nini kinatokea wakati wa kutawazwa?

Kutawazwa ni sherehe ambayo mfalme anakabidhiwa rasmi taji. Inafanyika baada ya muda wa maombolezo kwa kiongozi aliyetangulia.

Elizabeth II alikua malkia tarehe 6 Februari 1952 baada ya kifo cha babake King George VI, lakini hakutawazwa hadi 2 Juni 1953.

Kutawazwa kwake kulirushwa kwa mara ya kwanza moja kwa moja kwenye TV, na kutazamwa na zaidi ya watu milioni 20.

Kwa miaka 900 iliyopita kutawazwa kumefanyika huko Westminster Abbey William the Conqueror alikuwa mfalme wa kwanza kutawazwa huko, na Charles atakuwa wa 40.

Ni huduma ya kidini ya Kianglikana, inayofanywa na Askofu Mkuu wa Canterbury.

Mfalme hupakwa mafuta "mafuta matakatifu", na hupokea orb na fimbo, ishara za kifalme. Katika kilele cha sherehe hiyo, Askofu Mkuu ataweka Taji la St Edward juu ya kichwa cha Charles - taji thabiti ya dhahabu, tangu 1661.

Hiki ndicho kitovu cha Vito vya Taji kwenye Mnara wa London, na huvaliwa tu na mfalme wakati wa kutawazwa.

Tofauti na harusi za kifalme, kutawazwa ni tukio la serikali - serikali hulipia, na hatimaye huamua orodha ya wageni.

Nani mwingine yuko katika Familia ya Kifalme?

  • Duke wa Cornwall na Cambridge (Prince William) ni mtoto mkubwa wa kiume wa Mfalme Charles na mke wake wa kwanza, Diana, Princess wa Wales. Amemuoa Duchess wa Cornwall na Cambridge (Catherine). Wana watoto watatu: Prince George, Princess Charlotte na Prince Louis
  • Binti Mfalme (Princess Anne) alikuwa mtoto wa pili na binti pekee wa Malkia. Ameolewa na Adm Timothy Laurence. Ana watoto wawili na mume wake wa kwanza, Kapteni Mark Phillips: Peter Phillips na Zara Tindall
  • The Earl of Wessex (Prince Edward) alikuwa mtoto wa mwisho wa Malkia. Amemuoa Countess wa Wessex (Sophie Rhys-Jones). Wana watoto wawili: Louise na James Mountbatten-Windsor
  • Duke wa York (Prince Andrew) alikuwa mtoto wa pili wa Malkia. Ana binti wawili na mke wake wa zamani, Duchess wa York (Sarah Ferguson): Princess Beatrice na Princess Eugenie. Prince Andrew alijiuzulu kufanya "kazi za Kifalme" mnamo 2019 baada ya mahojiano yenye utata ya Newsnight kuhusu madai kwamba alimnyanyasa kingono Virginia Giuffre. Mnamo Februari 2022, alilipa kiasi ambacho hakikujulikana ili kutatua kesi ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo Bi Guiffre aliibua dhidi yake nchini Marekani.
  • Duke wa Sussex (Prince Harry) ni kaka mdogo wa William. Amemuoa Duchess wa Sussex (Meghan Markle). Wana watoto wawili: Archie na Lilibet. Mnamo 2020, walitangaza kuwa wanaachia majukumu makuu ya kifalme na kuhamia Marekani

Wanafamilia ya Kifalme wanaishi wapi?

Mfalme Charles na Malkia wanatarajiwa kuhamia Buckingham Palace. Hapo awali waliishi Clarence House huko London na Highgrove huko Gloucestershire.

Prince William na Catherine, Duchess of Cornwall na Cambridge hivi karibuni walihama kutoka Kensington Palace magharibi mwa London na kuishi Adelaide Cottage, kwenye jumba la malkia la Windsor Estate.

Prince George, Princess Charlotte na Prince Louis huenda kwenye Shule ya Lambrook, karibu na Ascot huko Berkshire.

Prince Harry na Meghan Markle wanaishi California.

Utawala wa kifalme una umaarufu gani?

Kura iliyofanywa na YouGov wakati wa Jubilee ya Platinum ilipendekeza kuwa 62% wanafikiri nchi inapaswa kubaki na utawala wa kifalme, huku 22% wakisema inapaswa kuwa na mkuu wa nchi aliyechaguliwa badala yake.

Kura mbili za Ipsos Mori mnamo 2021 zilitoa matokeo sawa, huku mmoja kati ya watano akiamini kuwa kukomesha ufalme huo kungefaa kwa Uingereza.

Walakini, matokeo ya YouGov yalionyesha kuwa kumekuwa na kupungua kwa kukubalika kwa ufalme katika muongo mmoja uliopita, kutoka 75% mnamo 2012, hadi 62% mnamo 2022.

Ingawa kulikuwa na uungwaji mkono mkubwa kwa utawala wa kifalme miongoni mwa vikundi vya wazee, kura ya maoni ilionyesha kuwa hii inaweza kuwa si kweli kwa vijana.

Mnamo 2011, wakati YouGov ilipoanza kufuatilia suala hilo kwa mara ya kwanza, 59% ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24 walidhani ufalme unapaswa kuendelea, ikilinganishwa na 33% mnamo 2022.