Sikuwa na budi ila kurudi- Mwanafunzi wa Kitanzania anayesomea Ukraine

    • Author, Esther Kahumbi
    • Nafasi, BBC News

“Nitarudia nini?”

Septemba iliyopita, Haifa Juma, mwanafunzi wa chuo kikuu kutoka Tanzania alijiuliza swali hili mara kwa mara.

Licha ya hofu yake, mwanafunzi huyo wa matibabu mwenye umri wa miaka 23 alifanya uamuzi mgumu wa kurejea Ukraine inayokumbwa na vita ili kumaliza shahada yake.

“Sikuwa na budi. Ingawa nilikuwa na shaka…. Tuliona kwenye habari mapigano bado yanaendelea. Kwa hivyo, sikuwa na uhakika nitapata nini, "anasema.

Mwezi huu ni miaka miwili tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. Tangu Februari 2022, zaidi ya vifo 30,000 vya raia vimeripotiwa, kulingana na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine idadi ya vifo vinaweza kuwa juu zaidi.

Mzozo huo umesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao, kuharibu miji na maeneo yaliyo kuharibu miundombinu muhimu.

Sawa na wanafunzi wengi wa kigeni, Haifa alikuwa na hofu vita vilipozuka hivyo akatorokea mpakani na kuingia Hungary.

Ilichukua miezi kadhaa kuishawishi familia yake nchini Tanzania kukubaliana na uamuzi wake wa kurejea Ukraine.

"Nimekuwa nikifanya masomo yangu mtandaoni kutoka Tanzania, na nilimaliza katika awamu ya kwanza. Ili kuhitimu, ilinibidi niwepo shuleni kwa mazoezi ya vitendo,” asema.

"Familia yangu tayari ilikuwa imetumia pesa nyingi sana kwa ajili yangu. Na sikuweza kukaa bila kufanya chochote, nikisubiri vita kuisha.”

Haifa sasa yuko katika mwaka wake wa nne wa shahada ya matibabu katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Sumy kaskazini-mashariki mwa Ukraine. Anatarajiwa kuhitimu mwaka wa 2027 na anatarajia kuwa daktari aliyebobea katika magonjwa ya wanawake.

Kituo cha Elimu ya Kimataifa cha Ukraine (USCIE) kinasema hakina data sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi wa Kiafrika ambao wamerejea masomoni.

Kabla ya vita, kulikuwa na wanafunzi 16,000 wa Kiafrika waliokuwa wakisoma nchini Ukraine.

Hivi sasa, kuna karibu wanafunzi 5,500 wa Kiafrika waliosajiliwa katika vyuo vikuu vya Ukraine, kulingana na takwimu kutoka Hifadhidata ya Kielektroniki ya Elimu ya juu. Kati ya hao, wanafunzi 3,950 wanatoka Morocco na Nigeria huku Tanzania ikiwa na wanafunzi 49 waliosajiliwa.

"Uamuzi wa kurudi kusoma Ukraine unafanywa na kila mwanafunzi kibinafsi. Vyuo vikuu vinahakikisha kuwa vyuo vikuu vina vifaa vya kujikinga na mabomu, na kwamba masomo ya mtandaoni na ya mseto ni ya ubora wa juu” msemaji wa USCIE alisema katika taarifa ya BBC.

Kwa Haifa, katika kitivo chuo kikuu cha Sumy, "kwa sasa tunafanya masomo ya mtandaoni pekee. Chuo kikuu kinasema masomo ya ana kwa ana yataanza hivi karibuni, kwani wanafunzi wengi wanatarajiwa kurejea."

USCIE inasema mzozo unavyoendelea kuna uwezekano muundo wa masomo utaendelea kubadilika kwa wanafunzi wa elimu ya juu, na ni juu ya vyuo vikuu binafsi na wanafunzi wao kuchagua kinachofaa.

"Taasisi zote za elimu ya juu zimehamishwa kutoka mikoa inayokaliwa kwa muda hadi miji salama katika eneo la kati na magharibi mwa Ukraine" msemaji wa USCIE alisema.

Elimu mseto

Tofauti na Haifa, kurejea Ukraine hakujawa chaguo kwa baadhi ya wanafunzi wa Kiafrika.

Wakati mzozo ulipozuka nchini Ukraine, kulikuwa na wanafunzi 16,000 kutoka nchi za Afrika waliokuwa wakisoma katika vyuo vikuu nchini kote.

Inaaminika karibu 10,000 kati yao walikimbia Ukraine. Wengi wanasitasita kurejea nchini humo.

Wakati baadhi ya wanafunzi wa Kiafrika walirudi katika nchi zao za asili, idadi fulani ilihamia Ulaya - huko Uholanzi, Ureno na Finland - ambapo waliweza kuhamisha kozi zao kwa vyuo vikuu vya ndani.

