Ni kwanini Twitter imeweka ukomo wa idadi ya jumbe unazoweza kuona?

Chanzo cha picha, Reuters
Elon Musk alituma ujumbe wa Twitter kwamba watumiaji ambao hawajathibitishwa wanaweza kusoma jumbe za Twitter 1,000, na watumiaji waliothibitishwa 10,000 kwa siku.
Watu walianza kushiriki skrini za jumbe ambazo "wamezidisha" idadi yao ya kila siku ya jumbe za Twitter.
Elon Musk alikuwa akifanya jambo ambalo linaonekana kutoeleweka kwa kampuni ya mitandao ya kijamii - alikuwa akizuia shughuli za watumiaji.
Hatua hiyo imewashangaza watendaji wakuu wa matangazo ya kiibiashara.
Hata hivyo hii ni sehemu ya mchezo mrefu zaidi ambao Elon Musk anacheza - vita na makampuni ya akili bandia (AI).
Hebu kwanza tuanze na jinsi Twitter inavyotengeneza pesa. Sehemu kubwa ya mapato yake hutokana kwa utangazaji wa biashara, kama vile Meta na Google.
Watumiaji wanapoingia kwenye jukwaa, wanaonyeshwa matangazo. Kadiri wanavyotumia muda mwingi kwenye Twitter, ndivyo wanavyoona matangazo mengi. Mahesabu ni rahisi sana. Hiyo ndiyo biashara.

Lakini , Elon Musk kijadi amekuwa akikwepa matangazo ya kibiashara. Tesla ambayo ni kampuni yake maarufu hafanyi matangazo ya kiashara.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo 2019 alituma ujumbe wake wa twitter akisema "Nachukia matangazo ya biashara".
Na bado amenunua kampuni inayoitegemea kabisa.
Kwa hivyo, Elon Musk anatamani sana kutoa njia tofauti za mapato.
Huu sio uamuzi wa biashara tu. Anaamini kuwa watangazaji wana nguvu nyingi juu ya kampuni za mitandao ya kijamii linapokuja suala la kudhibiti.
Watangazaji wanaweza, na wamechota pesa zao kutoka Twitter.
Watangazaji hawataki matangazo yao kuwekwa karibu na maudhui ya ubaguzi wa rangi au itikadi kali. Na kwa hivyo mkondo mkuu wa mapato wa Twitter pia una ushawishi juu ya ni kiasi gani cha "uhuru wa kujieleza" kinaruhusiwa kwenye jukwaa.
Bw Musk aliniambia mnamo Aprili kwamba "wengi" wa watangazaji wa matangazo ya biashara walikuwa wamerejea baada ya awali kusitisha matangazo yao kutoka kwa Twitter baada ya kuchukuliwa na yeye.
Hata hivyo Bw Musk ana mpango mwingine wa kuigeuza Twitter kuwa kampuni ya faida.
Anataka Twitter ipate pesa kutokana na idadi kubwa ya data iliyo nayo.
Majukwaa kama Twitter na Reddit hushikilia hazina ya mamia ya mabilioni ya mazungumzo halisi ya kibinadamu ambayo ni rasilimali kubwa kwa makampuni ya Akili bandia (AI).

Chanzo cha picha, Getty Images
Inawezekana kujifunza miundo mikubwa ya lugha (LLMs), kwa mawasiliano haya kutafuta jinsi ya kujibu maswali kwa njia zaidi kama za kibinadamu.
Lakini majukwaa kama Twitter na Reddit yanataka kulipwa kwa matumizi ya data zao kwa njia hii.
Mnamo Aprili, mtendaji mkuu wa Reddit Steve Huffman aliliambia gazeti la New York Times kwamba hakufurahishwa na kile ambacho kampuni za AI zilikuwa zinakifanya.
"Data ya Reddit corpus ni ya thamani sana," alisema. "Lakini hatuhitaji kutoa thamani hiyo yote kwa baadhi ya makampuni makubwa duniani bila malipo."
Wakati huohuo, Elon Musk alisema kwamba Microsoft ilikuwa "ikiondoa hifadhidata ya Twitter , kuiingiza kwenye mapato (kuondoa matangazo ya kibiashara) na kisha kuuza data zetu kwa wengine".
Siku ya Jumamosi ilikuwa wazi jinsi Bw Musk alivyokuwa akifadhaika.
"Tulikuwa tukiibiwa data," alisema.
"Takriban kila kampuni ya Akili Bandia, kuanzia iliyoanzishwa hadi mashirika makubwa zaidi Duniani, ilikuwa ikifuta data nyingi," alisema.
Na kwa hivyo, kwa kuzuia matumizi, Elon Musk anatumai kuzuia data yake kuvutwa kwenye LLMs. Anataka kujadiliana na makampuni ya Akili Bandia na kulipwa kwa maudhui ambayo wanayachukua.
Twitter ina nakili Meta?
Lakini kunaweza kuwa na sababu zingine zinazohusika pia, na inarudi kwa jaribio lingine la kupunguza utegemezi wa Twitter kwenye mapato ya utangazaji wa kibiashara.
Bw Musk anatamani sana watu wailipie Twitter.
Kwa miezi kadhaa, amekuwa akijaribu kusukuma watu kuelekea Twitter Bluu. Kumekuwa na karoti, inayowapa watumiaji wa Twitter alama ya tiki ya bluu na uthibitishaji wa uanachama wao, na fimbo fulani – ikiashiria kuondoa uthibitishaji kutoka kwa watumiaji ambao hawalipi.
Lakini Twitter Blue haijawa vile Elon Musk alitarajia. Watu hawalipi katika makundi yao.
Labda anaangalia njia nyingine ya kuwafanya watumiaji wafungue pochi zao. Katika siku zijazo, ikiwa unataka ufikiaji wa jumbe za Twitter bila kikomo, labda utalazimika kulipa ada ya kila mwezi?
Chochote ambacho Bw Musk anafikiria, jambo moja ni wazi ingawa, kuzuia jumbe za Twitter sio vizuri kwa watangazaji wa biashara kwenye jukwaa hilo la kijamii.
Mipaka ni "mibaya sana" kwa watumiaji na watangazaji ambao tayari wametikiswa na "machafuko" kwenye Twitter, Mike Proulx, mkurugenzi wa utafiti wa Forrester, aliiambia Reuters.
Mark Zuckerberg anaripotiwa kuzindua mtandao wa Twitter, unaoitwa Threads, wakati fulani majira ya joto.
Elon Musk ni mfanyabiashara aliyefanikiwa sana, na ana wasiwasi wa kweli linapokuja katika suala la kampuni za Akili Bandia (AI) kuchukua data zake. Lakini matukio ya wikendi hii yamekuwa ya kuumiza kichwa.
Hivi majuzi amemuajiri Linda Yaccarino kuwa mtendaji mkuu wa Twitter. Yeye ni mtendaji wa zamani wa utangazaji.
Inasemekana ana mawazo mazuri kuhusu jinsi Twitter inavyoweza kutengeneza pesa zaidi - ikiwa ni pamoja na matangazo ya video ya skrini nzima na kujaribu kuwashawishi watu mashuhuri zaidi kutumia programu.
Kazi yake inafanywa kuwa ngumu zaidi kwa kuwa na vikwazo vya ukomo wa jumbe za Twitter. Macho machache kwenye machapisho inamaanisha kuwa watangazaji wa biashara hawatavutiwa sana katika utumiaji wa pesa zao- kwenye mtandao huo . Na kisha kuna Meta.
















