Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka miwili ya uvamizi wa Urusi, Waukraine waliochoka wamekataa kukata tamaa
Inatafsiriwa kama "pembe potovu", lakini Rais Zelensky anauita Kryvyi Rih "roho yake kubwa na moyo".
Anaushukuru mji huu mgumu, wa viwanda kwa kuunda tabia yake. Alikulia katika eneo lenye vyumba vingi vinavyojulikana kama Anthill.
Unaposimama mbele ya jengo hili refu, safari ya Volodymyr Zelensky kutoka eneo hili hadi kiongozi wa wakati wa vita inashangaza.
"Nataka vita iishe hivi karibuni," anasema Vita, ambaye aliishi karibu na wazazi wa Zelensky. "Ni mtu wa kawaida, mzuri anayepigania watu. Nataka tu vita hivi na ving'ora viishe mapema."
Lakini kwa maendeleo madogo ya Ukraine na kuongezeka kwa utawala wa Urusi, hakuna mwisho unaoonekana, na hiyo inachochewa na mifuko ya nchi za Magharibi.
Katika Mkutano wa Usalama wa Munich hivi majuzi, Rais Zelensky aliwaambia wajumbe wasiulize Ukraine ni lini vita hivyo vitaisha, lakini badala yake "waulize kwa nini Putin bado anaweza kuviendeleza".
Huku msaada wa kijeshi uliozuiwa sasa ukiathiri moja kwa moja vikosi vyake kwenye mstari wa mbele, ilikuwa ni swali kwa wale wanaochelewesha risasi na silaha ambazo askari wake wanazihitaji sana.
"Mimi si mwanasiasa," anakiri Valeriy, mwanamume mwenye umri wa miaka 80 aliyeketi nje ya duka la mboga. "Hatuwezi kuuliza ni lini vita vitaisha.
"Lazima tupigane; hatutavumilia kitu kingine chochote. Watu wana hasira sana sasa."
Hamu hiyo ya kutetea imesalia sawa tangu asubuhi hiyo tarehe 24 Februari 2022. Katika hali isiyojulikana ya kutisha, watu walijitolea kwa maelfu kujiunga na vita vya Ukraine.
Macho ya ulimwengu yakageukia Kyiv, kutoka ambapo nilikuwa nikiripoti.
Wasifu na umaarufu wa Rais Zelensky ulienda kwa kiwango kikubwa alipokataa ofa za kuondoka na kubaki Kyiv.
"Ninahitaji risasi, sio safari," alisema katika nukuu iliyopta umaarufu.
Mahitaji yake hayajabadilika, lakini maombi yake yamepoteza mvuto.
Mashambulizi yaliyoshindwa mwaka wa 2023 yalisababisha maswali yasiyofurahisha kuhusu iwapo Ukraine ina uwezo wa kukomboa ardhi yake.
Wale wenye shaka wa chama cha Republican nchini Marekani wanazuia uwezo wa Ukraine wa kupigana kwa kuzuia msaada wa kijeshi wenye thamani ya mabilioni ya dola. Kyiv inasema wanajeshi zaidi walio mstari wa mbele wanakufa kutokana na uhaba wa silaha na risasi zinazopungua.
Wakati wote huo, Urusi imesalia kwenye mkondo wa vita, na washirika wake Korea Kaskazini na Iran wanasambaza makombora zaidi yanayovurumishwa katika miji ya Ukraine.
Kryvyi Rih hana kinga dhidi ya uchovu unaohisiwa na sehemu kubwa ya nchi. Wengine wametosheka na vita hivi, wanaume wengi wanaogopa kuandikishwa, na bado wanasema mzozo bado ni mapambano ya kuishi.
Wazo la maelewano au makubaliano kwa Urusi linatazamwa kama kushindwa.
Mara ya mwisho nilipoona watoto wakicheza ilikuwa katika shule karibu na gorofa yangu huko Kyiv, kabla ya uvamizi. Sasa ni mahame yaliyoharibiwa na makombora.
Ujana usio na hatia ulibadilishwa na mifuko ya miili na uharibifu.
Huko Kryvyi Rih, tunakutana na Yuriy mwenye machozi anapotazama gorofa yake ikibomolewa baada ya shambulio la kombora mwaka jana. Mitindo kwenye ukutanda inafichua maisha tofauti yaliyoharibiwa.
"Hakuna anayehitaji vita hivi, ni vya nini hata hivyo?" anauliza. "Watu wengi wanauawa."
Kwa hivyo, anafikiri Ukraine inapaswa kubadilishana eneo kwa amani?
"Hapana," anajibu kwa ukali. "Watu wengi walikufa kwa ajili ya maeneo hayo. Hakuna maana ya kufa moyo."
Ukosefu wa maendeleo kwenye uwanja wa vita ulisababisha mgawanyiko kati ya Rais Zelensky na mkuu wa jeshi lake Valerii Zaluzhnyi. Sasa akiwa amefukuzwa kazi, Jenerali Zaluzhnyi anaonekana kama mpinzani wa kisiasa wa bosi wake wa zamani.
Karibu Kryvyi Rih, Waukraine wanajaribu kusaidia ambapo washirika wa nchi yao hawawezi. Katika jengo moja lisiloonekana, jeshi linaloongezeka la watu wa kujitolea hushona nyavu za kujificha kwa wanajeshi walio mstari wa mbele.
Wanaume na wanawake wanawekwa tofauti kwa sababu ya " tofauti ya vicheshi vyao ," anaelezea mratibu.
Katika mrengo mwingine wa kiviwanda wa jiji, kilabu cha zamani cha baiskeli kimebadilisha baiskeli na moshi. Timu hii huchanganya kemikali katika mikebe ambayo itakuwa mabomu ya moshi. Kifaa muhimu cha kijeshi ikiwa unajaribu kushambulia, au kuwahamisha waliojeruhiwa.
“Haiwezekani kubaki nyumbani na mawazo yangu wakati mume wangu anapigana,” aeleza Ines, mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea. "Hapa nahisi ninaweza kufanya kitu ili iwe rahisi kwao."
Muongo wa uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine ulianza na kunyakuliwa kwa Crimea mnamo 2014 na kisha kusambaa katika vita kali mashariki mwa nchi hiyo. Katika siku ya 731 ya uvamizi kamili, ni aina tofauti ya vita.
Mafanikio ya Ukraine katika ulinzi na kudhalilisha jeshi la wanamaji la Urusi hayajabadilisha wimbi kwa upande wake.
Riwaya ya vita hivi imepita. Ukraine, Kryvyi Rih na mtoto wake maarufu watahitaji kupata akiba mpya za nguvu na werevu ili kufanya ulimwengu ushiriki.
Imetafsiriwa na Jason nyakundi na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi