Mataifa saba yenye matatizo ya idadi kubwa na ndogo ya watu duniani

Utafiti mkubwa uliochapishwa katika jariuda la kitabibu -Lancet unasema kuwa kushuka kwa viwango vya uwezo wa uzazi kunamaanisha kuwa kila nchi inaweza kukabiliwa na kupungua kwa idadi ya watu ifikiapo mwishoni mwa karne, na umetahadharisha kuwa kutakuwa na athari za kushangaza kwa jamii.

Tunaangalia mataifa yanayokabiliwa na mabadiliko makubwa na ya haraka ya idadi ya watu - na jinsi yanavyoshughulikia tatizo.

Japan

Idadi ya watu nchini Japan itapungua kwa zaidi ya nusu , kutoka idadi kubwa ya watu milioni 128 iliyorekodiwa mwaka 2017 hadi chini ya watu milioni 58 itakapofika mwishoni mwa karne, wamebashiri watafiti walioandika matokeo ya utafiti wao katika jarida la Lancet.

Japan ina idadi kubwa zaidi ya watu wenye umri mkubwa zaidi duniani na kiwango cha juu cha watu wenye umri wa wa miaka zaidi ya 100.

Hii imeliweka taifa hilo katika hali ngumu ya kukosa nguvu kazi na tatizo hili linatarajiwa kuwa baya zaidi.

Maafisa wanakadiria kuwa watu wazima watakua ni zaidi ya 35% ya idadi ya watu ifikapo mwaka 2040.

Hii , pamoja na kiwango cha chini cha uwezo wa kuzaa cha 1.4 cha uzazi cha kila mwanamke, inamaanisha kuwa idadi ya watu watakaokua na uwezo wa kujaza nafasi za kazi katika nchi inapungua.

Nchi zinahitaji kuwa na kiwango cha uwezo wa kuzaa wa takriban watoto 2.1 ili kuimarisha idadi ya watu wanaoishi kwa sasa.

Huku Japan kwa kawaida imekua ikihofia uhamiaji, miaka ya hivi karibuni imelegeza sheria za uhamiaji ili kukabiliana na tatizo hilo.

Hatahivyo, kumekuwa na ripoti nyingi zilizosambaa juu ya unyonyaji dhidi ya wafanyakazi wahamiaji .

Italia

Zaidi ya nusu ya Idadi ya watu nchini Italia pia inatarajiwa kupungua kutoka watu milioni 61 mwaka 2017 hadi watu milioni 28 kufikia mwishoni mwa karne, kwa mujibu wa utafiti wa Lancet.

Sawa na Japan, Italia inafahamika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri wa wazee. Zaidi ya 23% ya watu huko wakiwa na umri wa miaka 65 mwaka 2019, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya dunia.

Mwaka 2015, serikali alianzisha kampeni ya kutoa malipo ya €800 (£725) kwa wanandoa ili kuwashawishi kuzaa kwa ajili ya kuinua kiwango cha uzazi nchini humo

Hatahivyo, bado Italia inasalia kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya chini vya idadi ya watu katika Muungano wa Ulaya.

Nchi hiyo pia ilishuhudia viwango vya juu vya watu walioihama. Takriban watu 157,000 waliihama mwaka 2018, , kulingana na data za taifa hilo.

Miji kadhaa imeanzisha mifumo yake ya kujaribu kuinua kiwango cha idadi ya watu na chumi zake . hii ni pamoja na kuuza nyumba kwa €1 tu au hata kuwalipa watu kuishi katika maeneo yenye idadi ndogo ya watu - pale wanapoanzisha biashara.

Miji ambayo watu wake wanapungua nchini Uhispania, ambayo pia ilikadiria kushuhudia nusu ya watu wake wakipungua imeanzisha mifumo ya aina hiyo

China

Mwaka 1979, China f ilianzisha sera yake maarufu yenye utata ya mtoto mmoja ili kujaribu kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu huku kukiwa na hofu ya athari zinazoweza kutokea katika mipango yake ya ukuaji wa uchumi.

Hii leo nch hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani inakabiliwa na suala la kushuka kwa viwango vya watu wanaozaa.

Utafiri wa Lancet unabashiri kwamba idadi ya watu nchini China itaongezeka kwa kiwango cha juu cha watu bilioni 1.4 katika kipindi cha miaka minne, kabla ya kupungua hadi milioni 732 itakapofika mwaka 2100.

Data rasmi zinaonyesha kuwa kiwango cha uzazi kilishuka hadi chini kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miaka 70 mwaka 2019.

Baadhi wanahofu kuwa "muda wa bomu la idadi ya watu ", ambapo kutakua na idadi ndogo ya watu wenye umri wa kufanya kazi ambao watahitaji kuisaidia idadi kubwa ya wazee watakaokuwa wamestaafu. Ikiwa ni mojawapo ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, hii itakua na athari kwa dunia.

Hofu juu ya idadi ya watu wanaozeeka nchini Uchina iliifanya serikali kusitisha sera ya mtoto mmoja mwaka 2015, na kuwaruhusu watu kuzaa watoto wawili.

Lakini japo mabadiliko hayo yaliongeza kwa muda mfupi viwango vya uzazi , yalishindwa kurejesha ongezeko la muda mrefu la idadi ya watu kama ilivyokua awali.

Sera ya mtoto mmoja imekua ikilaumiwa kwa kusababisha kutokuwepo kwa uwiano wa kijinsia, ambapo wanaume bado ni wengi kuliko wanawake kwa zaidi ya watu milioni 30 kulingana na data za mwaka 2019. Hii kwa sehemu moja inatokana na baadhi ya wanandoa/ wapenzi kuchagua kutoa mimba za watoto wa jinsia wasiyoitaka.

