Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kifuatacho kati ya Marekani na Iran kinaweza kubadilisha historia
- Author, Lyse Doucet
- Nafasi, Mwandishi mkuu wa kimataifa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kwa miongo kadhaa, Marekani na Iran zimekwepa kuvuka mstari mwekundu wa makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi.
Rais mmoja baada ya mwingine wa Marekani walisita kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hofu ya kuitumbukiza Marekani katika vita hatari zaidi Mashariki ya Kati kuliko vyote.
Sasa, kamanda mkuu, ambaye aliahidi kuwa rais wa amani, Donald Trump amevuka mstari huo na kufanya mashambulizi ya moja kwa moja ya kijeshi kwenye maeneo ya nyuklia ya Tehran.
Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei mwenye umri wa miaka 86, ambaye sasa anaripotiwa kujificha kwenye chumba cha chini ya ardhi, ametumia takribani miongo minne kufanya maamuzi ya tahadhari dhidi ya adui yake huyo mwenye nguvu ili kuulinda utawala wake wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ikiwa hatojibu, atapoteza heshima; ikiwa atajibu kwa nguvu, anaweza kupoteza kila kitu.
"Maamuzi yanayofuata ya Khamenei yatakuwa muhimu sio tu kwa maisha yake mwenyewe, lakini kwa historia pia," anasema Sanam Vakil, Mkurugenzi wa kitengo cha Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya fikra tunduizi, Chatham House.
"Iran haitaki vita"
Katika siku kumi zilizopita, mashambulizi makali ya Israel yamesababisha uharibifu mkubwa kwa makamanda na vifaa vya kijeshi vya Iran kuliko vita vyake vya miaka minane na Iraq.
Mashambulizi ya Israel yamewaondoa wakuu wengi wa vikosi vya usalama vya Iran pamoja na wanasayansi wakuu wa nyuklia. Kuingia kwa Marekani katika mzozo huu kumeongeza shinikizo.
Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), lililoanzishwa baada ya mapinduzi ya Iran ya 1979, limeeleza litalipiza kisasi dhidi ya Marekani na kuiacha katika "majuto ya kudumu."
Lakini nyuma ya vita vikali vya maneno kuna mahesabu makubwa ili kuepusha hesabu mbaya.
"Hivi si vita ambavyo Iran inavitaka," anasema Hamidreza Aziz, kutoka taasisi ya utafiti ya Mashariki ya Kati. "Lakini kuna hoja za wafuasi wa serikali, wanaosema, bila kujali kiwango cha uharibifu ambacho Marekani imesababisha, taswira ya Iran kama nchi yenye nguvu [na] mamlaka kikanda, imetikiswa kwa kiasi kikubwa na inapaswa kujibu."
Hata hivyo, jibu lolote ni hatari. Shambulio la moja kwa moja katika mojawapo ya kambi 20 za Marekani katika Mashariki ya Kati, au dhidi ya wanajeshi zaidi ya 40,000 wa Marekani, huenda likasababisha Marekani kulipiza kisasi.
Kuufunga Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia ya kimkakati ya baharini kwa theluthi moja ya mafuta yanayosafirishwa duniani, kunaweza pia kuwaudhi washirika wa nchi za Kiarabu, pamoja na China, mteja mkuu wa mafuta ya Iran.
Wanajeshi wa majini wa nchi za Magharibi pia wanaweza kupelekwa ili kulinda mlango huu, kuepusha majanga makubwa ya kiuchumi.
Na kile ambacho Iran ilikiona kama "ulinzi wake," yaani mtandao wa washirika katika eneo hilo, wote wamedhoofishwa au kuangamizwa na mashambulizi na mauaji ya Israel katika kipindi cha miezi 20 iliyopita.
Haijabainika ikiwa kuna njia kwa Iran kulipiza kisasi, bila kuamsha hasira ya Marekani.
Uhusiano huu wa mbaya ulipitia majaribu mara moja huko nyuma. Miaka mitano iliyopita, Rais Trump aliamuru kuuawa kwa kamanda wa IRGC, Qasem Soleimani kwa shambulio la ndege isiyo na rubani mjini Baghdad, wengi walihofia hali ingekuwa mbaya.
Lakini Iran ilifanya shambulizi baada ya kutoa taarifa kwa simu kupitia maafisa wa Iraq, na ikalenga sehemu za kambi za Marekani na kuepusha kuwauwa wafanyakazi wa Marekani au kusababisha uharibifu mkubwa.
Lakini wakati huu mambo ni makubwa zaidi.
