Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Japan, nchi ambayo nepi nyingi za watu wazima zinanunuliwa kuliko nepi za watoto
Kampuni ya kutengeneza nepi za Kijapani imetangaza kuacha kuzalisha nepi za watoto nchini na kulenga soko la watu wazima.
Oji Holdings ni mojawapo ya kampuni za hivi karibuni kufanya uamuzi huu katika Japani inayozeeka, ambapo kiwango cha uzazi ni cha chini kihistoria.
Mauzo ya nepi za watu wazima yamepita yale ya watoto wachanga nchini kwa zaidi ya muongo mmoja.
Idadi ya watoto waliozaliwa nchini Japani mwaka 2023 ilikuwa 758,631, ikiwa ni upungufu wa 5.1% kutoka mwaka uliopita.
Pia ni idadi ndogo zaidi ya watoto waliozaliwa Japan tangu karne ya 19.
Kufikia miaka ya 1970, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi zaidi ya milioni mbili.
Katika taarifa, Oji Holdings ilisema kampuni yake tanzu, Oji Nepia, kwa sasa inatengeneza nepi za watoto milioni 400 kwa mwaka.
Uzalishaji umekuwa ukipungua tangu 2001, wakati kampuni ilifikia kilele cha nepi milioni 700.
Wakati huo huo, soko la nepi za watu wazima linakua na inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola bilioni 2.
Mnamo mwaka wa 2011, mtengenezaji mkuu wa nepi nchini Japan, Unicharm, alisema mauzo yake ya nepi za watu wazima yamepita yale ya watoto wachanga.
Japani sasa ina mojawapo ya wakazi vikongwe zaidi duniani, ikiwa na karibu 30% wenye umri wa miaka 65 au zaidi. Mwaka jana, idadi ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 80 ilizidi 10% kwa mara ya kwanza.
Oji Holdings pia ilisema itaendelea kutengeneza nepi za watoto nchini Malaysia na Indonesia, ambapo inatarajia mahitaji kuongezeka.
Si Wajapani tu
Kupungua kwa idadi ya watu, kutokana na kuzeeka na kushuka kwa viwango vya kuzaliwa, kumekuwa shida kwa Japan, moja ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni. Lakini juhudi za serikali ya Japan kukabiliana na changamoto hizo zimepata mafanikio madogo hadi sasa.
Ongezeko la matumizi katika programu na ruzuku zinazohusiana na watoto kwa wanandoa au wazazi wachanga halionekani kuongeza viwango vya kuzaliwa.
Wataalamu wanasema sababu ni tata na ni tofauti na kushuka kwa viwango vya ndoa, wanawake wengi katika nguvu kazi na kupanda kwa gharama za kulea watoto.
"Japani iko katika hatihati ya kujua kama tunaweza kuendelea kufanya kazi kama jamii," Waziri Mkuu Fumio Kishidaa alisema mwaka jana. Aliongeza kuwa lilikuwa swali la "sasa au kamwe".
Lakini Japan haiko peke yake. Viwango vya uzazi pia vinashuka katika Hong Kong, Singapore, Taiwan na Korea Kusini, nchi ya mwisho yenye kiwango cha chini zaidi cha kuzaliwa duniani.
China pia ilishuhudia idadi ya watu ikipungua kwa mwaka wa pili mfululizo mnamo 2023 na, kama Japan, imetekeleza motisha kadhaa ili kuongeza viwango vya kuzaliwa.
Lakini idadi ya watu wanaozeeka na athari za sera ya miongo kadhaa ya mtoto mmoja iliyomalizika mwaka wa 2015 pia inaleta changamoto za idadi ya watu nchini China.
Kubadilisha sera ya mtoto mmoja
Kwa upande wa serikali ya China imekuwa ikitoa punguzo la kodi na huduma bora za afya ya uzazi tangu ilipotupilia mbali sera yake yenye utata ya kuwa na mtoto mmoja mwaka 2016 na kuruhusu wanandoa kupata watoto wawili.
Rais wa China Xi Jinping aliweka kipaumbele katika kuongeza viwango vya kuzaliwa mnamo Novemba 2022, lakini kuviinua kumeonekana kuwa vigumu zaidi kuliko kuvipunguza.
Idadi ya watu nchini China ilipungua kwa mara ya kwanza katika miongo sita mwaka 2023, na watoto 6.77 pekee kwa kila watu 1,000.
Xi Jinping aliahidi kuwa serikali yake "itafuata mkakati madhubuti wa kitaifa" katika kukabiliana na watu wanaozeeka nchini humo.
Lakini siku zijazo hazionekani kuwa nzuri, kulingana na makadirio ya UN, idadi ya Wachina wenye umri wa miaka 15 na 64 itapungua kwa zaidi ya 60% karne hii.
Inahofiwa kuwa wafanyakazi wanaozeeka wanaweza kuathiri uchumi mkubwa wa Uchina, na kupunguza kasi yoyote katika hilo kunaweza kuleta athari kwa ulimwengu mzima.
Elimu ya muda mrefu
Hujo Singapore ni mojawapo ya jamii zinazozeeka kwa kasi zaidi duniani.
Ili kusaidia wafanyakazi kukabiliana na changamoto za idadi ya watu wanaozeeka, serikali imewekeza katika mipango ya kujifunza kwa muda mrefu.
Vyuo vikuu vingine hutoa kozi zao zinazohusiana na tasnia iliyochaguliwa na wahitimu kwa hadi miaka 20 kutoka wakati wa kuhitimu na zingine hutoa mikopo kwa wahitimu ili kulipa ada kwenye kozi zinazohusiana na ujuzi unaoibuka, kulingana na benki ya Dunia.
Raia wa Singapore pia wanaweza kutumia mpango wa malipo ya mwaka wa bima ya maisha marefu, ambayo huwapa malipo ya kila mwezi hadi mwisho wa maisha yao, kupunguza hatari za kuishi kwa rasilimali zao za kustaafu.
"Haijalishi unaishi muda gani, kamwe hupaswi kuwa na wasiwasi," inadai serikali. Inafadhiliwa kupitia michango ya kila mwezi ya lazima kwa akaunti ya mtu na hutoa malipo ya kila mwezi wakati wa uzee mradi tu mmiliki wa sera aishi.