Wataalamu pia wanaema kwamba kulegezwa kwa sheria hakukwenda sambamba na msaada wa nyongeza kwa familia, ikimaanisha kwamba watu wengi hawakuwa na uwezo wa kulea zaidi ya mtoto mmoja.

Iran

Iran pia inatarajia kushuhudia idadi yake ya watu kupungua kwa kiasi kubwa kufikia mwisho wa karne.

Nchi hiyo ilishuhudia ongezeko kubwa sana la watu baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 , lakini ikatekeleza sera ya udhibiti wa uzazi.

Mwezi uliopita, Wizara ya afya ilionya kwamba ongezeko la idadi ya watu limeshuka hadi chini ya 1% katika kipindi cha mwaka mmoja. Bila hatua, ilisema iwapo hatua hazitachukuliwa basi Iran itakuwa ni moja ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wazee katika miaka 30 ijayo.

Shirika la habari la taifa hilo Irna limeripoti kwamba ndoa na watoto ndani ya ndoa pia vimepungua , kwa sehemu kubwa kutokana na hali ngumu ya uchumi.

Katika juhudi za kuinua idadi ya watu wake, Iran iliamua mwezi uliopita kwamba wanaume hawatafanyiwa tena upasuaji wa kufunga uzazi(vasectomies) katika vituo vya serikali na dawa za kuzuwia mimba (contraceptives) zitatolewa tu kwa wanawake wanaoweza kuwa na hatari za kiafya.

Brazil

Brazil imeshuhudia kupungua kwa viwango vya uwezo wa kuzaa kwa miaka 40 iliyopita, kutoka karibu uwezo wa wastani wa watoto 6.3 kwa kila mwanamme mwaka 1960 hadi wastani wa 1.7 kwa makadirio ya hivi karibuni zaidi.

Utafiti wa Lancet unabashiri kwamba idadi ya watu wa Brazil itapungua kutoka watu milioni 211 kulingana na hesabu ya mwaka 2017 hadi chini ya watu milioni 164 mwaka 2100.

Utafiti wa mwaka 2012 ulisema kuwa tamthilia zinazoonyesha familia zenye watu wachache zinachangia kushusha viwango vya uzazi katika taifa lenye hilo wafuasi wengi wa Kikatoliki.

Huku viwango vya jumla vya uzazi vikipungua , Brazil inaendesha kampeni kubwa ya kuzuwia mimba za vijana wadogo, ikifungua kampeni iliyoiita "tarehe kwanza, mimba baadae".

" Tunahitaji kupunguza idadi. Tunadiriki kusema tunakwenda kuzungumzia juu ya kuchelewa kuanza mahusiano ya kingono ," Damares Alves, waziri wa wanawake, familia na haki za binadamu wa Brazil, aliiambia BBC mapema mwaka huu.

India

India Inatarajia kuipita China kama nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani ifikapo mwaka 2100, kulingana na utafiti mpya.

Hii ni pamoja na licha ya ukweli kwamba idadi iliyopo sasa itapungua kutoka bilioni 1.3 billion mwaka 2017 hadi chini ya bilioni 1.1 mwishoni mwa karne ,watafiti wanasema.

Kiwango cha uzazi katika nchi hiyo kwa sasa kiko katika wastani wa watoto 2.24, chini kutoka watoto 5.91 waliokua wakizaliwa hadi mwaka 1960.

Huku nchi nyingine zikijaribu kushawishi watu kuongeza viwango cha kuzaa, Waziri Mkuu Narendra Modi amewatolea wito watu kuwa na familia ndogo.

"Kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu kutasababisha matatizo mengi kwa kizazi chetu kijacho. Lakini kuna baadhi ya watu ambao wameacha kufikiria, kabla ya kumleta mtoto duniani, iwapo wanaweza kumpa haki mtoto na kumpa chochote anachokitaka .

"Wana familia ndoho na kuelezea upendo wao kwa taifa lao. Tujifunze kutoka kwao. Kuna haja ya kuielewesha jamii ," alisema katika hotuba yake mwaka jana.

Nigeria

Nigeria na nchi nyingine za Afrika zinabashiriwa kinyume kabisa na mataifa yaliyotajwa hapo awali juu ya kupungua kwa idadi ya watu wake.

Kwa mujibu wa utafiti mpya wa jarida la Lancet , idadi ya watu katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la sahara inatarajiwa kuongezeka mara tatu ya idadi iliyopo sasa na kufikia zaidi ya watu bilioni tatu tifikapo mwaka 2100.

Nigeria itakua ni nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, ikitarajiwa kuwa na watu milioni 791, inasema.

Utafiti mpya unakadiria kuwa Nigeria itakuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wenye umri wa kufanya kazi duniani ifikapo mwaka 2100 na kushuhudia kuongezeka kwa pato la ndani ya nchi-GDP.

Lakini kasi ya ongezeko la idadi ya watu inaliweka taifa hilo katika tatizo la miundo mbinu na mifumo ya jamii, na maafisa wa Nigeria wamekwishazungumzia juu ya kujaribu kupunguza ongezeko la idadi ya watu nchini humo.

Katika mahojiano na BBC mwaka 2018, Waziri wa fedha wa Nigeria Zainab Ahmed alisema kuwa kuna haja ya kuwepo kwa mazungumzo juu ya kiwango cha uzazi ambacho ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi duniani.

" Tuna familia nyingi sana ambazo hata haziwezi kuwalisha watoto walionao, ukiacha huduma nzuri za matibabu au hata kuwapatia watoto elimu bora, kwa hiyo ni lazima tuzungumzie mambo haya ," alisema.