"Marekani amesaliti diplomasia"
Rais Trump, ambaye mara kwa mara alielezea upendeleo wake wa "kufanya makubaliano na Iran" badala ya "kuishambulia" sasa anaonekana kuwa pamoja na Israel.
Alielezea Iran kama "mnyanyasaji wa Mashariki ya Kati," aliyedhamiria kuunda bomu la nyuklia - hitimisho ambalo halijafikiwa katika tathmini za awali za kijasusi za Marekani.
Timu za kijasusi sasa zinachambua kwa kina matokeo ya kile Pentagon inachosema ni "shambulizi kubwa zaidi la ndege za B-2 katika historia ya Marekani." Limesababisha "uharibifu mkubwa" katika maeneo makuu ya nyuklia ya Iran huko Natanz, Isfahan na Fordow.
Ni makombora ya Marekani pekee (bunker busting), yenye uwezo wa kupenya katika kituo cha Fordow kilicho ndani kabisa ya mlima.
Rais Trump sasa anaitaka Iran "kusaka amani."
Lakini Iran sasa inaiona njia ya kidiplomasia ya Marekani kama kujisalimisha. Mjini Geneva siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alikutana na viongozi wenzake wa Ulaya, ujumbe ulitolewa ni kwamba Washington inatarajia Tehran kupunguza urutubishaji wake wa uranium hadi sifuri.
Ni matakwa ambayo Iran inayakataa na kusema ni ukiukaji wa haki yake ya kurutubisha uranium, kama sehemu ya mpango wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia.
Iran inaamini juhudi za kidiplomasia za Rais Trump, ikiwa ni pamoja na duru tano za mazungumzo ambayo kimsingi si ya moja kwa moja yaliyofanywa na mjumbe wake maalum Steve Witkoff, kuwa ni udanganyifu.
Kipi kifuatacho kwa Iran?
Israel ilianzisha mashambulizi ya kijeshi siku mbili kabla ya duru ya sita ya mazungumzo mjini Muscat. Marekani iliingia vitani siku mbili baada ya Rais Trump kusema anataka kuruhusu wiki mbili kutoa nafasi ya diplomasia.
Sasa Iran inasema haitarejea kwenye meza ya mazungumzo wakati mabomu ya Israel na Marekani bado yanaanguka.
"Si Iran, bali ni Marekani ndio ambayo ilisaliti diplomasia," amesema Araghchi katika mkutano na waandishi wa habari huko Istanbul. Wakati alipokutana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 57 za Jumuiya ya Kiislam ambao walilaani "uchokozi wa Israel" na kuelezea "wasiwasi wao kuhusu mashambulizi hayo."
Iran pia imelezea mashambulizi dhidi yake kuwa yanakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kugusia maonyo kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwamba vifaa vya nyuklia kamwe visishambuliwe, "bila kujali mazingira yoyote."
Viongozi wa Ulaya pia wanatoa wito wa kupunguzwa kwa mashambulizi na kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran kwa upatanishi, na sio makombora.
Lakini pia wanasisitiza kuwa Iran haiwezi kuruhusiwa kupata bomu la nyuklia. Wanachukulia urutubishaji wa Tehran wa asilimia 60 ya uranium, kabla ya kiwango cha asilimia 90 cha silaha, kama dalili ya kutisha kwa nia yake.
"Iran inaweza kudogosha uharibifu katika maeneo yake na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia umenusurika mashambulizi haya," anasema Ellie Geranmayeh, naibu mkuu wa kitengo cha Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni.
"Marekani inaweza kutia uchumvi uharibifu, ili Trump aweze kudai ushindi wa kijeshi bila kuingizwa kwenye mashmbulizi zaidi."
Lakini Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu, ataendelea kuishambulia Iran ili kufanya uharibifu mkubwa zaidi, na kusababisha Iran kulipiza.
Na kiongozi wa Marekani pia anakabiliwa na shinikizo nyumbani kutoka kwa wabunge ambao wanasema alitenda bila kibali cha bunge, na wafuasi wanaoamini kuwa amevunja ahadi yake ya kuizuia Marekani isiingie kwenye vita.
Akili za watoa maamuzi wenye msimamo mkali wa Irani, zitakuwa ni kuzuia mashambulizi zaidi huku wakijaribu kuzuia kulengwa wenyewe.
"Jambo la ajabu," anaonya Bi Geranmayeh. "Ingawa Trump amejaribu kuondoa tishio la nyuklia kutoka Iran, sasa ameufanya uwezekano kuwa mkubwa zaidi kwa Iran kuwa taifa la nyuklia."