Jinsi Akili Mnemba ilivyowasaidia wagonjwa wa saratani kuona maisha yajayo ambayo wanaweza wasifikie

Yeyote anayeishi na ugonjwa usiotibika hukabili uchungu wa kuogopa kukosa nyakati zenye thamani za wakati ujao pamoja na familia yake.

Kuanzia kuhudhuria harusi ya mtoto hadi kuchukua likizo maalum, watu 10 wanaoishi na saratani ya matiti ya pili wameweza kutazama siku zijazo wanazojua wanaweza kutoishi kuona kwa macho yao wenyewe.

Kwa kutumia akili mnemba na picha zilizopigwa na mpiga picha mashuhuri Jillian Edelstein , picha hizi ziliunda "Nyumba ya Matumaini", maonesho yanayooneshwa hifadhi ya kumbukumbu ya Saatchi huko London.

Louise Hudson, kutoka Monmouthshire, kusini-mashariki mwa Wales, ni mmoja wa watu walioshiriki katika tukio hili.

Sasa akiwa na umri wa miaka 58, aligunduliwa na saratani ya matiti kwa mara ya kwanza mnamo Julai 2022, ambayo baadaye ilienea kwenye ini lake.

Mnamo Februari, MRI ilionesha vidonda kwenye ubongo wake na aliambiwa alikuwa na umri wa kuishi wa takribani miezi sita.

Picha hiyo inamuonesha akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 60, akitumbuiza na kampuni yake ya densi ya amateur Chelsea Ballet, huku mume wake ambaye wamekuwa pamoja kwa miaka 30, Barry, akitazama kwa fahari.

Kuiona kwa mara ya kwanza ilikuwa inaeleweka... kihisia kali sana.

"Picha hiyo ilikuwa ya kushangaza ... ilikuwa nzuri tu," anasema Louise.

Wengine wanaweza kudhani kuwa kujiona katika siku zijazo ambapo huna uwezekano wa kufanikiwa kunaweza kuhuzunisha sana, lakini Louise anasema uzoefu huu ulikuwa wa kusisimua zaidi.

"Kuna aina hiyo ya [kufikiria], 'Nataka sana kuifanya,' lakini watu wengi wanasema kwamba kwa mtazamo wangu mzuri hakuna sababu kwa nini siwezi, kwa hivyo niko tu. kuipokea kila siku inavyokuja," anasema.

Watu wengine waliopigwa picha kwa ajili ya onesho hilo pia walichagua kujiona na wapendwa wao katika hali ambayo wanahofia hawatafikia.

Picha za Katie Enell zinamuonesha akiwa na mwenzi wake, Liam, siku ya harusi yao mnamo 2025.

Katie, 31, ana mtoto wa kiume wa miaka minane, Theo, anaishi Liverpool. Aligunduliwa na saratani ya matiti ya pili baada ya kusumbuliwa na maumivu ya mara kwa mara ya bega.

Unapokea matibabu kadhaa tofauti ili kuzuia saratani kuenea.

Picha ya Oge Onwuachu (pichani juu ya hadithi hii) inamuonesha siku ya kuhitimu kwa mwanawe mnamo 2025, ambapo "nisingeweza kujivunia zaidi kusimama karibu na watoto wangu mahiri."

Oge, ambaye anaishi katika kaunti ya Kent kusini-mashariki mwa Uingereza na anafanya kazi kama mwalimu, aligundua uvimbe kwa mara ya kwanza mnamo Februari 2019, lakini haikuwa hadi alipomuona daktari kwa mara ya pili miezi 10 baadaye ndipo aliambiwa kuwa alikuwa na saratani ambayo tayari ilikuwa imeenea.

Amekuwa akipata sindano mfululizo katika kipindi cha miaka minne, na kumruhusu kuishi maisha ya furaha na yenye matokeo.

Picha ya Helena Awuakye inamuonesha siku ya harusi ya mwanawe Josh mwaka 2030.

"Singeweza kujivunia zaidi kuwa naye, sisi wawili tu, kabla ya sherehe kuanza," anasema.

Helena, daktari wa meno anayeishi Newport, Wales, ni shabiki wa mazoezi ya viungo.

Kabla ya uchunguzi wake wa pili wa saratani ya matiti mnamo 2021, alikimbia nusu marathoni na anaamini kabisa kwamba kujitolea kwake kukaa sawa kumemsaidia katika matibabu yake.

Bec Brown, 46, alichagua kukutana na binti zake kwenye sherehe yake ya miaka 50 mnamo 2028.

Mshairi huyo anaishi Hertfordshire, mashariki mwa Uingereza, pamoja na mumewe na binti zake wawili.

Kwa mara ya kwanza aliona uvimbe alipokuwa akinyonyesha na aligunduliwa na saratani ya matiti katika hatua za awali mnamo 2021.

Miezi tisa baadaye, baada ya tiba ya mionzi na mastectomy, aliambiwa kwamba sartani ilikuwa imeenea kwenye mifupa yake.

Simon Vincent, kutoka shirika la hisani la Saratani ya Matiti Sasa, anatumai onyesho hilo litaangazia kwamba utafiti zaidi ni muhimu kwa watu wanaokadiriwa kuwa 61,000 nchini Uingereza wanaoishi na saratani katika hatua ya pili.

"Kwa watu wanaoishi na saratani ya matiti ya hatua ya pili, matarajio ya kukosa nyakati za thamani katika siku zijazo ni ya kufadhaisha," anaelezea.

"Maonesho haya yanaonesha ni kiasi gani bado kinapaswa kufanywa ... ili watu walio na ugonjwa huu waishi ili kuona wakati ujao ambao ni muhimu sana kwao."

Kwa Louise, tukio hilo limekuwa moja ambalo anashikilia kati ya kumbukumbu zake nzuri zaidi.

"Nimekutana na wanawake wengine wa kutia moyo katika hali kama yangu; Nyumba ya sanaa ya Matumaini labda ilikuwa jambo la kushangaza zaidi ambalo nimewahi kufanya," anasema.

Anaendelea kubaki na shughuli nyingi; Mbali na kuandaa mazishi yake, pia amepanga kufanya upya viapo vyake vya harusi na Barry mbele ya marafiki na familia 200 mwezi Agosti.

Kisha, mnamo Septemba, anataka kuwa na karamu kubwa: "kuamka hai."

"Ninaweza kuwa na saratani, lakini nina wakati wa mzuri wa maisha yangu," anasema.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga