Kwa nini watu wengi zaidi wanaishi hadi miaka 100 kuliko hapo awali?

Jamaa wa Josefa Maria da Conceicao waligundua kuna kitu hakiko sawa wakati alipoacha kuulizia sigara yake ya kila siku mapema mwaka huu. 

Ilifanyika mara tu baada ya mfanyakazi huyo wa shambani aliyestaafu kutoka Brazili kusherehekea kile ambacho familia yake inasema ilikuwa siku yake ya kuzaliwa ya 120.

"Mama yangu amevuta sigara maisha yake yote," anasema Cicera, mmoja wa watoto wanne wa Josefa waliobaki. Joseph hapo awali alikuwa na 22.

"Umri wake uliposonga, tulijaribu kumfanya aache, lakini mama kila mara alitishia kununua sigara mwenyewe."

Jamaa sasa wanasema Josefa hana nguvu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, alipojipatia umaarufu nchini mwake baada ya kugunduliwa na wahudumu wa televisheni nchini humo kama "mwanamke mzee zaidi duniani".

Kitambulisho cha Josefa kinaonyesha kuwa alizaliwa tarehe 7 Februari 1902. Cha kusikitisha ni kwamba jitihada yake ya kutaka hadhi yake kutambuliwa na Guinness World Records haikufaulu.

Rekodi hiyo kwa sasa inashikiliwa na mzee mpya aliye hai, Lucile Randon, mwanamke wa Ufaransa na mtawa anayejulikana kama Sister Andre, mwenye umri wa miaka 118.

Miongoni mwa wanaume, anayeshikilia rekodi ni Juan Vicente Mora wa Venezuela, mwenye umri wa miaka 113.

Idadi ya wazee inakaribia milioni moja

Kitengo cha Idadi ya Watu cha Umoja wa Mataifa kinakadiria kuwa zaidi ya watu 621,000 wenye umri wa miaka 100 walikuwa wakiishi duniani mwaka wa 2021.

Idadi hiyo inatarajiwa kufikia milioni moja ifikapo mwisho wa muongo huu.

Mwaka 1990, ni watu 92,000 walikuwa wamefikia hatua hiyo muhimu, ambayo hata wakati huo haikuwa jambo dogo.

Sehemu kubwa ya watu duniani hutarajiwa kufikisha miaka, kwani wastani wa umri wa kuishi duniani unafikia miaka 73.

Hata hivyo taswira hiyo inabadilika sana kutoka nchi moja hadi nyingine.

Mtu wa kawaida Japan, kwa mfano anaishi miaka 85, huku mtu kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati akitarajiwa kuishi miaka 54.

Watu wengi wanaofikia uzee wana uwezekano wa kukumbwa na magonjwa ya kudumu.

"Kuishi muda mrefu sio sawa na kuishi vizuri," Janet Lord, profesa wa Biolojia ya katika Chuo Kikuu cha Birmingham, nchini Uingereza, anasema.

Profesa Lord anaeleza kuwa kwa wastani, wanaume hutumia miaka yao 16 ya mwisho kushughulika na magonjwa kuanzia kisukari hadi matatizo ya akili - kwa wanawake, takwimu inaonyesha ni miaka 19.

Je, siri ya kuishi zaidi ya miaka 100 ni gani?

Kuishi zaidi ya miaka 100 ni ngumu zaidi. Nchini Marekani, utafiti wa muda mrefu wa Chuo Kikuu cha Boston umekadiria kuwa ni Mmarekani 1 tu kati ya milioni 5 anayefikia hatua hiyo ya maisha- akiishi angalau 110.

Lakini wakati watafiti walihesabu karibu watu 60 hadi 70 wenye umri huo mnamo 2010, kufikia 2017 idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi 150.

"Supercentenarians" kwa kawaida huvutia usikivu mwingi kutoka kwa wanasayansi wanaojikita katika masuala ya kuzeeka kwa binadamu.

"Watu hao wanakiuka kile kinachowakabili watu wengi uzeeni. Na hatuna uhakika hali hiyo inatokana na nini," Profesa Lord anaongeza.

Pamoja na maisha marefu, watu wenye umri mkubwa zaidi wanasifika kwa kuwa na afya nzuri kwa umri wao.

Josefa Maria, kwa mfano, hahitaji dawa za kawaida na bado anakula nyama nyekundu na peremende, kulingana na familia yake.

Ijapokuwa kumbukumbu zake hazieleweki, na uwezo wake wa kuona umeharibika, Cicera anakiri kwamba wakati fulani bado anachanganyikiwa na hali ya mama yake.

"Hawezi kutembea sana kama zamani na inabidi tumbebe na kumbadilisha nepi kama mtoto.

Lakini bado nashangaa kuwa mama ameishi kwa muda mrefu kwa mtu ambaye alivuta sigara tangu utotoni na ambaye alikuwa na miongo kadhaa ya maisha. Ni kazi ngumu," mzee wa miaka 76 anasema.

Kinachowatatanisha wataalam wa umri hata zaidi ni kwamba baadhi ya watu wanaofikisha umri wa miaka 100 na zaidi hawana mazoea bora ya afya.