Lakini miaka miwili baadaye, Maelekezo ya Ulinzi ya Muda ya Umoja wa Ulaya - kifungu kilichowaruhusu kusoma - inakwisha muda wake.

Nchini Uholanzi hii ina maana kwamba baada ya Machi 4, wanafunzi wa Kiafrika watahitaji visa ya elimu ili kuendelea na masomo yao, kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Haki na Usalama ya Uholanzi.

Hili ni jambo la kusikitisha kwa Aisha, mmoja wa watu 17 wanaofahamika kama ‘raia wa nchi ya tatu’ ambao waliandikishwa katika vyuo vikuu nchini Uholanzi.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 25 pia ni mwanafunzi wa matibabu na yuko katika muhula wa mwisho wa shahada yake.

Ikiwa Aisha hatapewa visa ya mwanafunzi, anaweza kurejea Nigeria ambako anasema hawezi kuendelea na shahada yake.

Aisha anasema anahofia kupoteza kila kitu, kwa sababu hayuko tayari kurudi kwenye eneo la vita.

“Unataka twende wapi? Huwezi kutuambia turudi Ukraine ambako watu wanakufa,” anasema Aisha, ambaye hataki kufichua jina lake kamili kwa sababu za kibinafsi.

"Ninafuatilia kile kinachoendelea nchini Ukraine," anasema.

“Lazima, nitilie maanani uslama wangu. Ninawasikitikia Waukraine, lakini hali ni inasikitisha zaidi kwetu sisi ‘raia wa nchi ya tatu’ - Waholanzi hawatujali ingawa tunafanya kazi na kulipa kodi.

Wanatutendea kama watu wa chini kuliko wanadamu. Kwa nini tutendewe hivi, wakati tulipitia vita vile vile?” anauliza.

Wizara ya Sheria na Usalama ya Uholanzi inasema wanafunzi kama Aisha watakuwa na hadi siku 28 baada ya tarehe ya mwisho ya Machi kuondoka nchini humo.

"Wengi wa 'raia wa nchi ya tatu' waliokimbia Ukraine wanaweza, kimsingi, kurudi katika nchi yao ya asili. Iwapo raia wa nchi ya tatu anaogopa ghasia au kufunguliwa mashtaka katika nchi yake ya asili, anaweza kuomba hifadhi hapa,” wizara ilisema katika taarifa kwa BBC.

Derdelanders, shirika la Uholanzi lililoundwa kutetea haki za raia wa nchi ya tatu, limekuwa likifanya kampeni ili wanafunzi hao waruhusiwe muda zaidi wa kumaliza masomo yao.

"Usaidizi wa kibinadamu unapaswa kuwa wa huruma na kuonyesha huruma na kuelewa kwamba hawa ni binadamu, bila kujali asili," anasema Isaac Awodola ambaye anaongoza kundi la Derdelanders.

"Haipaswi kujali kama wanatoka kusini mwa ulimwengu, hawa ni watu ambao walikumbana na shida nyingi kuondoka Ukraine."

Analinganisha hali ya raia wa nchi ya tatu na wanafunzi 400 wa Ukraine ambao wana nafasi ya kusalia Uholanzi kusoma hadi Machi 2025.

Baadhi ya nchi za Kiafrika zimeshughulikia tatizo hilo kwa kuweka mipango ya kusoma nje ya Ukraine. Ghana imekubali kuwahamisha wanafunzi wake wa udaktari hadi Grenada kumaliza shahada zao.

Makubaliano hayo yalitangazwa mara baada ya vita kuzuka na yanajumuisha wanafunzi 200. Hungary pia ilitoa ofa kama hiyo ili kuwachukua wanafunzi wa Ghana ambao walikuwa wakisoma Ukraine.

Lakini, idadi kubwa ya wanafunzi wa Kiafrika waliokimbia wamelazimika kutafuta njia mbadala za kumaliza masomo yao, au kuacha tu masomo yao na kurudi nyumbani kutafuta kazi.

Ingawa hali katika mji wa Ukraine ambako Haifa inasoma sasa ni shwari, anasema ana wasiwasi mara kwa mara kwamba mapigano yatamlazimisha yeye na wanafunzi wengine kutoroka tena.

"Tulisafiri hadi Kyiv mnamo Februari kufanya mtihani wetu wa kitaifa, na kulikuwa na mlipuko mbele ya jengo letu.

Wakati huo nilikuwa nimeanza kutulia, nikifikiri hali inazidi kuwa nzuri,” anasema.

"Lakini baada ya kuona mlipuko huo ulivyokuwa wa kutisha, sasa nadhani huenda ikachukua muda hali kurejelea kuwa ya kawaida. Natumai mambo yatakuwa shwari hivi karibuni."

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi