Miji mitano bora inayoifanya dunia kuwa mahali pazuri

Chanzo cha picha, xbrchx/Getty Images
- Author, Amanda Ruggeri
- Nafasi, BBC
Taasisi ya Global Destination Sustainability Index (GDSI), hufichua miji ambayo inajikita kuelekea dunia ya baadaye yenye kuzalisha kiasi kidogo cha gesi ya kaboni.
Mabadiliko ya tabia nchi, wataalamu wanaonya yanaweza kusababisha joto kali, bahari kupanda juu na upotevu wa karibu miamba yote ya matumbawe duniani.
Orodha ya GDSI inazingatia mambo 69, yakiwemo viwango vya kuchakata taka, uchafuzi wa hewa, idadi ya njia za baiskeli na asilimia ya vyumba vya hoteli ambavyo vimeidhinishwa kuwa ni rafiki kwa mazingira.
Gothenburg, Sweden
Jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini Sweden limeshika nafasi ya kwanza katika fahirisi hiyo ya kila mwaka kuanzia 2016-2021.
Lilitajwa na Lonely Planet kama jiji bora zaidi ulimwenguni 2021; na mwaka 2022, lilitajwa kuwa moja ya miji 100 ya Umoja wa Ulaya ambayo yanapanga kutozalisha hewa chafu ifikapo 2030.
Kuna njia nyingi za kuendesha baiskeli na watu wengi hufanya hivyo. Magari ya umeme ni mengi na maeneno ya kuchajia magari hayo.
Asilimia 95 ya usafiri wa umma wa jiji hilo unatumia nishati mbadala, kama vile mabasi ya umeme. Uwanja wake wa ndege umeidhinishwa kuwa mojawapo ya viwanja vya ndege vinavyopambana na hewa chafu. Uwanja huo umejitolea kufuatilia na kupunguza utoaji wa kaboni.
Oslo, Norway

Chanzo cha picha, Roland Magnusson/Getty Images)
Jiji la pili kwenye orodha hiyo - Oslo, lilipewa jina rasmi la Mji Mkuu wa Kijani wa Ulaya mwaka 2019. Bila kusahau Oslo, ni mji mkuu wa Norway, pia.
Tembea Oslo, kwa upande wa usafiri, jiji lina vituo 270 vya baiskeli za jiji, vituo 5,000 vya kuchaji magari ya umeme na kuna skuta za umeme.
Mji huu ni wa kijani. 63% ni miti. 9% nyingine imeundwa na maeneo ya kijani kibichi na bustani za jiji.
Bodi ya utalii ya jiji hilo imeandaa kozi ya mazingira endelevu kwa sekta ya usafiri na utalii, yenye mada kama vile kupunguza taka na kupunguza kelele.
Glasgow, Scotland

Chanzo cha picha, Richard Johnson/Getty Images
Jina la Glasgow lina urithi wake wa mazingira. Takribani miaka 1,500 baada ya kuanzishwa kwake, jiji hilo la Scotland linashika nafasi ya juu zaidi ya jiji lolote nchini Uingereza na huingia katika 10 bora za GDSI kila mwaka tangu 2016.
Mwaka 2023, kwa mfano, liliweka eneo la uzalishaji wa chini wa hewa chafu, kwa kuzuia magari kuingia katikati ili kupunguza uchafuzi wa hewa.
Vituo vya kuchaji magari ya umeme vimejengwa, taa za barabarani za kisasa zinazozibiti mwanga zimewekwa, na pia kumekuwa na jitihada kuweka baiskeli za kukodisha na njia mpya za baiskeli.
Glasgow pia ina sifa ya jiji la kijani kibichi. Katikati ya Glasgow, kuna bustani nyingi (mji una zaidi ya bustani 90 kwa ujumla).
Bordeaux, Ufaransa

Chanzo cha picha, Lee Sie/Picha za Getty
Bordeaux inajuulikana kwa usanifu wake mzuri wa majengo. Lakini kuna sababu nyingine ya kupenda jiji hilo la Ufaransa:
Pamoja na kuorodheshwa katika 10 bora GDSI, Bordeaux ni mji wa tatu wa mujibu wa orodha ya TripAdvisor ya miji inayotunza mazingira.
Tembea kuzunguka jiji, juhudi za kutunza mazingira ziko kila mahali. Jiji linaweza kupitika kwa baiskeli, mabasi ya umeme, treni za umeme za katikati ya jiji na hata meli.
Kuna migahawa kila eneo la mji na maduka ya nguo za mitumba. Takriban robo tatu ya mashamba ya mizabibu ya Bordeaux na theluthi moja ya makampuni yake ya utalii yameidhinishwa katika orodha ya watunza mazingira.
Kulingana na Olivier Occelli, mkurugenzi wa ofisi ya utalii ya Bordeaux. Sekta ya utalii inataka 80% ya wadau wake, hoteli hadi mashirika ya watalii, wawe wameidhinishwa ni watunza mazingira ifikapo 2026.
Goyang, Korea Kusini

Chanzo cha picha, Joseph Dobson/Alamy
Mwaka 2017, Goyang, iliyoko nje kidogo ya Seoul, lilikuwa jiji la kwanza nchini Korea Kusini kuingia kwenye orodha ya GDSI.
Imekuwa ikipanda viwango vya GDSI tangu wakati huo. Jiji hilo hukusanya maji ya mvua kwa ajili vyoo, mabwawa na bustani. Jiji lenyewe pia lina bustani za kupumzikia 68 na njia za kuendesha baiskeli.
Zaidi ya hekta 1,000 za jiji hilo ni kijani na buluu (bustani na maji) kwa kila watu 100,000, na kilomita 424 ya njia za baiskeli.
"Ni jiji unaloweza kuishi ambapo maeneo ya vijijini na mijini yanawiana vyema, na jiji linajivunia sera nzuri za kutunza mazingira," anasema mkurugenzi wa Goyang Convention and Visitors Bureau, Peter Lee.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












